MIKOPO YA WANAFUNZI HESLB YAIVA

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), jana imetoa mwongozo kwa wanafunzi wahitaji wanaotarajia kuomba mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2015/2016 unaotarajiwa kuanza miezi michache ijayo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, ambao unapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz), waombaji wamepewa miezi miwili kuwasilisha maombi yao kuanzia Jumatatu (Mei 4) hadi Jumanne (Juni 30, 2015).

Mwongozo huo uliotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega, unasema wanafunzi wote wahitaji wa mkopo na ruzuku wanapaswa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum kupitia mtandao unaojulikana kama"Online Loans Application and Management System" ulioanzishwa na HESLB kwa ajili ya kupokea maombi hayo.

Mfumo huo unapatikana kupitia tovuvi ya Bodi au kwa kufungua kiunganishi chake (http://olas.heslb.go.tz).Mwongozo huo pamoja na mambo mengine, unafafanua kuwa waombaji wa mara ya kwanza wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Sh. 30,000 na kisha kutumia namba ya muamala na kuingia katika mtandao na kuanza kujaza fomu za maombi.

"Waombaji wa mara ya kwanza wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Sh. 30,000 ambayo inalipwa mara moja tu na haitarudishwa kwa njia ya M-Pesa," inasisitiza sehemu ya mwongozo huo.

Aidha, imesisitizwa kuwa wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea namasomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu, hawapaswi kuwasilisha maombi tena.

Kwa mujibu wa Nyatega, Bodi imewasihi waombaji na wadau wengine kuusoma na kuuzingatia mwongozo huo wakati wote wanapofanya na kuwasilisha maombi.

HESLB ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu.

Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.