MWAKYEMBE ATAJWA KASHFA TRL

Kuna kila dalili kwamba uhamisho wa Waziri Dk. Harrison Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki, akibadilishana nafasi na Samuel Sitta, ni sehemu ya kumwepusha na kadhia ya kashfaya mabehewa feki ambayo hadi sasa imegundulika kuwa ni kashfa nyingine inayoitafuna Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Uchunguzi huru umegundua kuwa hatua ambazo zilianza kuchukuliwa na Sitta katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA), nako TRL zimeanza kutikisa baada ya kubainika kwamba mabehewa ambayo yaliingizwa nchini kutoka China na kupokelewa na Dk. Mwakyembe kwa mbwembwe zote kisha kubainika hayana viwango, wakubwa wa kampuni hiyo walijua hilo, lakini wakafunika kombe kwa kuwa wakubwa walipeana zabuni kwa njia ya kujuana.

Habari zinasema kamati iliyoundwana Sitta kuchunguza kashfa ya uingizaji mabehewa hayo kutoka India, tayari imeibua mambo mazito ambayo yanaongeza orodha ya kashfa za ulaji na ufujaji wa fedha za umma uliosimamiwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakitumia madaraka yao vibaya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka TRL, uingizaji wa mabehewa hayo ulifanywa na Kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited ya India kwa kushirikiana na mfanyabiashara mmoja nchini ambaye kwa miaka mingi amehusika katika kadhia nyingi za kujipatia fedha kwa mikataba laghai dhidi ya serikali na mashirika yake.

Vyanzo vyetu ndani ya TRL vinasema kuwa kamati iliyoundwa kuchunguza kashfa hiyo ya ufisadi wa mabilioni ya fedha, inatarajia kukamilisha taarifa yake ya uchunguzi hivi karibuni na kuikabidhi kwa Waziri Sitta, lakini tayari imegundua madudu mengi ikiwamo wakubwa kupokea mabehewa yenye hitilafu wakati wakijua.

Waziri Sitta amesema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo lolote hadi atakapokabidhiwa ripoti ya uchunguzi. "Suala la mabehewa feki nimelikutana kuna tume (kamati) iliundwa kuchunguza na inatarajia kukamilisha ripoti yake hivi karibini, nadhani kwa sasa tungevuta subira ila niwahakikishie wananchi sitaogopa kuchukua hatua bila kujali kashfa hiyo inamhusu mtu au kiongozi wa namna gani," alisema. Kashfa ya uingizaji wa mabewa feki iligundulika mwishoni mwa mwaka jana, ikidaiwa kuwa kuna ufisadi mkubwa umefanyika ndani ya TRL katika utoaji wa zabuniya ununuzi wa mabehewa mapya.

Baadhi ya mafundi wa TRL wanasema kuwa mabehewa hayo ni mabovu na hayaendani na vipimo vya reli ya kati.Udhaifu wa mabehewa hayo uligundulika baada ya kufanyiwa majaribio, kufuatia mengi ya yale mapya 25 aliyopokea Dk. Mwakyembe kupata ajali katika mazingira ya kutatanisha, huku ikidaiwa kuwa hayana 'stability' yakiwa juu ya reli.

"Unajua hata yale ya mizigo mengi yalianguka sana. Sasa ikaonekana hebu na haya ya abiria yachekiwe vizuri, nakuambia matokeo yake ni balaa kama yangeachwa kusafirisha abiria. Ingekuwa ni kilio nchi nzima," alisema mtaalam mmoja wa masuala ya reli kwa sharti la kutokutajwa jina gazetini.

Mabehewa hayo tangu yapokelewe takribani miezi tisa sasa, hayajawahi kusafirisha abiria. Mtaalam huyo aliongeza kuwa kilichofanyika ni uongozi wa TRL wakishirikiana na wakubwa wizarani kuengua jopo la mafundi wa TRL na kuingiza mabehewa hayo kwa kuwa tayari wakubwa walikuwa na mtu wao katika tenda hiyo.

Dk. Mwakyembe alizindua mabehewa mapya 25 ya kubebea kokoto aina ya 'Ballist Hopper Bogie' (BHB), kutoka kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited yenye thamani ya Sh. bilioni 4.316 kwa ajili ya uimarishaji wa Reli ya Kati.

Upokeaji wa mabehewa ya mizigo ulifuatiwa na tukio jingi la kushuhudia upokeaji wa mabehewa mengine ya abiria Julai 24, mwaka jana Dk. Mwakyembe akiwa mmoja wa mashuhuda.

Alipoulizwa na NIPASHE kwa njia yasimu jana kuhusiana na kashfa ya mabehewa feki TRL, Mwakyembe alisema: "Hivi sasa niko nje ya nchi... vyombo vya habari vimesharipoti sana suala hili. Watu tayari walishachukuliwa hatua, inawezekana wewe (mwandishi) hujui, wenzako wameandika sana kuhusu suala hili, na watu walishachukuliwa hatua."

Katika hafla ya upokeaji na ushushaji wa mabehewa hayo katikaBandari ya Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alisema ununuzi wake ni sehemu ya utekelezaji wa makakati wa 'Matokeo Makubwa Sasa' (BRN), ambao umelenga kuhakikisha usafirishaji wa reli unaimarika kwa ajili ya kuhimili usafirishaji wa abiria na mizigo, hivyo kusaidia utunzaji wa barabara za lami zinazojengwa kila kona nchini kwa sasa.

Vyanzo vya habari kutoka TRL vinasema kuwa uhamisho wa Dk. Mwakyembe kutoka Uchukuzi, ni mkakati wa kumwepusha na kadhia yoyote ambayo inaweza kulipuka wakati wowote kutokana na zabuni hiyo ambayo inaonekana kama aina nyingine wa wizi wa wazi.

Mbali na Dk. Mwakyembe, menejimenti ya TRL nayo iko kikaangoni tangu Sitta aunde kamatiya kuchunguza kashfa hiyo.


CHANZO: NIPASHE