Chenge, anatuhumiwa kupokea fedha kutoka kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd Sh. bilioni 1.6.
Chenge aliitwa katika Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo ambazo ni kinyume cha maadili. Hata hivyo, alipinga akisema kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kumhoji kwa kuwa liko katika Mahakama ambayo ina mamlaka kuliko baraza, na kueleza kuwa atafungua kesi ya kupinga mahakamani.
Katika maombi yake, lililowasilishwa masjala kuu ya Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Chenge ameorodhesha sababu 13 za kupinga mwenendo wa baraza na mapendekezo yaliyowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na shauri hilo.
Kwa mujibu wa hati yake ya maombi, anadai kwamba mwenendo wa Baraza na maazimio ya Bunge ya Novemba 29, mwaka 2014, yalikuwa ni kinyume cha amri iliyotolewa Novemba 25, mwaka 2014 ikisimamisha kwa muda kuwasilishwa na majadiliano ripoti iliyohusiana na uhamishaji wa fedhaza akaunti ya Tegeta Escrow.
Kesi hiyo imepangwa mbele ya jopola majaji watatu likiongozwa na Stella Mugasha, Augustine Mwarija na Dk. Fauz Twaib.
Majaji wamewaelekeza walalamikiwa ambao ni Tume ya Maadili ya Baraza la Maadili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha majibu yao Mei 8 na Mei 21, mwaka huu kesi hiyo itasikilizwa.
Jopo la mawakili 10 linalomwakilisha Chenge katika kesi hiyo linawajumuisha Deogratias Ringia, Wilson Ogunde, Jamhuri Johnson, Michael Ngalo, Respicius Didace, Okare Emesu, Cuthbert Tenga, Dosca Mutabuzi, John Nyange na Stephano Kamala.
Katika maombi yake, Chenge anaiomba mahakama kutoa amri yakudumu ya kuizuia Tume na Baraza kuendelea au kutafakari kuanzisha malalamiko yoyote dhidi yake kuhusiana na ripoti za CAG na PAC.
Kadhalika, anaiomba mahakama kutoa azimio kwamba malalamiko yaliyoanzishwa na tume kupitia baraza lake ni batili kutokana na ukiukaji wa taratibu na kwamba majadiliano ya Bunge na maazimio yake hayakuwa sahihi, hayakuwa ya kisheria, na kwa hiyo yalikuwa batili.