MABAKI YA MOBUTU SESEKO KUZIKWA DR CONGO

Serikali ya Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo, imesema itahamisha mabaki ya mwili wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko kufuatia makubaliano na familia yake. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya rais wa nchi hiyo, President Joseph Kabila.

Hayati Mobutu alizikwa nchini Morocco, alikofariki mnamo mwaka 1997 baada ya kuondolewa mamlakani kutokana na uasi ulioongozwa na baba yake Rais Joseph Kabila.

Alikuwa mtu aliyechukiwa sana na wengi nchini Congo, lakini nchi hiyo imekumbwa na migogoro tangu alipong'olewa mamlakani.

Hatua ya Kabila inaonekana na wengi kama mpango wake wa kuwapatisha watu wa nchi hiyo.

Kabila alishinda uchaguzi wa mwaka 2007 bila ya pingamizi na anakabiliana na uasi Mashariki mwa nchi.

Rais Kabila ametoa tangazo hilo la kipekee katika hotuba yake kwa bunge ambapo aliahidi kuunda serikali ya pamoja.

''Serikali hii itajumuisha wanachamawa chama tawala na wale wa upinzani pamoja na viongozi kutoka mashirika ya kijamii,'' alisema katikahotuba yake.

Mtaalamu wa maswala ya Afrika Ibrahima Diane anasema kuwa huenda Kabila alishauriana na mwanawe Mobutu, Nzanga Mobutu, kabla ya kutangaza kuwa mabaki ya hayati Mobutu yatazikwa nchini Congo.

Mobutu Sese Seko angali anawakumbuka wengi hasa wafuasi wake wanaoamini kuwa moja ya mambo mazuri aliyoyafanya ni kuunganisha nchi hiyo.

Nzanga Mobutu ni mbunge ambaye sasa ni mshirika wa karibu wa Rais Kabila.

Mobutu Sese Seko alitoroka DR Congo wakati waasi walioongozwa na Laurent Kabila, kuzingira mji mkuu Kinshasa, mnamo mwaka 1997.

Wakosoaji wake wanamtuhumu kwakuwa mkatili na kiongozi mfisadi aliyekandamiza upinzani na kuponda maliasili ya DR Congo.

Pia alitumia mamilioni ya dola kuijengea kasri yake ya Gbadolite, iliyo ndani ya misitu ya DRC ambayo ilifanyiwa msako mkubwa alipotoroka DR Congo.

Aliingia mamlakani kupitia kwa mapinduzi na kuitawala DR Congo, iliyokuwa inajulikana kama Zaire, kwa zaidi ya miaka 30.

Hata hivyo alifariki akiwa na miaka 66 miezi michache tu baada ya kuikimbia nchi yake.