WAKIMBIZI 152,572 WAPATIWA VYETI VYA URAIA

Waliokuwa wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania zaidi ya 152,572 walioingia nchini humo tangu mwaka 1972, wamekabidhiwa vyeti vya uraia wa Tanzania na kuwa huru kuishi kama Watanzania wengine.

Wakimbizi hao walikuwa wameomba uraia wa Tanzania mwaka 2008 na kupewa na waziriwa mambo ya ndani mwaka 2010, sasa ni halali kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo za udiwani na ubunge.

Akizungumza wakati wa ugawaji wa vyeti hivyo, mkuu wa makazi ya Mishamo, Frederick Nisajile alisema ugawaji wa vyeti hivyo ulianza Novemba 24 mwaka 2014 katika makazi ya Katumba mkoani Katavi magharibi mwa Tanzania ambako watu 56,554 walipewa vyeti vya uraia na baadaye kuhamia katika makazi ya Ulyankulu mkoani Tabora, magharibi mwa Tanzania ambako wakimbizi 43,453 tayari wamepewa vyeti hivyo.

Kwa upande wake msemaji wa wizara ya mambo ya ndani, Isaack Nantanga amesema hatua ya Tanzania kuwapa uraia wakimbizi hao ni kutokana na hiyari yao na kwamba serikali ya Tanzania ilishauriana na Burundi na hatimaye kukubaliana wapatiwe uraia wanaotaka wa kuwa Watanzania.

Hata hivyo si mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa uraia kwa wakimbizi wanaoishi Tanzania kwa muda mrefu.

Tanzania imefanya hivyo kwa wakimbizi waBurundi na Somalia ambao wameishi Tanzania kwa miaka mingi.