OBAMA KUIONDOA CUBA KATIKA ORODHA YA UGAIDI

Rais Barack Obama amesema ataiondoa Cuba kutoka orodha ya Marekani ya nchi zinazofadhili ugaidi duniani.

Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani imesema hatua hiyo inakuja huku kukiwa na jitihada za kujenga uhusiano kati ya Marekani na Cuba.

Uwepo wa Cuba katika orodha hiyo pamoja na nchi za Syria, Iran na Sudan kilikuwa kigezo cha Cuba katika mazungumzo yake na Marekani ya kufungua ofisi za balozi kati ya nchi hizo.

Seneta wa chama cha Republican Marco Rubio ameishutumu Ikulu ya Marekani kwa uamuzi huo, akisema kuwa Cuba bado ni taifa linalofadhili ugaidi.

"Wanawahifadhi Wamarekani ambao wanakimbia mkono wa sheria, akiwemo mtu aliyemuua afisa wa polisi huko New Jersey zaidi ya miaka 30 iliyopita," amesema Bwana Rubio, Mmarekani mwenye asili ya Cuba ambaye alizindua kampeni yake ya uchaguzi wa rais wa Marekani 2016.

"Ni nchi ambayo pia inaisaidia Korea Kaskazini kukwepa vikwazo vya silaha vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa."

Bwana Obama alitangaza tukio la kihistoria la kurejesha uhuasiano kati ya Marekani na Cuba mwezi Desemba 2015 lakini vikwazo vya kibiashara vya Marekani dhidi ya Cuba vinabakia, na vinaweza kuondolewa tu na baraza la Congress.