WAHAMIAJI WATIKISA SOKA ITALIA

*Timu ya weusi tupu yapanda daraja

Timu ya soka nchini Italia inayoundwa na Waafrika wahamiaji tupu imepanda kutoka daraja la chini kabisa nchini humo.

Timu hiyo, Koa Bosco, ilishinda kwenye mechi ya mtoano Jumapili na hivyo kuwa juu kabisa ya msimamo wa ligi katika Jimbo la Calabria Kusini. Maana ya jina la timu hiyo ni Watumishi wa Madhabahu.

Shirikisho la Soka la Italia lina mfumo wenye ngazi tisa, kuanzia Serie A ambayo ni Ligi Kuu hadi ile ya mwisho, Terza Categoria, ambayo ni ya ridhaa na ambako Koa Bosco wanaondoka.

Wanaounda timu hii ni wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi mbalimbali, zikiwamo Senegal, Ivory Coastna Burkina Faso. Jimbo waliloweka makazi ni moja ya maeneo masikini zaidi nchini Italia.

Wengi wa wachezaji wa timu hii huishi kwenye mahema au makontena katika kambi inayoendeshwa na Serikali ya Italia ikaribu na mji wa Rosarno, kusini mwa nchi.

Timu hiyo iliundwa na Padre wa Kanisa Katoliki, Roberto Meduri na inaendeshwa na kufundishwa na Wataliano wa eneo hilo.

"Si rahisi kuendesha mradi wa aina hii, kuna magumu mengi. Vijana hawa wamepiga hatua kubwa, ni ushindi na ni wazi kwao kwamba maisha ya kila siku yanasonga mbele," Mkurugenzi wa Koa Bosco, Domenico Bagala ananukuliwa na jarida la Il Calcio akisema.

Anaeleza kwamba kuanzia asubuhi hadi alasiri wahamiaji hao hufanya kazi kwenye mashamba yaliyo jiranina pia kwenye bustani za machungwa.

Haikuwa rahisi kwa timu hii kupanda daraja, kwani wachezaji walikuwa wakikashifiwa kwa sababu ya rangi yao, kwa mfano Machi mwaka huu wakicheza ugenini zilitokea fujo na wachezaji wao wakatupiwa mawe kutoka majukwaani.

Mechi hiyo ilivunjwa na baadaye timu zote zikaadhibiwa, ambapo wenyeji, Vigor Paravati waliambiwa kwamba hawakuonesha kitendo cha kimichezo.

Hata hivyo, tangu kupanda kwao daraja watu kutoka maeneo mbalimbali wamekuwa wakiwatumia salamu za pongezi na sifa.

Kocha wao, Domenico Mammoliti, amekuwa akitundika mtandaoni baadhi ya salamu hizo, akieleza mwenyewe kufarijika na kwamba huu ni mwanzo wataendelea kupanda madaraja.

Tayari timu hiyo imeanza kuwa na mvuto kwa klabu kubwa kamaJuventus, ambapo Mkurugenzi wa Juve, Pavel Nevded majuzi alialika kikosi chote na viongozi kwenye Makumbusho ya Juventus.

Hapo walikutana na wachezaji wa Juventus na wakabadilishana jezi kama kutakiana heri na pia kuwapongeza Koa Bosco kwa hatua waliyopiga.

Padre Meduri anasema awali alipounda timu hiyo alikuwa na nia ya kuwachanganya wageni katika jamii, kujenga urafiki na kusitisha hali mbaya iliyokuwapo, ambapo fujo zilipata kuua watu 53 kujeruhiwa baada ya Waafrika wawili kupigwa risasi 2010.

Ni mara chache Koa Bosco hupata ufadhili wa kifedha, lakini kwa kupanda daraja na kuanza kujulikana sehemu nyingi, wanatarajia mambo mazuri baadaye.

Hata hivyo, watu wa maeneo ya jirani wamekuwa wakikusanya na kutoa msaada wa mablangeti na mavazi ya kuwatia joto wachezaji.

Eneo wanaloishi lina ukosefu wa ajira na nahodha wa timu hiyo anayetoka Ivory Coast,Yaya Diallo, anaamini ni vyema Waafrika wengine wakabaki nyumbani ambako wanaweza kufanikiwa kuliko hatari ya kusafiri kwenda Italia.

Italia huwa na wahamiaji wengi ambao husafiri kwa boti kutoka Afrika wakipitia pwani ya Libya, na wengi hufia baharini katika kile wanachosema ni kwenda kutafuta maisha Ulaya.