Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa12:50 asubuhi muda mfupi tu baadaya basi hilo kuanza safari.
Mashuhuda walisema basi hilo likiwa kwenye mwendo mkali lilitaka kulipita lori lililokuwa mbelena wakati likiwa limeingia upande wa kulia wa barabara, lilitokea lori lingine la kusafirisha mafuta kwa mbele na hivyo magari hayo yakataka kugongana uso kwa uso.
Gasper Alfred, mkazi wa kijiji cha Shamwengo, alisema baada ya basi hilo kumshinda dereva na kutumbukia mtoni, abiria waliokuwamo walitoka wakiwa wameumia, huku watatu baadhi yao wakionekana kupoteza maisha.
"Nililiona basi hili likijaribu kulipita lori la mbele, lakini kwa upande wa pili likatokea lori lenye tenki la mafuta ndipo dereva wa basi akaamua kulikwepa ili wasigongane uso kwa uso, lakini dereva alipotakakurudi barabarani gari lilimshinda na kutumbukia mtoni, nimeona watu wengi wametolewa wakiwa wameumia na watatu wakiwa wamekufa," alisema Alfred.
Alisema kuwa miongoni mwa watu alioshuhudia wakitolewa kwenye gari wakiwa wamekufa, mmoja wao ni mzungu wa jinsia ya kiume na wengine wawili ni Watanzania, mmoja akiwa mwanaume na mwingine mwanamke.
Daktari wa zamu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Lathan Mwakyusa,alithibitisha kupokea miili ya marehemu watatu pamoja na majeruhi 28 hospitalini hapo.
Dk. Mwakyusa alisema miongoni mwa majeruhi hao 28, kati yao 24 walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku wengine wanne wakilazimika kulazwa hospitalini hapo kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo pamoja na maeneo wanayoishi kwenye mabano kuwa ni Patric Mwakasege (Uyole), Erasto Nyoni (Iyunga), Ester Nyange (Kilosa), Agness Mwambosyo (Kiwira), OmaryAlly (Jacalanda), Fatma Nyambi (Loleza), Tabia Sward (Kyela), Maua Ngonyani (Songwe), Catheline Mbula (Dar es Salaam), Edson Omary (Chunya), Asukenye Mwandanege (Tukuyu), Veronica Emmanuel (Kilosa), Emmanuel Mwandanege (Tukuyu).
Wengine ni Charles Lwambano (Mbeya), Baraka Abiah (Airport) Patrick Mlimbilwa (Songea), Mwangaza Shaibu (Airport), Felicia Mwalongo (Songea), Francis Abel (Songea), Adam Raphael (Mbinga), Anuary Hemed (Njombe), Canoe Ho(Rudewa), Petili Mbema (Songea), Fatma Abdallah (Airport), Ginny Warley (Njombe), Cecilia Rengina (Njombe) na Ashraf Abiah (Airport).