WAFARANSA WAWILI WAUWAWA MADAGASCAR KWA KUHUSISHWA NA BIASHARA YA VIUNGO VYA BINADAMU

Raia wawili wa Ufaransa wameuawa nchini Madagascar na watu wenye ghadhabu waliowashuku kwa kufanya biashara haramu ya viungo vya binadamu hasa baada ya mtoto mmoja kupotea.

Mwanamume mmoja mwenyeji alikamatwa baada ya kuhusishwa na kutoweka kwa mtoto huyo siku ya Jumatano katika kisiwa cha Nosy Be,ambacho hutembelewa sana na watalii.

Kundi moja la watu baadaye lilifanya vurugu nje ya kituo cha polisi likiamini kuwa mtu huyo alilipwa kumtoa mtoto huyo viungo vyake vya mwili. Baadaye walianza kuwasaka raia haowafaransa , kwa mujibu wa polisi.

Vurugu hizo zilisababisha vifo vya raia wawili wa kigeni ambao baadaye walisemekana kuwa wafaransa.

Mwandishi wa BBC Tim Healy mjini, Antananarivo, anasema kuwa hakuna mwili wa mtoto umepatikana hata baada ya msako.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa watu hao walimpata na sehemu za mwili wa binadamu kwenye jokofu katika nyumba ambamo raia hao walikuwa wanaishi.

Kisiwa cha Nosy Be ni kitovu cha utalii nchini Madagascar na kimekuwa kikitumiwa kuwavutia watalii wengi nchini humo kufuatia mgogoro wa kisiasa wa miaka mingi.

Kwa mujibu wa taarifa , angalau mtu mmoja aliuawa kwenye ghasia hizo ambazo zilizuka nje ya kituo cha polisi.

Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wanawatupia mawe.

Watu hao baadaye waliteketeza nyumba zilizozingira kituo hicho chapolis kabla ya kuanza msako wa raiahao wafaransa.