Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba ameunga mkono tamko
la Jukwaa la Wakristo Tanzania kupinga Katiba Inayopendekezwa, akisema
hoja zao ni za msingi kwa kuwa kuna mambo mengi yanayopingwa na
wananchi.
Kauli ya Profesa Lipumba ni mwendelezo wa kauli
tofauti zilizotolewa na watu mbalimbali kuhusu tamko la jukwaa hilo,
wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasiasa kuhusu
hatima ya Kura ya Maoni na muswada wa Makahama ya Kadhi.
Alhamisi iliyopita, jukwaa hilo linaloundwa na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) liliwataka
waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kushiriki kikamilifu
katika elimu ya Kura ya Maoni, na kisha kuipigia kura ya “hapana” Katiba
Inayopendekezwa.
Pia, tamko hilo lililotiwa saini na maaskofu Dk
Alex Malasusa wa (CCT), Tracisius Ngalalekumtwa (TEC) na Daniel Awet wa
CPCT, lilishauri mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya
kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria
ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya
masuala hayo bila kuihusisha serikali wala waumini wa dini nyingine.
Jana gazeti hili lilimnukuu makamu mwenyekiti wa
TEC, Askofu Severine Niwemugizi akisema tayari tamko hilo
limeshasambazwa katika majimbo yote ya kanisa katoliki nchini.
Kauli ya Lipumba
Akizungumzia tamko hilo, Profesa Lipumba alisema
ni sahihi kuipinga Katiba hiyo kwa sababu wananchi walilalamikia
mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya baada ya kubaini kuwa mambo mengi
waliyoyapendekeza yaliondolewa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Wananchi walitaka kuwepo na ukomo wa wabunge wao,
viongozi wasifungue akaunti nje ya nchi na mambo mengine yote hayamo
kwenye Katiba Inayopendekezwa. Hoja yao (maaskofu) ni ya msingi,”
alisema Profesa Lipumba aliyeongoza wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge la Katiba na kususia mchakato huo
moja kwa moja.
Alisema Serikali imeonyesha kutokuwa na uaminifu
kwa wananchi ndio maana haikujali hisia zao, badala yake iliamua
kuendelea na mchakato huo licha ya baadhi ya wajumbe kuususia.
Profesa Lipumba, ambaye ni mtaalamu wa uchumi,
aliongeza kuwa wananchi walitaka kuwepo na utaratibu maalumu kuhusu
viongozi wao kupewa zawadi wawapo madarakani, lakini Katiba
Inayopendekezwa ililitupa nje suala hilo.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi, Profesa Lipumba
alisema pia Serikali isitishe uamuzi wake wa kupeleka Muswada ya
Mahakama ya Kadhi katika Bunge lijalo kwa kuwa bado yapo mambo mengi
yanayotakiwa kuwekwa sawa.
CHANZO: MWANANCHI
Profesa Lipumba alisema pamoja na mahakama hiyo kutokuwa ngeni
hapa nchini kwa kuwa ilikuwapo Tanzania Bara wakati wa ukoloni na
Zanzibar, bado inaendelea kufanya kazi bila tatizo, mfumo unaotaka
kutumiwa na Serikali kuianzisha hivi sasa unapingwa na baadhi ya
Waislamu na Wakristo hivyo kusababisha mgawanyiko.
Alisema hali hiyo imefikia hapo kutokana na CCM
kuliingiza suala hilo kwenye ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005, hivyo
njia bora ya kuondoa sintofahamu iliyopo ni kwa kutumia muda mrefu
zaidi katika kutafuta muafaka.
“Ni bora tungetumia muda mrefu zaidi kutafuta muafaka, Serikali isiendelee na muswada huo,” alisema Profesa Lipumba.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema
Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, likiwamo suala la Mahakama
ya Kadhi, utawasilishwa katika bunge lijalo ukiwa na maudhui ya
kuangalia namna ya kuendesha masuala ya imani ya dini ya Kiislamu.
Nyambabe aunga mkono
Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema anaunga mkono uamuzi uliofikiwa na maaskofu hao kwa kuwa
haiwezekani nchi ikapiga Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa wakati
wananchi wamegawanyika.
“Msimamo wa maaskofu ni kama wa Ukawa. Bila kuchukua hatua mmomonyoko wa maadili hautaisha,” alisema Nyambabe.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Nyambabe alisema:
“Hakuna mtu anayepinga kuwepo kwa mahakama hiyo, lakini isiwe chini ya
serikali moja kwa moja, iwe huru.”
Kauli za wachungaji
Baadhi ya wachungaji waliunga mkono uamuzi wa
Jukwaa la Kikristo kwa maelezo kwamba jambo hilo limeamuliwa na viongozi
wao wa juu, lazima litekelezwe.
“Kwa kuwa wameshaamua, naamini tutapata hiyo barua
haraka tu, lakini mpaka sasa hatujasikia jambo lolote,” alisema
Mchungaji Emmanuel Owoya wa Usharika wa Nkwatira, Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Hai.
Naye, Mchungaji Jackson Mwaisabile wa Kanisa la
Pentecostal Assemblies of God (PAG) mkoani Iringa, alisema bado hajauona
waraka unaosambazwa na Jukwaa la Maaskofu na kwamba utakapowafikia
watajua nini cha kufanya.
Mzee wa Kanisa la Nguvu ya Uponyaji wa Ukombozi (LHPM) la Dar es
Salaam, Ayubu Luchenje alisema masuala la Katiba Inayopendekezwa na
Mahakama ya Kadhi yanahitaji kuyafahamu vyema kabla mtu hajatoa uamuzi
wake.
Luchenje alisema suala la Mahakama ya Kadhi
linakiuka misingi ya Taifa kwa kuwa Katiba iliyopo inaitambua nchi isiyo
na dini. Alisema kwa msingi huo jambo hilo linafanywa kisiasa kwa
malengo ya kutaka kulifurahisha kundi fulani katika jamii.
“Waziri Mkuu Mizengo Pinda anachofanya ni kutaka
kuwafurahisha watu fulani tu, jambo hilo haliwezekani ufanye kitu
kisichokubaliwa na Katiba,” alisema Luchenje.
CHANZO: MWANANCHI