Operesheni hiyo inayoendelea katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita chini ya mkuu wa operesheni za jeshi la polisi Tanzania, naibu Kamishna Simon Sirro, pia imewanasa jumla ya wahamiaji haramu 425, wakiwemo raia wa Burundi 180, Wanyarwanda 149, Waganda 82 na Wakongomani 14 , na kufanya jumla ya wahalifu wa makosa mbalimbali waliokwisha kamatwa kufikia 529 wakiwemo wahusika wa mtandao wa ujambazi wa kutumia silaha katika kipindi cha siku 10.
Kuhusu ng'ombe 103 mali ya Bw. Kalemela George ambao wametaifishwa kwa amri ya mahakama ya wilaya ya Biharamulo kwa kosa la kukutwa ndani ya hifadhi ya taifa ya Burigi na wengine 220 waliokamatwa kwenye hifadhi ya Kimisi wilayani Karagwe, naibu kamishna wapolisi Simon Sirro akatumia wasaa huo kuwaalika wananchi wanaohangaika kutafuta ng'ombe wa kuchinja kuchangamkia soko kwenye maeneo ya operesheni, kwani ng'ombe ni wa kumwaga.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera kanali Fabian Masawe, wakati wa operesheni Kimbunga, mkuu wa wilaya ya Kyelwa kanali mstaafu Issa njuki amesema kwamba vyombo vya ulinzi na usalama ngazi zote vimepewa jukumu la kuwabainisha popote walipo wahamiaji haramu na kisha kukusanywa na kuwekwa sehemu moja na baadaye kuhojiwa ili ambao watabainika si raia warejeshwe kwenye nchi zao wanakotoka.
Chanzo:ITV