NEC YASEMA BVR 1600 KUWASILI MUDA WOWOTE

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema vifaa BVR Kts 1,600 vinatarajiwa kuwasili wakati wowotekuanzia leo.

Kadhalika, Nec imesema itatoa ratiba ya uandikishaji kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR), kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara, Iringa na Ruvuma.

Mikoa hiyo ni yenye watu 4,809,428kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na kati yao watu 2, 599,205 ndiyo wenye sifa ya kupiga kura hadi kufika siku ya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva (pichani), alisema aliliambia NIPASHE kuwa baada ya vifaa hivyo, 248 vilivyowasili hivi karibuni na 250 vilivyokuwa vinatumika mkoani Njombe, vitatumika kwenye mikoa hiyo kwa pamoja.

Aidha, alisema ratiba ya uandikishaji kwenye mikoa hiyo itatolewa wakati wowote wiki hii ili kuwafanya wananchi wa maeneo husika kujitokeza kwa wingi kushiriki.

Jaji Lubuva alisema Nec ina uhakika wa kuandikisha Watanzania wenye sifa ya kupiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura hadi Julai, mwaka huu na kwamba uchaguzi mkuu ni lazima ufanyike.

Akizungumzia uwezekano wa kugawanywa kwa majimbo na kata za uchaguzi, alisema utaratibu huo ni wa kawaida na unafanyika kila mwaka wa uchaguzi mkuu.

"Kwa sasa tunaangalia maeneo ya utawala wa serikali, mipaka na kujua kama kuna ongezeko la mgawanyo wa maeneo ndipo tuweze kutangaza maeneo mapya ya uchaguzi," alisema.

Alisema kwa sasa wako kwenye mchakato na wakati wowote baada ya kukamilisha watatangaza kama kuna ongezeko la maeneo ya uchaguzi kwa ngazi ya kata na majimbo.

CHANZO: NIPASHE