WAKAMATWA NA SHEHENA YA BUNDUKI NA NYARA ZA SERIKALI

WAKAZI tisa Wilaya ya Handeni na Kilindi mkoani Tanga wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka kwa kosa la kukutwa na bunduki zaidi ya 25 na nyara nyingine za Serikali kinyume cha sheria.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, Nzagalila Kikwelele mbele yaHakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Handeni, Patrick Maligana kuwa, Oktoba 11, mwaka huu katika nyakati tofauti wilayani Handeni na Kilindi, Jeshi la Polisi, maofisa wanyamapori na misitu walifanya msako wa kutafuta wawindaji haramu katika maeneo hayo na kufanikiwa kuwakama watu hao.

Alidai kuwa, katika msako huo watu tisa walikamatwa wakiwa na nyara mbalimbali za Serikali ikiwemo ngozi za pongo, tandala na nyati, pembe za nyati, meno matano ya ngiri na vifaa vya kutengenezea magobore, pia walikamata magobore zaidi ya 25 yakiwa katika makazi yao.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa, hadi sasa upelelezi kuhusu watu hao umekamilika na kwamba, mahakama inaweza kuendelea na mchakato wa usikilizaji wa shtaka hilo.

Akitoa hukumu kwa mtuhumiwa wa kwanza, Iddi Abdalah (51), Hakimu wa mahakama hiyo, Patrick Maligana alidai kuwa, anamtia hatiani kwa kosa la kukutwa na ngozi tatu za tandala zenye thamaniya zaidi sh. milioni 25 na bunduki aina ya gobore ambazo ni nyara za Serikali.

Alipotakiwa kujitetea kabla ya kupewa hukumu, mtuhumiwa alidaikuwa, anaomba kupunguziwa adhabu kwani ana watoto watano wadogo na kwamba, hawana mlezi.

Baada ya utetezi huo, hakimu alisema anamhukumu kwenda jela miaka 20 ama alipe faini ya zaidi ya sh. milioni 125, ambapo mtuhumiwa alisema hana fedha hizo. Wengine waliohukumiwa ni Muya Kidundo (63), ambaye amehukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la kukutwa na meno matano ya ngiri na ngozi ya swala.

Mwingine ni mkazi wa Negero, Bakari Mwikalo (50), ambaye alihukumiwa miaka saba jela kwa kosa la kukutwa na silaha bila kuwa na kibali. Pia, alimhukumu Selemani Mzimba (45), kwenda jela miaka sita kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.


HakimuMaligana alimuachia Hamza Msami (70), kutokana mazingira ya kosa lake kuwa dogo na umri wake mkubwa, kwani hakuisumbua mahakama katika kujua ukweli wa kesi yake na kwamba, watuhumiwa wengine wapo nje dhamana.

Watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika operesheni okoa maliasili inayoendeshwa nchini koteambapo katika Wilaya ya Handeni na Kilindi, watu tisa walikamatwa.


Chanzo:Jambo leo