WAGANGA 32 WATIWA MBARONI

Waganga 32 wakiwa na vifaa vya kupigia ramli chonganishi inayochochea mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi wamekamatwa katika operesheni iliyofanyika jana na juzi mkoani Geita.

Waganga hao pamoja na wengine walitiwa mbaroni baada ya kuwekewa mtego na makachero wa polisi waliojifanya wachimba madini.

Baadhi ya zana zilizokamatwa katika msako huo ni pamoja mnyama aina ya Kakakuona, ngozi za wanyama kama Chui, Fisi, nyoka waliokaushwa na sarafu zinazotumika kupima ubora wa viungo vya albino ambavyo ndani yake hupachikwa sumaku ndogo ili kuwarubuni wateja.

Taarifa zinasema kuwa mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa waganga 3,000 huku wilaya ya Geita pekee ikikadiriwa kuwa na waganga 900.

Hatua hiyo inatokana na Jaji aliyetoa hukumu jana aliyehoji kutofikishwa mahakamani waganga wa kienyeji na wanunuzi wa viungo.

Pia, msako huo ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete.