WEZI WA MTANDAO WAIBA DOLA BILIONI 1

Genge la wezi wa kompyuta limefanikiwa kuiba takriban dola bilioni moja kutoka kwenye akaunti za wateja wa mabenki 100 katika mataifa 30.

Kampuni inayosimamia usalama wa programu ya kompyuta inayohakikisha data ya wateja iko salama Kaspersky Lab imesema katika ripoti yake maalum.

Ripoti hiyo inaelezea mbinu mpya ya wezi wa Kompyuta wanaotumia mbinu mpya ya kudakua nambari za akaunti za wateja za siri kabla ya kuingia na kupora pesa.

Kaspersky imesema kuwa wizi huo ulianza mwaka wa 2013 na bado unaendelea hata leo kwani mabenki yote yalioathirika hayana uwezo wa kuwazuia wezi hao.

Hadi kufikia sasa ripoti hiyo inadai kuwa takriban dola bilioni moja zimeporwa kutoka kwenye akaunti za wateza.

Genge hilo la wezi, lililoanzia shughuili yake nchini Urusi, Ukraine na pia Uchina ndilo linalo laumiwa kwa wizi huo.

Kampuni hiyo ya Kaspersky inasema inafanya juhudi za kuzima wizi huo kwa ushirikiano na polisi wa kimataifa Interpol na polisi wa bara ulaya Europol.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mabenki katika mataifa 30 yakiwemo, Russia, Marekani , Ujerumani , Uchina, Ukraine na Canada yameathirika pakubwa.

Wezi walitumia programme ya kipekee

Kamanda wa kikosi cha polisi wa kimataifa Interpol bwana Sanjay Virmani, amesema kuwa wezi wataendelea kutumia upungufu wa miundo msingi katika sekta ya uchumi wa mataifa husika hadi pale kutaibuka umoja wa kuzuia mapengo.

Kaspersky hata hivyo inasema kuwa genge hilo linalenga mabenki bila ya kuwaibia watu binafsi.

Genge hilo kwa jina Carbanak, linatumia mbinu ya kuambukiza virusi kwenye mashine za benki ikiwemo kamera za CCTV ilikunakili kila kitu kinacho andaliwa kwenye kompyuta.

Kutokana na uweledi wao genge hilo lilituma pesa kwenye account zao huku wengine wakiamrisha mmitambo ya kutoa pesa ATM kumimina pesa bila kikomo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kila tukio la wizi lilihusisha takriban dola milioni kumi.