TCRA: KUFUNGIA MITANDAO YA KIJAMII,RADIO, TV ZINAZOKIUKA MAADILI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema iko mbioni kuifungia mitandao ya kijamii, redio na televisheni inayokiuka maadili ya Mtanzania.

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Innocent Mungy, alisema kuwa mitandao hiyo ni pamoja na facebook, whatsapp na instagram.

Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo kutokana na kuwapo kwa watumiaji wengi wa mitandao hiyo katika kuelekea Siku ya Mawasiliano duniani inayofanyika Machi 15, kila mwaka.

Mungy alisema kuwa Mamlaka hiyo inafanya utafiti ili kubaini mitandao inayoongoza kwa kulalamikiwa na wateja ili hatua zichukuliwe.

"Tangu TCRA iwezeshe kuwa na wingi wa simu na kuwezesha kuwepo kwa mitandao mingi ya kijamii changamoto zimeongezeka, maadili yameporomoka tofauti na miaka ya nyuma wakati kuna redio moja tu maadili yalizingazitiwa, kwasasa utasikia lugha za matusi kwenye radio ikiwa ni pamoja na vipindi visivyofuata maadili na kanuni za habari, tuna mpango wakuifungia mitandao hiyo na vyombo vya habari visivyokidhi mahitaji," alisema.

Alisema kuwa Mamlaka hiyo lengo lake ni kuwezesha Watanzania kwenda na wakati na kuelewa mambo mengi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na kupata habari ndani na nje ya nchi na kuongeza ajira kwa Watanzania kama ilivyo kwenye makampuni ya simu.

Aliwataka wamiliki wa mitandao kufuata maadili ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, wazazi, kuwafundisha wananchi na waumini wao kuwa na maadili ili kuondoa upotofu huo ambao unaweza kugeuza kizazi kisichofuata maadili na wengine kukosa ajira kutokana na kutumia mitandao vibaya.

Aidha, alifafanua kuwa utumiaji wa simu kwa Tanzania ulianza mwaka 1962 zikiwa ni simu zenye uzito wa kilo tatu na mwaka 1990 ndipo zilipoingia simu za ujumbe mfupi nazo hazikuwa na matatizo ya kuporomoka kwa maadili.

Alisema utafiti uliofanyika kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii unaonyesha watumiaji wanaingia bila kusoma masharti yakuingia ambapo mitandao hiyo inatoa onyo la kutokurusha picha chafu au za mtoto chini ya miaka mitano.

Alisema watumiaji wa simu wanafikia milioni 32,000,000 wakati vyombo vya utangazaji vimeongezeka na kufikia 123 ikiwa ni pamoja na televiasheni 28 na redio 95.

Changamoto ni kwa watumiaji kutumia mitandao kwa njia salama ikiwa ni pamoja na kujali afya za watumiaji na kuondoa uhalifu.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI