WATU WENYE ULEMAVU WAFUNGA BARABARA KUPINGA KUVUNJIWA MEZA ZAO

Walemavu wanaofanya biashara katika soko la Karume Mchikichini wamelazimika kulala katika makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya masaa sita wakilalamikia kuvunjiwa meza zao za biashara na halmashauri ya manispaa za Ilala, hali iliyosabaisha baadhi ya barabara kushindwa kupitika kutokana na kuwepo kwa msongamano mkubwa wa magari.

ITV imeshuhudia walemavu hao wakiwa wamekaa katikati ya makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru bila woga, huku wakifukuza watu ovyo kwamba hawahusiki katika kuwasidia, ambapo katika mahojino na baadhi yao wamesema wamesikitishwa na kitendo cha serikali ya wilaya ya Ilala kuwavujia meza zao na kusababisha upotevu wa baadhi ya mali zao na kuongeza kuwa iwapo serikali haitaingilia kati sakata lao watalala hapo barabarani.

Licha ya barabara mbalimbali kushindwa kupitika kutokana na sakata hilo ambalo limevuta hisia za watu wengi, baadhi ya madereva wamelalamikia kusimama katika msongamano kwa masaa mengi
Huku wakidai kuwa kuendelea kwa sakata hilo inasababisha shughuli mbalimbali muhimu ikiwemo shughuli za maendeleo kusimama.

Kutokana na hasira za kuvunjiwa meza zao majira ya usiku bila taarifa, baadhi ya viongozi waliofika katika eneo hilo ili kuzungumza nao walijikuta katika wakati mgumu huku askari wa polisi wakitumia hekima ya kutowatawanya watu hao kwani kwa kufanya hivyo wengi wao wangeumia.

Majira ya saa kumi jioni huku msongamano wa magari ikiendelea kutesa watu, baadhi ya watu walionekana kutembelea kwa mguu katika baadhi ya barabara kwa kukosa usafiri huku mkuu wa wilaya ya Ilala Reymond Mushi akikubali kuwepo kwa maelezo ya maaandishi kuwa wafanyabiashara hao watarudi katika maeneo yao huku uchunguzi ukianza mara moja ili kubaini madhara ya vunjavunja hiyo pamoja na suala la fidia.

CHANZO:ITV