Habari kutoka ndani ya chuo hicho zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa kabla ya Kilungi kuchota fedha hizo Februari 7, mwaka huu, mwanzoni mwa Januari alichota tena Sh12 milioni katika akaunti hiyo kwa ajili ya safari ya Bunge la wanafunzi lililotembelea vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kwanyakati tofauti, kuanzia Oktoba 2, mwaka jana hadi Januari 26 mwaka huu, Bunge la wanafunzi limekuwa likiuandikia barua utawala wa chuo hicho kutaka ufafanuzi wa matumizi ya fedha na kushinikiza vifanyike vikao, lakini utawala ulizuia.
Akizungumza na gazeti hili jana,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki alisema kwa sasa Kilungi yuko nje kwa dhamana na uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili unaendelea.
"Kwa sasa yupo nje kwa dhamana na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani," alisema Nzuki.
Kilungi alipotafutwa na gazeti hili jana, mazungumzo yalikuwahivi;
Mwananchi: Pole kwa matatizo yaliyokupata.
Kilungi: Asante.
Mwananchi: unazungumziaje tuhuma zinazokukabili, je ni kweli kuwa ulichukua fedha kinyume na utaratibu.
Kilungi: Kata simu nitakupigia baada ya nusu saa.
Baada ya kupita muda huo, rais huyo hakupiga simu, hata alipopigiwa simu yake iliita tu bila majibu.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Uhusiano wa Chuo hicho, Leonidas Tibanga aliliambia gazeti hili kwa kifupi kuwa uongozi wa CBE hauwezi kushirikiana na wanafunzi kufanya udanganyifu wowote kwa sababu fedha hizo ni zao nasiyo za chuo.
Tibanga ambaye kabla ya kutoa ufafanuzi wa kina alikata simu, hata alipotafutwa kwa zaidi ya mara tano hakupatika.
Awali, alisema huenda mvutano huo unatokea kwa sababu ya kukaribia kwa uchaguzi wa Serikali ya wanafunzi ya chuoni hapo.
"Unajua wanafunzi nao wana siasa zao. Huwezi kusema kuwa CBE kuna mgogoro. Kilichofanyika ni mwenzao mmoja kutuhumiwa kuchukua fedha kinyume na utaratibu. Zile fedha ni zao na wao ndiyo wanaojua wanazitumia vipi," alisema.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Ramadhani alikuwa akizuia vikao vilivyokuwa vikiitishwa na Bunge la Serikali ya wanafunzi kwa kushirikiana na utawala, kuweka mkakati wa kuwaondoa wabunge wa bunge hilo walio onekana kuwa mstari wa mbele kuhoji matumizi mabaya ya fedha.
"Kila mwanafunzi wa CBE huchangia Sh12,000 kila mwakakwa ajili ya kugharamia shughuli mbalimbali zinazowahusu wanafunzi. Jumamosi iliyopita ziliingia Sh32 milioni, baada ya siku tatu Ramadhani alikwenda Benki na kutoa fedha hizo bila kufuata Katiba ya Serikali ya wanafunzi,"zilieleza habari hizo.
Ziliendelea kudai kuwa Ramadhani na mshauri wa wanafunzi (Deen of Student) ndiyo walikuwa wakitia saini ili kutoa fedha benki, lakini baada ya kuongezeka kwa utolewaji wafedha kiholela, mshauri huyo alijitoa.
"Alichokifanya Ramadhani ni kwenda benki na kufoji sahihi ya mshauri wa wanafunzi na kuchukua fedha. Tuliandaa mtego kupitia Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi na kumkamata akiwa na Sh 16 milioni, nyingine aliwapa alioshirikiana nao wakiwamo baadhi ya wanafunzi," zilieleza habari hizo.
Kuhusu Sh12 milioni zilizotolewa kwa ajili ya safari ya bungeni Dodoma, habari hizo zilidai kuwa wanafunzi waliotakiwa kwenda bungeni walikuwa 59, lakini walienda 24 huku idadi iliyobaki ikijazwa na watu ambao hawakuwa wanafunzi wa chuo hicho.
"Wanafunzi walitakiwa kulipwa posho ya Sh150,000 kwa siku tatu walizokaa Dodoma, ila cha ajabu walilipwa Sh50,000 kwa siku tatu," zilidai taarifa hizo.
Chanzo: Mwananchi