MGOMBEA URAIS CCM KUJULIKANA JULY 12

Chama cha Mapinduzi(CCM) kimetoaratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku ikionyesha mgombea urais atapatikana Julai 12, mwaka huu baada ya kupitishwa na mkutano mkuu.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar mgombea urais anatarajiwa kupatikana Julai 10, mwaka huu baada ya kupitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, alisema mchakato wa uchukuaji na urudishaji fomu katika nafasi ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajia kuanza Juni 3 hadi Julai 2,mwaka huu saa 10 jioni.

Alisema ndani ya tarehe hizo mgombea atatakiwa kutafuta wadhamini 450 kwenye mikoa 15, mitatu ya Zanzibar na mmoja wapo uwe kati ya Unguja na Pemba, huku Tanzania Bara ikiwa mikoa 12.

Akifafanua zaidi, alisema ongezeko la wadhamini kwa mgombea wa urais kutoka 250 miaka ya nyuma hadi 450 linatokana na ongezeko la mikoa pamoja na wanachama wa CCM.

Aidha, Nape alisema vikao vya mchujo vinatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 8, mwaka huu, ambapo itakaa Kamati ya Usalama na Maadili ikifuatiwa na Kamati Kuu Julai 9 wakati NEC ikitarajiwa kuwa Julai 10, huku Mkutano Mkuu utafanyika Julai 11 hadi 12 mwaka huu.


MASHARTI YA UGOMBEA URAIS
Kuhusu masharti kwa wagombea wa Urais upande wa Tanzania, alisema yameongezeka ikiwa ni pamoja kutafuta wadhamini 450 kwa mwaka huu badala ya 250 kama ilivyokuwa kwa chaguzi zilizopita za mwaka 2005 na 2010.

Alisema mgombea wa urais hatatakiwa kudhaminiwa na mjumbe yeyote wa mkutano mkuu kwa sababu wanashiriki katika mchakato wa kuteua mgombea.

Aliongeza kuwa mwanachama mmoja hataruhusiwa kudhamini zaidi ya mgombea mmoja, pia fomuhiyo itathibitishwa na katibu wa wilaya kama waliodhamini fomu hiyo ni wanachama.

"Hayo ni masharti matatu ya kwanza ya msingi wanatakiwa kuyajua…wajumbe wa mkutano mkuu ni marufuku kumdhamini mgombea, adhaminiwe na wanachama wa kawaida au viongozi ambao hawaingii katika huo mchakato," alisema.

Kwa upande wa Zanzibar, Nape alisema fomu za urais zinatarajiwa kuanza kuchukuliwa Juni 3 na kurudishwa Julai 2, mwaka huu saa 10 jioni.

Alisema ndani siku hizo, mgombea atatakiwa kutafuta wadhamini 250 kwenye mikoa mitatu ya Zanzibar na mmoja uwe Unguja au Pemba.

Alisema vikao vya mchujo wa wagombea vinatarajiwa kuanza Julai 4, mwaka huu kwa Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar ikifuatiwa na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Zanzibar itakayokaa Julai 5, mwaka huu, Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa itafanyika Julai 8, mwaka huu, wakati Kamati Kuu ikikaa Julai 9, mwaka huu na NEC ikikaa Julai 10, mwaka huu.

Alisema CCM inategemea kupata mgombea wa urais wa Zanzibar Julai 10, mwaka huu kwa utaratibu ambao mgombea huyo anapatikana kwa kupitia NEC na si Mkutano Mkuu kama ilivyo kwa mgombea waUrais wa Jamhuri wa Muungono wa Tanzania.


MASHARTI YA UGOMBEA URAIS ZNZ
Nape alitaja masharti ya mgombea wa urais wa Zanzibar kuwa anatakiwa kuwa na wadhamini 250 sharti ambalo lilikuwapo na halijabadilika.

Alisema wajumbe wote wa NEC ambao ndiyo watakaofanya uamuzi hawaruhusiwi kumdhamini mgombea wa urais.

