RAIS KIKWETE NA UHURU WAMALIZA TOFAUTI

RAIS Jakaya Kikwete na Uhuru Kenyatta wa Kenya wameingilia kati mgogoro uliopo baina ya mataifa hayo mawili kuhusu masuala ya usafirishaji na utalii.

Makubaliano yaliyofanywa na marais hao ni pamoja na Kenya kuruhusu magari ya Tanzania, yanayofanya safari za kupeleka wageni na watalii, maarufu kama 'Shuttle' kuingia kupeleka na kuchukua watalii katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKNIA).

Makubaliano mengine ni kwa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiriwa Anga (TCAA), kurudisha safari za ndege ya Shirika la Kenya (KQ) kutoka siku 14 za sasa hadi 42 za awali.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kikao kilichowakutanisha marais hao wawili jijini Windhoek, Namibia.

"Kuanzia saa 10:00 leo hii (jana) magari yote ya Tanzania yana ruksa ya kuingia Kenya kuchukua na kupeleka watalii katika uwanja wa Jomo Kenyatta na ndege za Kenya kuanzia leo zitaruhusiwa kurusha ndege zake kama kawaida kwa siku 42 badala ya 14," alisema Waziri Membe.

Aidha, Membe alisema katika kikao hicho, walizungumzia mambo mawili muhimu ambayo ni sekta ya usafirishaji na utalii, ambapo pia walikubaliana ndani ya wiki nne, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo waitishe mkutano utakaowajumuisha Mawaziri wa Usafirishaji, Utalii na Maofisa kutoka katika ofisi za Marais.

Alisema kabla ya kutoa taarifa hiyo, waliwasiliana na Mawaziri wa Uchukuzi na Utalii ambapo pia taarifa hiyo imetangazwa kwa wakati mmoja hapa nchini na Kenya.

Waziri Membe alisema mkutano wakwanza utafanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam, ambapo alisema katika mkutano huo ndipo kiini cha mgogoro huo kitabainika.

"Tanzania na Kenya ni ndugu, ni majirani tusikubali kuchonganishwa wala kuonesha tofauti zetu waziwazi, kama zipo ni vizuri tukaitana na kuzimaliza kimya kimya," alisema.

Rais Kikwete na Kenyatta wamekutana jijini Windhoek ambako walikwenda kuhudhuria sherehe za miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo na kuapishwa kwa rais wa tatu wa nchi hiyo, Dk Hage Geingob.

Hatua ya mgogoro huo inatokana na serikali ya Kenya kupiga marufuku magari ya Tanzania kuingia nchini humo, kupeleka na kuchukua watalii.

Hata hivyo hivi karibuni Mamlaka yaUsafiri wa Anga (TCAA) ilipunguza idadi ya safari za ndege za shirika la nchi hiyo kutoka 42 kwa wiki hadi 14.

Mgogoro huo umekuwa na madhara kiuchumi na maisha ya wananchi wa nchi hizi mbili.