RAIA 800 WA BURUNDI WAINGIA TANZANIA WAKIKIMBIA MACHAFUKO NCHINI KWAO

Idadi ya watu wanaokimbilia nchini kutafuta hifadhi kutokea Burundi imezidi kuongezeka huku Serikali ya Tanzania ikithibitisha kuwa jumla ya watu 800 wameingia na kuorodheshwa.

Raia hao wanakimbia machafuko ya kisiasa nchini humo yaliyoanza hivi karibuni.

Aidha, kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, watu 51 waliongia nchini wiki iliyopita kupitia mkoani, Kagera wamerudishwa makwao kutokana na kukiuka sheria na taratibu za uhamiaji.

Nantanga alisema wakimbizi hao walirudishwa Burundi kwa sababu kabla ya kuingia nchini walitokea Rwanda na huku akisisitiza kuwa sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa (UN) haziwahesabu kama wakimbizi kamili.

"Watu 51 waliongia nchini wiki iliyopita kutokea Burundi na kuingia mkoani Kagera wamerudishwa kwao kutokana na kuingia nchini kupitia Rwanda tofauti na sheria za Uhamiaji zinavyoelekeza," alisema Nantanga.

Aliongeza kuwa kati ya wakimbizi 800 waliongia nchini kupitia mkoaniKigoma, 720 tayari wamepelekwa katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoaoni humo.

Nantanga alisema mpaka Aprili 30, mwaka huu katika mkoa wa Kigoma watu 500 waliingia kupitia vijiji sita ambavyo ni vya Kibuye, Kagunga, Kosovo, Kakonko, Sekeeye na Kigaye.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella, jana alithibitisha kuwa kuna raia wa Burundi wanaoingia mkoani humo, lakini alisema kutokana na kutokuwapo kwa kambiya wakimbizi, wamekuwa wakipelekwa mkoani Kigoma ambako kuna kambi ya kuwahifadhi.

"Wapo baadhi wanakamatwa na kurudishwa nchini mwao, lakini wengine tunawakabidhi mkoa wa Kigoma ambao kwa sasa una kambi kwa ajili ya kuwahifadhi, hata tukisema wakae hapa hatuna mahala pa kuwahifadhi," alisema Mongella.

Alisema kwa sasa mkoa wa Kagera hauna mpango wa kufungua kambi kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi hao, na kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutowapokea nakuwahifadhi watu hao na badala yake watoe taarifa wakati watakapoona wameingia katika maeneo yao.

"Waharifu nao wanaweza kutumia fursa hiyo kuingia, ninachowaomba wananchi wasijiingize katika masuala ya kupokea watu na kuwahifadhi, badala yake wawakabidhi kwa wenyeviti au maafisa watendaji walioko katika maeneo yao," alisema Mongella.

Burundi imekumbwa na vurugu kutokana na maandamano yanayofanyika kwenye mji mkuu wanchi hiyo Bujumbura, wakipinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutaka kugombea tena urais kwa muhula wa tatu, baada ya kumaliza muda wake wa mihula miwili.

Katiba ya Burundi inataja muda wa urais kuwa ni vipindi viwili, lakini Rais Nkurunziza anasema kwa mujibu wa makubaliano ya Mkataba wa Arusha, kipindi chake kinaanza pale mkataba huo uliposainiwa, hivyo muda aliokuwa madarakani kabla ya kusainiwa usihesabiwe.

Anasema kuwa, muhula huu ndio utakuwa kipindi chake cha pili na cha mwisho.

Hata hivyo, upinzani unapinga na yamekuwepo maandamano kuanzia Jumamosi ya kupinga hatua hiyo, natayari watu kadhaa wametiwa nguvuni na baadhi wanadaiwa kupoteza maisha.

CHANZO: NIPASHE