UBUNGE
Kuhusu wagombea ubunge alisema wanatarajiwa kuchukua fomu Julai 15, mwaka huu na kurudisha Julai 19, mwaka huu.

Nape alisema wagombea wa ubunge watafanya mikutano ya kampeni ya kujinadi kwa wanachama kuanzia Julai 20 hadi 31, mwaka huu.

"Ratiba itapangwa kwenye matawi namna ya kuyajumuisha matawi kama ilivyofanyika mwaka 2010, wagombea wataenda kwa wanachama watakuta mkutano umeandaliwa kwa ajili ya kuomba kura," alisema.

Aidha, alisema Agosti Mosi itakuwa ni siku ya kupiga kura ya maoni kwanchi nzima kwa ajili ya kuwapata wagombea ubunge wa CCM, baada ya hapo kutakuwa na vikao vya mchujo kwa ajili ya kuwapata wagombea watakaopambana na wagombea wa vyama vingine.

Hata hivyo, alisema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, uchukuaji fomu na urejeshwaji itakuwa kama michakato ya kwenye ubunge.


VITI MAALUM na WAWAKILISHI

VITI MAALUM
Alisema uchukuaji na urudishaji wa fomu utakuwa kama kwenye ubunge isipokuwa mchakato wa kuwachuja utapitia kwenye vikao vya Jumuiya ya Wanawake (UWT).

UDIWANI
Alisema kwa upande wa udiwani ratiba itakuwa kama ya ubunge.

"Tofauti ni kwamba Tanzania Bara kutakuwa na masanduku mawili yaani ya ubunge na udiwani na Zanzibar kutakuwa na masunduku matatu yaani ubunge, wawakilishi na udiwani," alisema.

Kuhusu Viti Maalum kupitia vijana, Nape alisema utaratibu wa mwisho wa kutoa majina utafanywa na UWT Taifa badala ya Baraza la Umoja wa Vijana.

Pia, alisema Jumuiya ya Wazazi imepewa viti viwili vya ubunge na mchakato wake utapitia Baraza la UWT.

Aidha, alisema daftari la wanachama wa CCM litafungwa Julai 15, mwaka huu na pia zipo hatua zitazochukuliwa kudhibiti wanachama feki.

Alisema viwango vya uchukuaji fomu vipo kwenye kanuni kama ilivyo katika vipindi vya uchaguzi vilivyopita. Hata hivyo, aliwataka wagombea kuzingatia kanuni na taratibu za chama hicho ikiwa ni pamoja na kuzisoma na kuzielewa kanuni hizo ili wasifanye kinyume na taratibu.

"Tusingependa kuona wale wanaokuja kuchukua fomu na kurudisha wanakuja kwa mbwembwe na hatutaki sherehe wala madoido, safari hii kosa moja goli moja," alisema.

Kuhusu upigaji kura, alisema mwanachama anatakiwa awe na kadi mbili, yaani kadi ya uanachamana kadi kupiga kura kwa ajili ya utambulisho wake.

Baadhi ya wajumbe wa Nec, wamesema hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, juzi imewafanya wanachama wa chama hicho kuwa wamoja na kutambua dhamira ya mwenyekiti wao ndani ya chama na Taifa kwa ujumla.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Makao Makuu ya chama hicho maarufu 'White House', walisema hotuba hiyo imedhihirisha kuwa Rais Kikwete hana mgombea na hatakuwa tayari kukiacha chama kikienda ovyo wakati yupo.

Pia wameeleza kuwa hotuba yake imeleta matumaini mapya ya kuwaunganisha wanachama kuwa wamoja.

BALOZI KARUME
Mmoja wa wajumbe wa NEC kutoka Zanzibar, Balozi Ali Karume, alisema hotuba hiyo ni kama darasa kwa wanachama wa chama hicho."Nimefurahishwa na hotuba ya Rais Kikwete kwani ameonyesha ukomavu wake kwenye medani ya siasa ndani ya chama," alisema.

