WATU WAWILI WAUAWA KWA RISASI MJINI TEXAS

Polisi mjini Texas wanasema kuwa wamewapiga risasi na kuwaua watu wawili waliokuwa nasilaha, waliowashambulia walinda usalama kwa risasi, walipofika katika eneo la hafla moja yenye utata ya uchoraji wa vibonzo vya kuwakejeli waislamu na mtume Mohammed.

Duru za habari zasema kuwa kisa cha ushambuliaji wa risasi kimefanyika katika sherehe moja, iliyokuwa ikifanyika mjini Dallas, mahala ambapo waandalizi walikuwa wakiendesha onyesho hilo.

Hafla za Sherehe hiyo iliyoandaliwa na kundi moja la kisiasa la kihafidhina, ambalo limekuwa likikejeli Uislamu, lilikuwa litoe zawadi nono ya dola milioni kumi kwa mchoraji kibonzo mahiri zaidi, atakayeibuka mshindi kwa kumchora mtume Mohamed.

Mwanasiasa kutoka Uholanzi Geert Wilders -- ambaye anafahamika kwa matamshi yake dhidi ya kuwadunisha waislamu, alikuwa msemaji mkuu katika hafla hiyo.

Aliyeshuhudia ameiambia BBC kuwa, aliwaona maafisa wa polisi wakimtia mbaroni mshukiwa wa tatu, ambaye alionekana kuwa hana silaha.

Kikosi cha kutegua mabomu pamoja na ndege za helikopta za polisi zimefika mahali hapo kwa sasa.