Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Henry Mwaibambe alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi katika kijijicha Kyota kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani humo baada ya jeshi hilo kuweka mtego kwa watuhumiwa hao ambao walikuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Rutozi (66) mkazi wa Kimwani ambaye ndiye aliyekuwa anahifadhi viungo hivyo na Emanueli Kaloli (50)ambaye pia ni mkazi wa Kimwani aliyekuwa anatafuta mteja wa viungo hivyo.
Alisema mara baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanauza viungo hivyo kwa Sh milioni 3 waliweka pesa za mitego na kujifanya wao ni wateja na ndipo walipowakamata watuhumiwa hao wawili ambao walikutwa na mfupa mmoja na walipowabana zaidi ndipo walitoa mifupa miwili.
Alisema mnamo mwaka 2006 katikakijiji cha Rushwa kata ya Mushabago wilayani Muleba, Zeulia Jestus akiwana miaka 24 mwenye ulemavu wa ngozi (albino) alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua na ndipo watuhumiwa hao walifukua kaburi hilo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi.
Alisema pia walipotaka kujiridhisha jeshi hilo liliomba kibali mahakamani ili kufukua kaburi hilo mnamo Machi 23, mwaka huu lilipofukuliwa liligundulika kuwa viungo hivyo vimetolewa katika mwili wa marehemu huyo.
Aidha, jeshi hilo linamtafuta mganga wa jadi aitwaye Mutalemwa Revocatus ambaye ametoroka kabla hajakamatwa ambaye ndiye aliyewashawishi wafukue hilo kaburina kuwapa dawa ya kinga ili wasidhurike wakati wanafukua.
Aliongeza kuwa mnamo mwaka 2008 wananchi wa kata hiyo ya Mushabago walitoa taarifa kwa Jeshila Polisi kuwa kaburi alilozikwa marehemu Zeulia lilifukuliwa na watu wasiojulikana baada ya kugundua tukio hilo.