Balozi Karume alisema hotuba ya Rais Kikwete itatumika kuivusha CCM katika uchaguzi mkuu na chaguzi nyingine zinazotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

"Naamini hata nukuu zake zitakuwa dira ya kukiongoza chama chetu wakati kutakapokuwa na viongozi wengine," alisema.

Alisema Rais Kikwete amezungumza mambo ya msingi na wazi, amedhihirisha anatanguliza maslahiya chama chake na si marafiki zake kwani ameweka wazi kwenye suala la kuchagua kiongozi kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama hakuna sababu ya kutanguliza urafiki.

"Mwenyekiti wetu wakati anazungumza alinukuu baadhi ya meneno yaliyokuwa yakizungumzwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, lakini naamini hotuba ya Rais aliyoitoa leo(juzi) itakumbukwa na kizazi cha sasa na kijacho".

"Hotuba hii ya Rais itatumika kama nukuu kwa ajili ya chaguzi na namnaya kukiendesha chama.
Nimekaa nje ya nchi kwa muda mrefu, lakini alichozungumza Rais amedhihirisha kiwango chake kwenye siasa ni cha hali ya juu na amekomaa katika demokrasia. Amekuwa kwenye chama muda mrefu kwa hotuba yake hii anakwenda kupumzika akiwa ameacha historia iliyotukuka," alisema Balozi Karume.

Alisema moja ya mambo yanayoharibu chama ni pamoja na kuingiza urafiki kwenye masuala ya uongozi.

"Na hilo Rais Kikwete amezungumza kwa ufasaha na ameonyesha kutokuwa tayari kuchagua kiongozi kisa urafiki au kujuana kwa maslahi binafsi," aliongeza.

Balozi Karume alisema Rais Kikweteamezungumza na wajumbe wa NEC lakini hakuonyesha anataka nani achaguliwe kwani hakuwa upande wowote zaidi ya kuzungumzia hali halisi ya chama hicho na wakati uliopo.

"Ingekuwa wengine hapa tungeanza kupata maelekezo ya Rais kuhusu nani anataka awe Rais baada ya kumaliza muda wake, lakini yeye hana chaguo lake, hivyo ametaka sifa, kanuni na maadili ya chama iwe dira ya kupata viongozi wake."

ABDALLAH BULEMBO
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, alisema mgombea wa CCM lazima awe msafi na asiyekuwa na kashfa chafu.

Alisema mgombea wa CCM anayetaka kugombea uongozi si yule mwenye mbwembwe na madoido mengi, bali ni mtu mwenye kujitambua na kujiamini.

KHAMISI MGEJA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, alisema hotuba ya Rais Kikwete ni darasa tosha kwa wanachama wa CCM hasa kipindi hiki kwa kuwa suala la kuchagua viongozi ni la muhimu.

Aliwataka wajumbe wa Nec na wanaCCM kwa ujumla kuisikiliza kwa umakini hotuba hiyo ili kufahamu misingi ya chama hicho.

"Lazima wanachama wasome alama za nyakati kwa kuchagua viongozi si utashi wa viongozi, bali kwa utashi wa wananchi ambao ndiyo wanaopiga kura"."Nimesikiliza vizuri hotuba ya Mwenyekiti wetu, amezungumza mambo ya msingi ambayo kwetu sisi ni darasa tosha. Lazima tusome alama za nyakati.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka jana tumeshuhudia baadhi ya mitaa imekwenda upinzani kwa sababu ya viongozi kuwa na watu wao na si wale wanaotakiwa na wananchi," alisema na kuongeza:"Hivyo lazima tuchague viongozi kwa kuangalia wananchi wanamtaka nani na si kiongozi anataka nani awekiongozi."Mjumbe wa Nec kutoka Wilaya ya Musoma, Vedastus Mathayo, alisema hotuba hiyo imetoa mwelekeo kwa chama hicho na njia madhubuti kuelekea katika uchaguzi mkuu.


MWIGULU AJIUZULU
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba, amejiuzulu wadhifa huo.

Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha anatajwa kuwa miongoni mwa makada wa CCM wenye nia ya kuwania kupitishwa nachama hicho kuwania urais uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

CHANZO: NIPASHE