MTIKILA ATAKA MAHAKAMA YA KADHI ISIJADILIWE

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameiomba Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kutoa amri kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusitisha kujadili suala lolote linalohusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Mtikila aliwasilisha maombi yake jana mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Richard Mziray, anayesaidiana na Jaji Lawrence Kaduri na Said Kihio.

Kesi ya msingi ambayo Mtikila anaomba Mahakama ya Kadhi isiruhusiwe nchini, ilipangwa kutajwa jana.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Gabriel Malata na Kasori Sarakikya, ulidai kuwa utawasilisha majibu ya maombi ya Mtikila leo.

Mtikila alidai kuwa anaomba kuwasilisha hati ya dharura mahakamani akitaka bunge hilo lisijadili wala kuzungumzia suala la Mahakama ya Kadhi.

"Ina maana suala hili baada ya kufunguliwa mahakamani linajadiliwa huko nje ya Mahakama?," alihoji Jaji Mziray na kuitikiwa na Mtikila.

Jopo hilo lilisema upande wa Jamhuri uwasilishe majibu ya maombi ya Mtikila kwa njia ya maandishi leo na kesho kesi hiyo itatajwa.

Mtikila alifungua kesi ya madai kupinga kitendo cha serikali kupeleka muswada bungeni wa kutunga sheria ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, kwamba kuanzishwa kwake ni kinyume cha Katiba ya nchi.


Mtikila ameiomba Mahakama itoe amri kwamba wale walio kwenye mamlaka ya serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano naUratibu), Mary Nagu; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na wenzao, watoe sababu kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka mitano ikiwa watashindwa kujieleza.

Pia, Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14 yamwaka huu, ameomba Mahakama itoe amri ya vigogo hao kufungwa kifungo hicho kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.

Katika hati yake, Mtikila pia anaiomba Mahakama itoe amri kwamba Mahakama ya Kadhi na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC), itangaze kuwa ni haramu kwenye ardhi ya Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Mtikila anadai kuwa suala la serikali kuandaa Muswada wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo cha Bunge kukubali zaidi ya kuukataa ni sawa na uhaini, kinachofanywa na waliopanga kuupeleka muswada huo bungeni.

Anaendelea kudai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo vya viongozi hao walivyoapa wakati wa kushika nafasiza uongozi wa umma na ni kinyume cha kifungu cha 19 cha Katiba ya nchi kinachoeleza kwamba masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kuongeza kuwa uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya nchi.

CHANZO: NIPASHE