MTOTO ANYAKULIWA MGONGONI NA FISI

Watu wawili wamefariki dunia mkoani Simiyu katika matukio tofauti akiwamo mtoto wa miezi mitatu aliyenyakuliwa na fisi akiwa mgogoni mwa mama yake.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Simiyu, Gemin Mushy jana alisemakuwa mtoto Ng'wanza Samwel, akiwa amebebwa na mama yake alinyakuliwa na fisi Mei 25, majira ya saa 1;30 jioni katika kijiji cha Ngugunu, Tarafa ya Kisesa wilayani Meatu.

Alisema katika kufuatilia tukio hilo, mabaki ya mtoto huyo yalipatikana mita 200 tu fisi kutoka eneo alilonyakuliwa huku kichwa, kifua, tumbo, mikono na miguu ikiwa haipo.

Katika tukio jingine mpanda baiskeli aliyefahamika kwa jina la Magina Supa(20), mkazi wa Nyaumata mtaa wa Kisiwani wilayani Bariadi, aliuawa kwa kukatwa na kitu chenyencha kali shingoni na bega la kushoto na mtu aliyekuwa amempakiza kama abiria wake.

Akifafanua, Kamanda Mushy alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 26 majira saa 1;00 jioni katika mtaa wa Izunya, kata ya Somanda tarafa ya Ntuzu wilayani Bariadi kwa mtuhumiwa wa mauaji hayo anayedaiwa kuwa abiria wa mpanda baiskeli huyo aliyekuwa anajishughulisha na biashara ya daladala ya baiskeli.

Kamanda huyo alisema kuwa mara baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye hajafahamika na anasakwa baada uhalifu huo alitoroka. Chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI