Mama huyo mkazi wa kijiji cha Karema, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda, kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini Mpanda kwa matibabu baada ya mkono wake kunyofolewa na mamba aliyemshambulia wakati akifua kando ya Mto Ikola.
Akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyemtembelea hospitalini hapo masaibu yaliyomsibu, alisema anamshukuru sana binti yake mwenye umri wa miaka tisa aliyeweza kuokoa maisha yake licha ya kuwa amenyofolewa mkono na mamba huyo.
Akisimulia mkasa huo, Magreth alieleza kuwa juzi akiwa anafua kando ya mto Ikola ghafla mnyama huyo aliibuka majini na kumpiga usoni na mkia wake.
"Mamba huyo aliibuka ghafla mtoni na kunichapa usoni na mkia wake nami nikaangukia majini ndipo aliponidaka mkono wangu na kunivutia mtoni ….binti yangu aliyekuwa jirani yangu alipoona nikokaribu kuliwa na mamba kwa ujasiri aliweza kukabiliana naye … Alinishika mkono mwingine na kunivutia nje huku akipiga kelele kumtisha mnyama huyo ili aniachie hatimaye akaunyofoa mkono wanguna kutokomea nao mtoni …." alieleza.
Aliongeza kuwa watu waliokuwa wakifua mtoni hapo wengi wao wakiwa wanawake walifika eneo la tukio ambapo wakiwa na binti yangu walimvuta na kumtoa nje na baadae wakamkimbiza hospitalini mjini Mpanda kwa matibabu.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa amethibitisha kuwa hali yamama huyo inaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.