MSHINDI WA URAIS KUTANGAZWA

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Nigeria INEC, Attahiru Jega, amesema kuna uwezekano wa kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa rais nchini humo ifikapo leo jioni kama zoezi la kuhesabu kura litamalizika mapema.

Jega amesema kuwa jumuiya ya kimataifa inaweza kuipongeza Nigeria jinsi ilivyoendesha uchaguzi mkuu.

"Tuna amini zoezi la kupiga kura limeenda vizuri ingawa kumekuwepo na changamoto mbalimbali lakini hatuwezi kuzipuuzia.
Ni hakika haukuwa muda kamilifu lakini tunaaminikwa ujumla tumefanya vizuri, japokuwa bado tunayo nafasi ya kuzidi kuboresha upigaji kura. Ndiyo maana tuliwaalika waangalizi vikiwemo vyombo vya habari na waangalizi wengine wa uchaguzi, ili kuweza kutangaza habari za uchaguzi na tunaweza kujifunza kutokana na ripoti zitakazotolewa na vyombo hivi pia tunaweza kuendelea kuboresha mchakato wa uchaguzi", amesema Jega.

Upigaji kura umeendelea kwa siku mbili kutokana na kutokea hitilafu katika kadi za kielektroniki na kuchelewesha usajili kwa baadhi ya wapiga kura.

Matokeo ya awali yamepangwa kutangazwa ndani ya saa 48 baada ya uchaguzi.