KATAVI KUNUFAIKA NA NYUMBA ZA NHC

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limeingiza sokoni nyumba 406 katiya 2,000 zilizopo kwenye awamu ya kwanza ya nyumba za gharama nafuu huku likihadharisha umma kuhusu uwepo wa matapeli wanaotumia jina lao kama madalalikuwarubuni watu wawape fedha ili wawapatie nyumba kwa urahisi.

NHC imesema hakuna dalali katika uuzaji wa nyumba hizo zinazoanza kuuzwa leo katika mikoa 10 kati ya 11 inayohusika na awamu hii kupitia kampeni iitwayo "Nyumba Yangu-Maisha Yangu".

Meneja wa Biashara na Maendeleowa NHC, David Shambwe aliyasema hayo na kutoa hadhari hiyo jana, Dar es Salaam alipozindua uuzaji wa nyumba hizo 406 za awali ambazo gharama ya chini ya nyumba ni Sh milioni 33 hadi Sh milioni 49 bila Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Akifafanua, alisema katika mradi wa uuzaji nyumba Kibada Kigamboni shirika hilo lilitangaza kuzuia wananchi wasitumie madalali.

Alisema mhitaji afike ofisi za NHC matawi yote nchini ama kutumia mtandao wao au simu namba 0754444333 kwa maelezo zaidi.

Alisema ili kuondoa watu kujimilikisha, NHC itauza nyumba moja kwa mtu mmoja katika mkoa wowote husika na ikiwa watu wa familia moja wana uwezo wa kununua nyumba zaidi ya moja kwa kila mtu, hawazuiwi.

Alitaja maeneo zilipo nyumba hizo na mikoa kwenye mabano ni Bombambili (Geita), Ilembo na Mlele (Katavi), Kongwa (Dodoma) na Mkinga (Tanga).

Mengine ni Mkozo mkoani Ruvuma, Mlole (Kigoma), Mrara (Manyara), Mtanda (Lindi), Mvomero (Morogoro) na Unyankumi(Singida).

Kwa mujibu wa Shambwe kila Mtanzania anaruhusiwa kununua nyumba moja kati ya hizo kwa kulipia asilimia 10 ya gharama kupitia akaunti namba 01500250887500 iliyopo benki ya CRDB Kariakoo na kutakiwa kukamilisha malipo ya nyumba husika ndani ya siku 90 kupitia mkopo wa benki zinazoshirikiana na NHC au fedha binafsi.