ALBINO MWINGINE AKATWA KIGANJA

LICHA ya Serikali, jamii na jumuiya ya kimataifa kukemea ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), bado kuna wanaoendelea kung'ang'ania mila potofu za kuamini kwamba bila ya ushirikina unaohusishwa na matumizi ya viungo vya albino, hawawezi kufanikiwa kimaisha, iwe katika kisiasa au kibiashara.
Hayo yanathibitishwa na kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya ukatili dhidi ya albino, ambapo usiku wa kuamkia jana, watu wasiojulikana walimshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kishakutokomea nacho kusikojulikana.

Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban.  ukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda.

Alisema tukio hilo ni la saa 8 usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo. Akielezea zaidi, Kamanda Mwaruanda alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada yakukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.

"Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya … "Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana," alibainisha.

Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.

Kwa mujibu wa Mwaruanda, mtoto huyo amelazwa katika katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama yake mzazi.

"Watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo hicho cha kiganja cha mkono wa mtoto Baraka," alisisitiza Kamanda.


Mchango wa CRDB

Wakati huo huo, Lucy Lyatuu anaripoti kuwa katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Benki ya CRDB ilikabidhi hundi ya Sh milioni 20 kwa mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda kwa ajili ya mapambano dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk Charles Kimei alikabidhi hundi hizo jana ambapo Sh milioni 10 zilitolewa kupitia akaunti ya Malkia. Akizungumza, Dk Kimei alisema benki hiyo inatambua mchango mkubwa ambao amekuwa akiuonesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kupigania haki na uhai wa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, huku akipinga mauaji yanayowakumba.

"Kutokana na hali hiyo, tunamkabidhi mke wake kiasi hiki cha fedha ili kisadie mapambano dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini," alisema Dk Kimei na kuongeza kuwa akaunti ya Malkia imeona umuhimu wa kulinda uhai wa kundi hilo, ambalo linatokana na uzao wa matumbo ya wanawake.

Alisema katika fedha hizo, akaunti ya Malkia ambayo kwa kiwango kikubwa ni kwa ajili ya wanawake, imetoa Sh milioni 10 huku benki ikiona umuhimu wa mapambano hayo na kuongeza kiwango kingine cha Sh milioni 10 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya mapambano hayo.

Kuhusu Siku ya Wanawake, Dk Kimei alisema ili mwanamke aweze kufanikiwa ni lazima yeye mwenyewe kuwa na utayari wa kujiwezesha kwa kujiongezea elimu, kupata mafunzo mapya na vilevile kuchangamkia fursa mbalimbali zipatikanazo.

Tunu alisema ni wazi kuwa juhudi za kumkomboa mwanamke, hazitafanikiwa kama hawatapata ukombozi wa kiuchumi. "Wanawake wengi wanashindwa kupiga hatua katika maisha yao kutokana na kuwa ni wategemezi kiuchumi na mara nyingi pia wanakandamizwa ili wasichukue hatua za kujikomboa," alisema Pinda.

Kikwete na viongozi wa albino Alhamisi wiki iliyopita, 

Rais Jakaya Kikwete alikutana na viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest Kimaya, Ikulu jijini Dar es Salaam. Katika kikao hicho, Rais Kikwete alisema Serikali ya Tanzania inasikitishwa na kufedheheshwa namauaji ya albino nchini na itafanya kila linalowezekana kukomesha mauaji hayo.

"Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo" alisema Rais.

Katika kikao hicho, viongozi hao waalbino nchini walisoma risala ambayo ilitoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda Kamati ya Pamoja, ambayo itajumuisha Serikali, viongozi wa watu wenye albino, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu na mkakati wa pamoja, ambao hatimaye mauaji hayo kukomeshwa nchini.

Rais alisema Kamati ya Pamoja inatarajiwa kukamilika wiki hii na alisisitiza kuwa kamati hiyo ya pamoja, itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya watu wenye albino.

Aidha, katika hotuba yake kwa Taifa ya mwisho wa mwezi Februari mwaka huu, Rais Kikwete alisema anaungana na Chama cha Albino Tanzania, kulaani ukatili dhidi ya albino na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huo wasakwe, wakamatwe, wafikishwe mahakamani na kupewa adhabu kali.