RAIS KIKWETE AKANA NJAMA ZA KUMMALIZA DK.MENGI

RAIS Jakaya Kikwete ameshtushwa na taarifa za kuhusishwa na mikakati ya kummaliza Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi. Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya Dk. Mengi kudai kuwa kiongozi huyo wanchi ameapa kupambana naye kama ilivyoripotiwa na moja ya magazeti ya kila wiki nchini.

Kauli ya Rais Kikwete ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa waandishi wa habari.

Madai ya Dk. Mengi yalitokana na taarifa za gazeti hilo, zikidai kuwa Rais Kikwete aliyasema maneno hayo baada ya kukutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye alimweleza mkakati wa mfanyabiashara huyo wa kutaka kupambana naye baada ya kung'atuka madarakani.

Baada ya maelezo aliyotoa katika hotuba yake, waandishi walitaka kujua msimamo wa Ikulu juu ya madai ya Dk. Mengi, ambapo Rweyemamu alisema: "Wakati niko Jordan ndio tulipata habari kuwa mzee Mengi amesema hayo aliyosema, kila mtu akiwapo rais alishangazwa sana na kauli hiyo." Alisema kwa muda mrefu Rais Kikwete hajafanya kikao chochote na Zitto wala kuwasiliana naye kwa njia ya simu. "Hata wakati wa Escrow hakuwasiliana naye kwa sababu alikuwa nje ya nchi," alisema Rweyemamu.

Alisema Dk. Mengi ana mawasiliano ya Rais Kikwete na ni marafiki, hivyo ilitarajiwa baada ya kupata taarifa hizo angewasiliana naye.

Rweyemamu alisema hivi sasa kunauzushi mwingi nchini, hivyo siyo jambo jema mfanyabiashara huyo kusikiliza maneno ya watu kwani kufanya hivyo atakosana na watu wengi. Aprili 15, mwaka huu Dk. Mengi alituhumiwa kutaka kuiangusha Serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza uongozi wake Oktoba, mwaka huu.

Dk. Mengi alisema habari hiyo imempa hofu kubwa juu ya mustakabali wa maisha yake kutokana na kile kilichoandikwa kuwa Kikwete aliapa atapambana naye. "Hofu yangu kubwa inasababishwa na Ikulu na Maelezo kwa kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi. "Ikulu na Maelezo wako makini katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu Rais Kikwete, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa," alisema Dk. Mengi.

Aprili 18, mwaka huu naye Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema watu waliotajwa katika wizi wa fedha za Escrow wasitapetape kutafuta mchawi wakati wao ndio wezi wenyewe.

Kutokana na hali hiyo amesema suala la kumuhusisha mfanyabishara huyo kuwahonga wabunge ili kuishughulikia Serikali ni sawa na porojo. Kauli hiyo aliitoa mjini Shinyanga alipokuwa akihutubia ambapo alisema hatorudi nyuma katika kusimamia haki za Watanzania na kama kuna mtu ana chembe ya ushahidi wa jambo hilo apeleke kwenye vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.

JK kimya kimya Jordan Rweyemamu alisema pia kuwa Jumamosi ya juma lililopita Rais Kikwete alisafiri kwenda nchini Jordan bila kutoa taarifa kwa umma kutokana na jambo hilo kuwa nyeti hali iliyochangiwa na mazingira ya mkutano aliokwenda kuhudhuria.

Alisema Rais Kikwete alikwenda nchini humo kwenye mkutano ambao pamoja na mambo mengine walizungumzia masuala ya ugaidi ambayo kwa sasa yamekuwa tishio duniani. "Ule mkutano ulitakiwa uwe wa siri kutokana na uzoefu wa Jordan na mambo ya ugaidi na pia majirani zake ambao ni Syria, Israel, Iraq na mataifa mengine," alisema. Sheria ya mtandao Rweyemamu alisema Rais Kikwete ataisaini sheria ya makosa ya mtandao licha ya baadhi ya wadau kuipinga.

Alisema sheria hiyo ilipitia hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Lazima rais aisaini kwa sababu ilipitia hatua zote muhimu ikiwa ni pamoja na kupitishwa na Bunge," alisema Rweyemamu.