WATU WATATU WAUAWA SHAMBULIZI LA BOMU BURUNDI

Watu watatu wameuawa katika shambulizi la bomu lililowalenga askari polisi nchini Burundi ambapo zaidi yawatu mia sita wametiwa mbaroni wakati wa maandamano na ghasia za kupinga raisi wa taifa hilo Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu wa kiti cha urais.

Mkuu wa Polisi nchini humo Generali Andre Ndayambaje amesema kuwa maafisa wawili wa polisi waliuawa na mmoja kujeruhiwa katika wilaya ya Kamenge ya mji mkuu wa Bujumbura.

Shambulizi kama hilo linatajwa kutekelezwa katikati mwa jiji hilo ambapo maafisa watatu walijeruhiwa.

Afisa mmoja wa polisi ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema kuwa ni wazi kuwa waandamanaji wameanzisha mashambulizi ya ghafla na ameongeza kuwa ikiwa raia hao wanataka vita watakiona cha mtema kuni.