Watu hao wanadaiwa kuingia katika taasisi hiyo mwendo wa saa kumi asubuhi wakati ambapo waislamu walikuwa wakifanya sala yao ya alfajiri.
Hatahivyo maafisa wa polisi wanasema kuwa shambulizi hilo lilifanyika mwendo wa saa kumi na moja unusu.
Mwandishi wa BBC mjini humo anasema kuwa walinzi wawili waliuawa katika lango la chuo hicho huku maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda chuo hicho pamoja na wanafunzi wakijeruhiwa.
Walioshuhudia wanasema kuwa kumekuwa na majeruhi mengi ndani ya chuo hicho.
Mwandishi wetu anasema kuwa wapiganaji hao bado wako ndani ya chuo hicho na wamewateka nyara watu kadhaa.
Jeshi la Kenya KDF ,maafisa wa polisi na magari ya ambulance yamewasili katika eneo la tukio ambapo kumekuwa na ufyatulianaji wa risasi.
Jeshi la Kenya KDF ,maafisa wa polisi na amabulansi wamefika katika eneo la tukio na sasa wameingia ndani ya majengo ya chuo hicho ambapo kumekuwa na ufyatulianaji wa risasi kati ya washambuliaji na maafisa wa jeshi.
Wanafunzi 27 wamefanikiwa kutoroka na sasa wako katika kituo kimoja cha kijeshi.
Kufikia sasa hakuna kundi ambalo limekiri kutekeleza shambulizi hilo ijapokuwa kundi la wapiganaji wa Somalia Al Shabaab limeshukiwa kutekeleza shambulizi hilo.
Chuo hicho ndio taasisi ya kipekee ya masomo ya juu katika eneo hilo kilichofunguliwa mwaka 2011 na kiko takriban kilomita 350 kutoka mji mkuu wa Nairobi.