WAKATI taifa linaadhimisha miaka 14 ya kifo cha mwasisi wa taifa, na rais wa kwanza wa Tanzania, kizazi kinahitaji kujua Nyerere alikuwa mtu gani na alianzia wapi.
Nia yetu ni kutaka kumuezi na kujikumbusha.
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa mwaka 1922 , katika kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara. Alikuwa mmoja kati ya watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabilala Wazanaki.
Alipokuwa mtoto, Nyerere alichunga mifugo ya babake. Katika umri wa miaka 12, aliingia shule akitembea kilomita 30 hadi katika shule ya msingi ya Mwisenge, iliyoko Musoma Mjini.
Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusoma shule ya wamisionari Wakatoliki iliyoko Tabora. Katika umri wa miaka 20, Nyerere alibatizwa akawa mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.
Kutokana na ujasiri na nia ya kuwa mwelewa wa kila kitu, mapadre wa Kanisa katoliki waliona akili yake na nia yake nzuri ya kutaka kujifunza , wakamsaidia kusoma kozi ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.
Akiwa katika Chuo cha Makerere, Nyerere alianzisha tawi la Umoja wa wanafunzi Watanganyika pia aliamua kujihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya kumaliza masomo yaualimu, Nyerere alirudi Tabora nakuanza kufundisha shule ya sekondari ya Mtakatifu Maria (St.Mary´s). Mwaka 1949 alipata skolashipu ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uskoti / Uingereza , akasoma Shahada ya Uzamili ya historia na uchumi... Kwa hatua hiyo Mwalimu alikuwa mtanzania wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.
Aliporejea Tanganyika kutoka masomoni, Nyerere alifundisha Historia, Kingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu na Dar es Salaam, (siku hizi Pugu Sekondari).
Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika huo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954, alikibadilisha chama cha TAA kwenda katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA.
Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kilikuwa tayari chama cha siasa kinacho ongoza Tanganyika.
Uwezo wa mwalimu uliwashitua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha Nyerere kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.
Aliamua kujiuzulu ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika mapigano ya uhuru.
Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Mkutano wa Baraza la udhamini (Trusteeship council) ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York. Uwezo wake wa kimaongezi na kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.
Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuumwaka 1960. Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na Desemba 9,1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuuwa Tanganyika huru na mwakammoja baadae Nyerere alikuwa raisi wa kwanza wa jamhuri ya Tanganyika.
Nyerere alikuwa kiungo muhimu sana katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964, yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
Hayati Mwalimu Nyerere mnamo Februari 5, 1977, aliongoza chama cha TANU katika tendo la kuungana na chama tawala cha Zanzibar ASP na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa mwenyekiti wake.
Nyerere aliendelea kuongoza Taifa hadi 1985 alipong'atuka na kumwachia nafasi rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi.
Aliendelea kuongoza Chama cha CCM hadi 1990 na kuwa makini na mfuatiliaji huku akionya katika mambo kadhaa katika siasa za Tanzania hadi kifo chake.
Baada ya kustaafu kazi ya ukuu wanchi, Nyerere alikaa muda mwingi kijijini kwake alikozaliwa Butiama akilima shamba lake la mahindi.
Pamoja na hayo, Nyerere alianzisha taasisi yenye jina lake inayojulikana kama "Mwalimu Nyerere Foundation", mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi wa pande mbalimbali za vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.
Mwishoni mwa maisha yake Mwalimu aliishi kama mkulima wa kawaida kijijini kwake Butiama Mwalimu alianza kujisikia vibaya mwezi Augost mwaka 1999, akaanza kupata matibabu ya kila mara, baadae alihamishiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas huko Uingereza. Oktoba 14, 1999 aliaga dunia katika hospitali hiyo ambapo madaktari walisema kuwa alikuwa akisumbuliwa na kansa ya damu (leukemia).
