Licha ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, mwingine ameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira baada ya kumshambulia na kumkata kwa jambia shingoni askari polisi mwenye namba F. 3323 Koplo Nassoro.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha jana na kusema watu hao walikamatwa juzi majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha Nyandeo, Kijiji cha Chicago, kata na tarafa ya Kidatu, wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Hata hivyo, alisema Polisi walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa mashaka.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, waumini wote walitakiwa kutoka nje ya msikiti wakiwa na mabegi yao, nandipo katika ukaguzi na upekuzi huo walifanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na milipuko hatari.
Hata hivyo, alisema kukamatwa kwao ni baada ya Polisi kupokea taarifa za siri zinazohusu watu hao kujihusisha na vitendo vya uhalifu na pia alimtaja aliyefariki katika tukio hilo kuwa ni Hamad Makwendo mkazi wa Manyasini, Ruaha wilayani Kilombero ambaye ndiye anadaiwa kuwa mwenyeji wa watuhumiwa hao wengine.
Akielezea zaidi alisema, baada ya kupokea taarifa hizo, Polisi ilifuatilia na kwamba, katika ufuatiliaji huo waliona pikipiki mbiliza matairi matatu aina ya Bajaj zikielekea katika mji wa Mkamba eneo la wilaya ya Kilombero ambazo ziliwapotea na baada ya kitambo kidogo, Bajaj hizo zilirudi tena zikiwa na abiria mmoja.
Alisema, Polisi waliokuwepo eneo hilo walisimamisha bajaj moja na iliposimama, mtu mmoja akiwa na jambia mkononi aliruka kwenye bajaj na kuanza kukimbia ndipo askari walipoanza kumkimbiza.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mtuhuyo alipogeuka alimshambulia kwakumkata na jambia shingoni askari mwenye namba F. 3323 Koplo Nassoro na ndipo askari mwenye namba E. 9245 Koplo Chomola alipompiga risasi ya mguuni upandewa kulia mtuhumiwa huyo.
Alisema wananchi walifika eneo la tukio na baada ya kuona askari ameumizwa ndipo walipomchoma moto mtuhumiwa na kusababisha kifo chake.
Alisema baada ya tukio hilo, taarifa zilifikishwa mkoani na ndipo Polisi mkoa walikwenda eneo la tukio wakiwa na timu ya askari na kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo ndipo walipokamatwa watuhumiwa zaidi ya tisa waliokutwa ndani ya Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, vitu vilivyokutwa katika mabegi hayo ni pamoja na milipuko 30 aina ya 'Water Explosive Gel', bendera nyeusi yenye maandishi ya Kurani na Kiswahili yenye maneno Mungu Mmoja; nyaya, majambia, bisibisi, nguo za jeshi, misumeno yachuma, spana piperange, madaftari na vitabu mbalimbali vikiwemo vya risiti.
Vitu vingine walivyokutwa navyo ni vifaa vya kuficha uso 'mask' na kitambulisho kimoja chenye jina la Ramadhani Hamis kinachojieleza ni Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hata hivyo, alisema kwa mtuhumiwa aliyeuawa na wananchi alikutwa na risasi sita kati ya hizo tano zikiwa za bunduki aina ya SMG na risasi moja ya bunduki aina ya Mark IV, pamoja na nyaya mbili za umeme zikiwa kwenye mfuko mdogo wa kijeshi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa ambapo askari aliyekatwa na jambia shingoni amelazwa Hospitali ya Kiwanda cha Sukari Kilombero na hali yake inaendelea vizuri.