Wiki iliyopita, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walitangaza kuwa fomu kwa wagombea urais zitatolewa kwaSh1 milioni, ubunge Sh250,000 na udiwani Sh50,000.
Kwa upande wa Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema mgombea wa urais, atalazimika kulipa Sh1 milioni kwa nafasi hiyo.
Naibu Katibu Mkuu-Bara, John Nyambabe alisema jana kwamba fedha zitakazopatikana kwa gharama za fomu zitatumika kusaidia shughuli za chama.
"Tayari tumeshatoa fomu kwa mtu mmoja kwa upande wa urais ambaye ni Dk George Kahangwa, lakini bado fomu zipo na chama kinakaribisha wengine," alisema Nyambabe.
Alisema gharama za fomu za ubunge ni Sh50,000 na udiwani Sh20,000.
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema mgombea urais atalazimika kulipia fomu Sh500,000.
Ofisa Uchaguzi wa CUF, Lugoni Abdulrahaman alisema tayari wabunge wamesharejesha fomu na kura za maoni zinaanza Mei 20, mwaka huu.
Alisema wagombea hao walichukua fomu kwa Sh50,000, huku za udiwani zikiwa ni Sh20,000.
"Wagombea wa ubunge na udiwani tayari wamesharejesha fomu mchakato wa kura za maoni unaanza na kwa kuanza tunaanzia Zanzibar," alisema Lugoni.
Vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ambavyo vimekubaliana kumteua mgombea mmoja wa urais.
Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 22 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 23 na 24 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za uchaguzi ikiwamo kutoa fomu.