Kama dawa hizo haramu zingeuzwa mitaani nchini Uingereza, zingekuwa na thamani ya Sh1.5 trilioni, kiasi ambacho nchi wafadhili zinatarajiwa kuichangia Tanzania kwenye bajeti ya mwaka 2015/16.
Matukio mengine yaliyoichafua nchi ni la meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Tanzania ambayo ilikamatwa Septemba 2013, jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterranian nchini Italia wakati ikielekea Uturuki ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni 50 milioni za Uingereza (sawa na Sh125 bilioni). Tukio jingine ni lile la Watanzania wawili kukamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6 bilioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.
Kiwango hicho cha dawa zilizokamatwa kimeweka rekodiya ukubwa wa mzigo wa dawa hizo haramu nchini Uingereza. Awali shehena ya cocaine iliyokuwa kubwa ilikamatwa Septemba mwaka jana ikiwa na mzigo wenye thamani ya Sh 450 bilioni.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, meli ya MV Hamal ilikamatwa kwenye Bahari ya Kaskazini na baada ya kupekuliwa kwenye bandari ya Arberdeen nchini Scotland, ilikutwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 32 na uwezo wa kubeba tani 422, ilikamatwa na askari wa kikosi cha majini cha Royal Navy waliokuwa kwenye meli ya HMS Somerset pamoja na askari wa uhamiaji wa Border Force waliokuwa kwenye meli ya Valiant, karibu kilomita 160 mashariki mwa mji wa Aberdeen Alhamisi baada ya kupewa taarifa na kitengo cha makosa ya jinai, NCA.
Baadaye, meli hiyo ilipelekwa bandari ya Aberdeen, ambako maofisa wa Border Force wenye stadi maalumu ya upekuzi, waliipekua meli hiyo kwa kusaidiana na polisi wa Scotland.
John McGowan – afisa mwandamizi wa uchunguzi wa NCA, alisema: "Upekuzi wa meliulikuwa mrefu na unaosababisha maumivu, na uliofanywa na watu wenye utalaamu mkubwa wa kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
"Matokeo yake ni ugunduzi huu mkubwa – unaoaminika kuwa mkubwa kuwahi kutokea kwenye rekodi nchini Uingerezana ambao unaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya fedha."
Hata hivyo, rekodi za mtandao wa shughuli za baharini unaonyesha kuwa katikati ya Februari, meli hiyo ilikuwa Uturuki na wiki mbili zilizopita ilianza safari kutoka visiwa vya Tenerife nchini Hispania na ilipokamatwa ilikuwa inaelekea Hamburg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ujerumani ikitazamiwa kufika jana usiku.
Meli hiyo imekutwa na watu tisa wenye umri kati ya miaka 26 na 63 wote raia wa Uturuki na wameshitakiwa kwa kukutwa na dawa za kulevya. Washitakiwa wote hawakusema lolote waliposomewa mashtaka yao. Washitakiwa hao ni Mustafa Ceviz, 54, Ibrahim Dag,47, Mumin Sahin, 45, Muhammet Seckin, 26, Umit Colakel, 38, Kayacan Dalgakiran,63 na Emin Ozmen, 50, wote wanatoka jiji la Istanbul. Wengine ni Abdulkadir Cirik, 31, anayetoka Mersin na Mustafa Guven, 47, kutoka Yozgat, nchini Uturuki. Walifikishwa mahakamani Jumatatu.