UHUSIANO TETE KENYA TANZANIA WAFUKUTA

Mgogoro unaofukuta kati ya Tanzania na Kenya umefikia hatua mbaya baada ya juzi usiku kikao cha makatibu wakuu wa Wizara za Maliasili na Utalii, Wizara za Afrika Mashariki za pande zote mbili kuvunjika.

Kikao hicho kilikuwa kikitafuta suluhu ya pande hizo mbili baada ya Serikali ya Kenya kuzuia magari ya Tanzania kuchukua watalii Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta(JKIA).

Kutokana na kuvunjika kwa kikao hicho, jana Waziri wa Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie alisusia kikao cha kutafuta suluhu na waziri mwenzake wa Tanzania, Lazaro Nyalandu.

Akizungumzia kuvunjika sakata hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Adelhelm Meru alisema kikao kilivunjika baada ya wajumbe wa Kenya kutaka kufumuliwa Mkataba wa Ushirikiano wa Utalii uliosainiwa mwaka 1985.

Alisema wajumbe wa Kenya wakiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii, Dk Ibrahim Mohamed na wa Wizara ya Afrika ya Mashariki, John Konchellah walisema suala la kuzuiwa magari ni dogo, lakini wanataka kufumuliwa kwa mkataba wote.

"Sisi Watanzania tulipinga kwa kuwa ajenda yetu ilikuwa ni moja, kwa nini magari ya Tanzania yamezuiwa kuingia JKIA na kama kuna matatizo basi ielezwe," alisema.

Alisema kutokana na mvutano huo, walishindwa kuelewana na hivyo kikao kuvunjika bila kufikia maridhiano.

Kuvunjia kwa kikao hicho kumekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) kupunguza safari za ndege kutoka Kenya kuingia Tanzania kutoka 42 hadi 14 kwa wiki.

Suala hilo limeibua hisia tofauti nchini na baadhi ya wadau wa uchumi wamesema Serikali haikutafakari kabla ya kufikia hatua hiyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema hakuna nchi inayonufaika na uamuzi huo, hivyo aliishauri Serikali kukaa meza moja na Kenya na kufikia suluhisho mapema.

Mchumi kutoka Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Abel Maganga alisema uamuzi huo utakuwa na changamoto kwa kipindi kifupi kwa watalii ambao tayari walishalipia tiketi za safari kuja nchini.

Pia, alisema endapo hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu, itakuwa na athari kwa Tanzania kwa kuwa sekta ya utalii ndiyo inayoliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana kuhusu waziri mwenzake kutokuhudhuria mkutano wa majadiliano, Waziri Nyalandu alisema walikubaliana kikao hicho kiwe na ajenda moja ya sababu za Serikali ya Kenya, kuzuia magari ya Tanzania.

Alisema kuzuia magari ya Tanzania kuingia JKIA ni kukiuka mkataba huo wa 1985 ambao unatoa ruhusa magari ya kila nchi kuingia nchi nyingine kuleta watalii.

"Tulikubaliana magari ya Kenya, yanaweza kuingia Tanzania, katika miji ya Arusha, Moshi, Tanga na Musoma kuleta watalii, hivyo hivyo magari ya Tanzania kuingia Kenya lakini tunashangaa wenzetu wameweka zuio la magari yetu na yao yanaingia nchini," alisema.

Nyalandu alisema baada ya kushindikana vikao hivyo, msimamo wa Tanzania ni kuwataka mawakala wa kampuni za utalii na watalii kuwa wavumilivu wakati mgogoro huo unafanyiwa kazi.