TOTO AFRIKA NA MWADUI ZATIMIZA NDOTO ZA KUKWEA LIGI KUU

Ndoto ya Oljoro JKT kupanda daraja zimezimika baada ya Mwadui na Toto African kushinda mechi zake na kufuzu kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Oljoro ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tabora na kufikisha pointi 44, ilikuwa ikiomba Mwadui au Toto wapoteze mechi zao jambo ambalo halikutokea.

Mshambuliaji Jafari Mohamed alifunga mabao mawili na kuiongoza Toto African kuichapa Rhino Rangers 2-0, wakati Mwadui ikiibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Burkina Faso.

Mohamed alifunga bao la kwanza dakika ya 8, akiunganisha vizuri krosi ya William Kimanzi na kupachika bao la pili dakika ya 90 akimalizia pasi ya Hamim Karim.

Katika mchezo mwingine Oljoro JKT ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tabora. Bao la Oljoro lilifungwa na Sultan Kasikasi akiunganisha krosi ya Sino Augustino katika dakika ya 60 na kuwafanya wanajeshi hao kufikisha pointi 44.

Mwadui na Toto African zinaungana na Majimaji na African Sports kupanda Ligi Kuu.