MARUBANI WAZIKUNJA KWENYE CHUMBA CHA KUONGOZEA NDEGE

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati dunia bado ikiwa na kumbukumbu mbaya ya ndege yashirika la ndege la Ujerumani na vifo vya abiria 150 ndaniye,kituko kingine kimegubika tasnia ya urubani baada ya marubani wawili kuondolewa kwenye zamu ya urushaji ndege kufuatia madai yawawili hao kuzikunja katika chumba cha kuongozea ndege.

Marubani hao hurusha ndege za shirika la ndege la India, Air India walishushwa katika ndege yao baada ya rubani msaidizi kumshambulia captain wake ama nimwite rubani kiongozi.

Hata hivyo ili kulinda hadhi ya shirika la ndege la India, maafisa wa juu wa shirika hilo walidai kuwa marubani hao wawili walirushiana maneno na hawakuingiana mwilini.

Msemaji wa shirika hilo la ndege amedai kwamba marubani hao wawili wote waliondolewa kwenye zamu zao na maswali tele yaligubika msuguano wa marubani hao,na kitengo cha nidhamu cha shirika hilo la ndege kilipewa jukumu mara moja kuwaketisha marubani hao kujua chanzo cha sintofahamu hiyo na hatimaye kuyamaliza.

Lakini askari wa ngazi za juu nchini India wamedai kwamba chanzo cha mzozo huo kilianzia pale Rubani kiongozi alipomtaka rubani msaidizi kurekodi mwenendo wa ndege hiyo ikiwemo idadi ya abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo kabla haijaanza safari yake.

Ndege hiyo inadaiwa ilikuwa ifanye safari kutoka Delhi kuelekea Jaipur na baada ya kutua salama wafanyakazi wa ndege hiyo waliarifiwa juu ya tukio hilo.

Tukio hili limekuja siku chache tubaada ya rubani wa shirikisho la ndege za kukodi nchini India kumuandikia waraka mkurugenzi kuu wa mamlaka ya anga nchini humo akielezea msongo wa mawazo unavyowatesa marubani.

Katika barua hiyo rubani huyo alielezea namna marubani wanavyozongwa na mambo na chanzo ni mishahara midogo, masuala ya kifamilia, hayo ndo baadhi aya vyanzo vya matatizo yanayozonga vyumba vya marubani.

Kwa taratibu za mamla za anga rubani anapaswa kuwa mtulivu kwa namna yoyote,na inawezekanaje rubani wa shirika la ndege la India afanye kazi wakati akiwa amevurugwa?