MWANAFUNZI AUAWA NA BABA YAKE BAADA YA KIPIGO

Mwanafunzi aliyefahamika kwa jina la Alson Kibona (17) mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Nsemlwa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi ameuwawa baada ya kupigwa kichwani na mpini wa koleo na sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi kwa kosa la kutokwenda shuleni.

Kaimu kamanda wa jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi Rahid Mohamed alimtaja mzazi anayetuhumiwa kumuuwa mwanae kwa kumpiga na mpini wa koleo kuwa ni John Kibona(35) mkazi wa mtaa wa Nsemulwa Mjini hapa Alisema tukio hilo la mauwaji ya mwanafunzi lilitokea hapo juzi majira ya saa tisa usiku nyumbani kwa mtuhumiwa katika mtaa wa Nsemulwa

Kwa mujibu wa Rashid Mohamed Siku hiyo ya tukio marehemu Alson alikuwa amelala chumbani mwake ndipo baba yake alipomwamsha na kuanza kumuoji kwanini amekuwa na tabia ya utoro wa mara kwa mara wa kutokwenda shuleni.

Mohamed alisema ndipo mtuhumiwa alianza kumpiga marehemu kwa kutumia mpini wa koleo kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake huku akiwa akimkanya kwa maneno kuwa aache tabia ya utoro wa shuleni.

Alisema marehemu baada ya kuona kipigo kimemzidia alianza kupiga mayowe ya kuomba msaada hata hivyo mtuhumiwa hakujali aliendelea kwa kumpa kichapo mwanae huyo.

Siku iliyofuata marehemu aliamka huku akiwa na maumivu makali katika sehemu mbalimbali za mwili wake hari ambayo ilimlazimu ashindwe hata kwenda shule na mtuhumiwa hakujali wala kumpeleka kwenye matibabu Kaimu Kamanda Rashid Mohamed alieleza siku hiyo ilipotimia majira ya saa sita marehemu alikwenda kisimani kuteka maji ya kuoga ambapo alipoinama ili achote maji damu zilianza kumtoka mdomoni na puani na kisha kuanguka chini pembezoni mwa kisima hicho.

Alisema majirani waliokuwa karibu na eneo hilo walimchukua marehemu na kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa ajiri ya kupatiwa matibabu.

Alifafanua wakati akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali hiyo alifariki Dunia kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata kutokana na kipigo alichokuwa amekuwa amekipata Baada ya mtuhumiwa kupata taarifa kuwa mwanae amepelekwa Hospitali na wakati akiwa anapatiwa matibabu amefariki Dunia aliamua kutoweka na kukimbilia sehemu kusiko julikana

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu na uongozi wa mtaa linamsaka mtuhumiwa ili kumkamata na awezekujibu tuhuma inayomkabili.

Aidha kaimu kamanda wa jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kutumia nguvu kwa kuwapiga watoto wao na badala yake wawaelimishe na kuwaeleza umuhimu wa elimu ili kuepuka matukio mbaya ya nanma hii ndani ya jamii.