WATU WATATU WAFARIKI, 18 WAJERUHIWA WAKATI WAKIJARIBU KUIBA MAFUTA

Watu watatu wamefariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuiba mafuta kutoka kwenye lori la kusafirisha mafuta aina ya petroli ambalo limepinduka na baadaye kulipuka na kuwaka moto katika kijiji cha Idweli eneo la Number One, wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.

Lori hilo lenye namba za usajili T 891AQZ likiwa na tela lake lenye namba za usajili T 821 ARF mali ya Ailis Sanga ambalo lilikuwa likisafirisha mafuta aina ya petroli kutoka Dar es Salaam kwenda nchini Malawi limefeli breki katika mteremko mkali wa eneo hilo na kupinduka majira ya saa nne usiku.

Baada ya lori hilo kulipuka wananchi wakatoboa matenki ya mafuta ya lori hilo hali ambayo ilisababisha mafuta kutiririka na kusambaa kuelekea kwenye makazi ya watu ambako inadaiwa mama mmoja aliwasha kibatari kilichosababisha moto kulipuka na kupelekea lori hilo kuteketea kwa moto.

Moto huo pia umesababisha maafa kwa watu waliokuwa wakiiba mafutana wale waliokuwa jirani na eneo hilo.

Baadhi ya majeruhi wa moto huo wamesema kuwa tukio hilo lilikuwa ni ghafla kiasi kwamba haikuwa rahisi kwao kujiokoa.

Akizungumza kwa tabu akiwa katika hospitali ya misheni ya Igogwe, dereva wa lori hilo amesema aliwaonya wananchi wasithubutu kuiba mafuta lakini baada ya yeye kukimbizwa hospitali wananchi walianza kuiba mafuta na ndipo moto uliporipuka.

Mganga mkuu wa hospitali ya misheni ya Igogwe, Tauryeti Wakosya amethibitisha kupokea majeruhi 15 lakini mmoja kati yao ambaye ni utingo wa lori hilo alipoteza maisha wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Hilo ni tukio la pili la watu kupoteza maisha wakati wakiiba mafuta kutoka kwenye lori lililopata ajali kijijini hapo, ambapo mwishoni mwa miaka ya 90 watu zaidi ya 20 walipoteza maisha wakiiba mafuta.