Mafanikio na kasoro
Kitendo kikubwa ambacho Mwalimu alikifanya na dunia inakumbuka ni kuchanganya ardhi ya Zanzibar na Tanganyika ambapo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulizaliwa rasmi na hadi leo upo.
Mengine ni Kujenga umoja wa kitaifa na utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, kushinda ubaguzi wa rangi, kutetea usalama wa taifa katika vitadhidi Nduli Idi Amin Dadaa wa Uganda.
Watu walimuita mwalimu kuwani mwanamapinduzi wa afrika, kiongoizi wa bara nzima kutokana na nia yake ya kutaka kila Mwafrika kuwa huru na kuwa na amani.
Mwalimu pia alifanikiwa kutoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za kusini ya Afrika kama; Zimbabwe {ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola (MPLA) na Msumbiji (Frelimo) Kutofanikiwa kwake Kitu ambacho kilimuumiza mwalimu na kumfanya akose raha mara nyingi ni juu ya kutofanikiwa kwa nia yake ya kuanzisha siasa za Kijamaa.
Siasa zake za ujamaa zilishindwa baada ya mwaka 1976.
Baada ya kuona kuwa uchumi wa Tanzania hautaweza kusimama kwa siasa za kijamaa na kutoweza kuvumilia kuendesha nchi kwa siasa ambazo yeye hakuwa muumini, Nyerere kwa maamuzi yake mwenyewe aliamua kustaafu nafasi ya urais baada ya uchaguzi wa mwaka 1985 na kumwachia usukani rais Mwinyi aliyetawala kwa siasa za uchumi wa soko huria.
Katika hali ya kukubali ukweli, Nyerere alitamka katika tafrija ya kumuaga juu ya siasa yake kiuchumi :
"Nimefeli. Tukubali hivyo."
Alikosolewa pia
Kutokana na hali hiyo na kufikia yeye kukubali kushindwa , Mwalimu Nyerere analaumiwa kwa siasa zake za kiujamaa kuwa zilichelewesha maendeleo ya uchumi wa Tanzania, pamoja na kwamba hata leo kuna makundi ya watanzania kwa mtazamo waoyanazitamani siasa hizo.
Mbali na hayo, kuna makundi ya waislamu wanaomtuhumu kwa kuendesha kwa siri vita dhidi ya uislamu na upendeleo wa elimu na madaraka kwa wakristo. Kutangazwa mwenye HeriKwa taratibu za Kanisa Katoliki,mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu ulianza mwaka 2005,na tayari kanisa hilo kwa kibali rasmi kutoka Roma makao ya Baba Mtakatifu, limeshamtangaza kuwa mwenyeheri.
Kuwa mwenyeheri ni hatua ya kwanza ya kuingia utakatifu. Wakristo wakatoliki wameanzisha sala maalumu na kufanya maombi kwa nia yamaombezi yake ili aweze kutangazwa kuwa mtakatifu. Ibada ya kwanza ilifanyika katika kanisa kuu la Jimbo la Musoma, na kuongozwa na aliyekuwa askofu wa Jimbo hilomarehemu askofu Justine Samba.
Alikuwa mwana michezo Licha ya Kuwa mwalimu na mwanasiasa hususani kiongozi mkuu wanchi, pia Nyerere alikuwa mwanamichezo.
Alianzisha mchezo wa Bao, akiwa Butiama alicheza bao nyumbani kwake na majirani zake, wakati mwingine alipotembelewa na wafuasi wake wa kisiasa alikuwa akishiriki nao kucheza bao.
Kutokana na maisha yake aliyoishi ambayo yalijaa uvumilivu, unyenyekevu na uadilifu bado anakumbukwa na watanzania hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake zakujali utu na ubinadamu.
Ni mmoja wa viongozi wachache wanaokumbukwa kwa kutojilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.
Taifa linamkumbuka kwa hayo na mengine mengi ambayo aliyafanya, ameacha machapisho mengi ambayo pia yamekuwa hazina ya maarifa kwa watanzania.