MAUFI AHUKUMIWA JELA MIAKA MITANO KWA KUUA BILA KUKUSUDIA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga imemhukumu aliyekuwa Katibu wa Mwenezi na Itikadi wa CCM Mkoa wa Rukwa, Patrick Maufi (48) kifungo cha miaka mitano jela kwa kumuua mpenzi wake bila kukusudia kwa wivu wa kimapenzi.

Alikutwa na hatia ya kumuua Ntuli Mwakibinga (40) ambaye alikuwa mhudumu wa afya katika Hospitali ya Mkoa, Mjini Sumbawanga.

Mshitakiwa alitiwa hatiani kwa kumuua mpenzi wake huyo mwaka 2011.

Mwanasheria wa Serikali, Fadhil Mwandoroma alimweleza Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kakusulo Sambo kuwa usiku wa manane wa Septemba 5, 2011 mshitakiwa alimuua mpenzi wake katika eneo la Kristu Mfalme mjini hapa.

Upande wa mashtaka uliita mahakamani mashahidi wanne ambao hawakuweza kutoa ushahidi wao baada ya mshitakiwa kukiri kosa. Mwanasheria wa Maufi, Boniventura Chambi aliomba mahakama hiyo isitoe adhabu kali dhidi ya mteja wake.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, usiku huo wa tukio, mshitakiwa alimpiga na kumjeruhi vibaya mpenzi wake huyo sehemu mbalimbali za mwili, ikiwa ni pamoja na kumnyofoa nywele zake na kumsababishia kifo. Uchunguzi wa kitabibu ulibaini Ntuli alivuja damu nyingi kwenye ubongo na shingo ilivunjika.

Mshitakiwa katika utetezi wake, alidai mkewe wa ndoa alifariki dunia 2010 na kumwachia mzigo mkubwa wa kulelea watoto watano. Alidai watoto wanne ni wa marehemu mkewe na mwingine ni ndugu ambao wote wanamtegemea.

Alidai alishakaa rumande miezi 22 kabla ya kupewa dhamana baada ya shitaka lake la kuua kubadilishwa kuwa la kuua bila kukusudia.

Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, alisema baada ya kuzingatia utetezi wa mshitakiwa inawezekana kweli ameachiwa mzigo mkubwa wa watoto wanaomtegemea, lakini pia kwa upande mwingine, marehemu pia alikuwa akitegemewa na taifa kitaaluma, rafiki na familia yake.

Chanzo: Habari leo