Gwajima amelazwa ikielezwa hali yake ilibadilika wakati akihojiwa na makachero wa Polisi waliokuwa wanamhoji baada ya kujisalimisha baada ya kutakiwa kufanya hivyo kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.
Kukamatwa kwa watu hao, wakiwemo wachungaji sita, mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu chaDar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), Dar es Salaam kumethibitishwa na taarifa ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Katika taarifa yake, amesema watu hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama pamoja na kujaribu kumtorosha Askofu Gwajima ambaye amelazwa katika Hospitali ya TMJ kwa matibabu.
Alisema saa tisa na nusu usiku wa kuamkia jana, watu 15 walifika hospitalini hapo kwa lengo la kumuona mgonjwa huyo.
"Askari ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia mashaka watu hao hivyo waliwakatalia kuingia. Na hapo walijaribu kutumia nguvu, lakini walikamatwa," alisema.
Kova alisema baada ya kuwapekua, watu hao walikutwa na begi lenye bastola aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za Short gun na vitabu viwili vya hundi.
Alisema begi hilo pia lilikuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundicha Benki ya Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya Simu na Tablets, suti mbili na nguo za ndani.
Aliwataja waliokamatwa ni Chitama Mwakibambo (32), fundi seremala mkazi wa Gongo la Mboto, Mchungaji Edwin Audex (24) mkazi wa Kawe Maringo, Adam Mwaselele(29), mhandisi na mkazi wa Kawe Maringo, Frederick Fusi (25) mkazi wa Mbezi Beach.
Wengine mwanafunzi wa chuo cha IMTU, Frank Minja (24) mkazi wa Mbezi Beach, Emmanuel Ngwela (28) mkazi wa Keko juu ambaye ni mlinzi shirikishi, Geofrey William (30), Mhadhiri UDSM mkazi wa Survey Chuo Kikuu, Mchungaji Mathew Nyangusi (62) mkazi wa Mtoni Kijichi, mchungaji Boniface Nyakyoma (30) mkazi wa Kitunda.
Pia wametajwa Geofrey Andrew (31), dereva mkazi wa Kimara Baruti, Mchungaji David Mgongolo (24) mkazi wa Ubungo Makoka, Mfanyabiashara George Msava (45) mkazi wa Ilala Boma, Mchungaji Nicholaus Patrick (60) mkazi wa Mbagala Mission, George Kiwia (37) ambaye ni dalali wa magari na mkazi wa Tandale Uzuri na mchungaji Yekonia Bihagaze (39) mkazi wa Kimara Stop Over.
Kova alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni yakubaini sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote zilizotumika kutaka kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.
Pengo Asamehe
Wakati hayo yakiendelea, jana Pengo aliwatangazia waumini wake kumsamehe Gwajima na pia kuwataka waumini wake pia wamsamehe.
Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph ambako iliendeshwa misa ya Jumapili ya Matawi, alitoa msamaha kwa Gwajima na kusema kuwa hana chuki na mtu yeyote.
Aidha, Pengo alisema hawezi kuingilia hatua ya Polisi kumhoji kiongozi huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Gwajima: Niombeeni Aidha, katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Gwajima amewaomba waumini wake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili aweze kuendelea na kazi aliyotumwa na Mungu ya kuhubiri Injili.
Taarifa iliyotolewa na kusomwa kanisani kwake imedai kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri na afya yake imeanza kuimarika. Alisema waumini wake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili kuendelea na kazi aliyotumwa na Mungu ya kuhubiri injili.Kiongozi huyo bado amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na anaendelea kupatiwa matibabu ya karibu na madaktari kutokana na hali yake kubadilika mara kwa mara.
Hata hivyo, kwa taarifa iliyotolewa na daktari anayemtibu askofu Gwajima, Fortunatus Mazigo, alisema hali ya mgonjwa inaendelea vizuri japokuwa alikataa kusema ni nini tatizo linalomsumbua hadi akamilishe kukusanya taarifa ya vipimo vyote ambavyo vingine bado majibu yake hayajapatikana na huenda kila kitu kikawa hadharani leo.
Chanzo:Habari Leo