Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuhudhuria
mkutano wa tisa wa nchi zilizoungana kutekeleza Miradi ya Miundombinu
Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects uliofanyika jijini
Kigali, Rwanda, akisema ni hatua muhimu katika kufungua utekelezaji wa
miradi ya miundombinu katika kanda nyingine za EAC.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa
Rais Kikwete alihudhuria kikao hicho kwa mwaliko wa Rais Kagame na
kwamba mkutano huo ulifanyika kwenye Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Naye Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kuwa ni
jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete ameweza kuhudhuria mkutano wa
jana kwa sababu sasa njia imefunguka kuanza kazi ya utekelezaji wa
miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central Corridor unaokatisha katikati ya
Tanzania.
Marais Kagame na Kenyatta walikuwa wanazungumza
wakati wa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika zaidi ya saa
mbili baada ya Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi za
Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda. Mbali na nchi hizo, Burundi na Sudan
Kusini pia zilialikwa kwenye mkutano huo kujadili hatua za utekelezaji
wa miradi mbalimbali kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano
wa nane uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana Marais hao
wawili wamekuwa wakitofautiana katika suala la waasi wa Rwanda baada ya
Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na waasi wa Rwanda ili
kumaliza tofauti zao zinazosababisha maisha ya watu kupotea.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda wakati
akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika
mapema mwaka jana mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukijadili
suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Ukanda
wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa
Uganda na Joseph Kabila (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na
waasi wanaopingana na Serikali zao. Akizungumza katika hotuba yake ya
kila mwezi Rais Kikwete alisema: “Ushauri ule niliutoa kwa nia njema
kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia
ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.
Rwanda imekuwa ikiituhumu Tanzania kuwa
inashirikiana na waasi hao na mara kadhaa magazeti ya nchi hiyo
yameripoti taarifa kuwa viongozi wa waasi wa nchi hiyo wamekuwa wakija
nchini.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi