Sasa wananchi hao wameiomba Polisi kutoa tamko, kuhusu kikundi kilichorushiana risasi na askari Polisi na kusababisha kifo cha mwanajeshi mmoja.
Aidha, wananchi hao wameitaka Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu mwendelezo wa matukio mengi ya uhalifu wa kutumia silaha, ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi, ikiwemo kutokamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo.
Hata hivyo, Msemaji wa Polisi, Advera, alisema Jeshi lake halina taarifa zaidi ya iliyotolewa juzi na Mkuu wa Opersheni wa jeshi hilo, Kamishna Paul Chagonja.
Habari za kipolisi zinasema kwambabado wanaendelea kusaka wahalifu hao huku baadhi ya vikosi vya ulinzi na usalama, vimeongezwa kwa ajili ya kupambana na wahalifu hao. Juzi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi walipambana na kundi la wahalifu katika maeneo ya mapango ya Amboni na kusababisha wanajeshi wanne na polisi wawili kujeruhiwa.
Hata hivyo, kuna habari kuwa majeruhi mmoja ambaye ni mwanajeshi alifariki baadaye akiwa hospitalini.
Habari zingine zinasema kwamba majeruhi wengine ambao ni polisi wanne na mwanajeshi mmoja, wanaendelea vizuri.
Kuhusu mwanajeshi aliyekufa, polisiwamegoma kuzungumzia suala hilo,lakini habari zinasema aliyekufa ni mwanajeshi mwenye cheo cha sajenti. Wananchi wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti jana, walipozungumzia tukio la juzi, lililosababisha mapigano ya kurushiana risasi baina ya askari na wahalifu, wanaodaiwa kuficha silaha katika eneo la Mapango ya Amboni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Walisema mpaka sasa bado hawajaridhishwa na mwenendo wa utendaji wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, pamoja na taarifa hafifu wanazotoa, kuhusu namna walivyoshughulikia tukio hilo la juzi kwenye mapango hayo ya Amboni.
Ibrahim Mshote, mkazi wa Ngamiani Kati, alisema mbali na tukio la juzi, yapo matukio mengine yakiwamo yaliyosababisha mauaji kwa raia, ambao walivamiwa na kuporwa mali na watuhumiwa kushindwa kupatikana. Alisema hakuna taarifa za mwendelezo wa kushughulikiwa kwa matukio hayo.
"Kwa mfano kuna wananchi walilipuliwa na bomu la kutupwa kwa mkono wakati wakitazama mpira kwenye kibanda cha video hapo Amboni… pia yupo mfanyabiashara wa eneo la Mkumbara wilayani Korogwe ambaye hivi karibuni alivamiwa na kuuawa kwa risasi kabla ya kuporwa mali, pia tukio la utekaji wa gari eneo la Michungwani wilayani Handeni baada ya kuwekewa magogo barabarani", alisema.
Aliongeza "Katika matukio kama hayo, tunaambiwa tu wahalifu hawakupatikana, upelelezi unaendelea, lakini ni zaidi ya wiki mbili sasa hakuna taarifa zozote zinazoonesha juhudi za mwendelezo wa kudhibiti wahalifu kama hao, badala yake matukio yameendelea kuongezeka".
Miriam Jonas, mkazi wa Barabara yaTano jijini Tanga, alisema kitendo cha askari kunyang'anywa silaha mbili za SMG zenye risasi 60 kwenye kibanda cha chipsi ni fedheha kwa kuwa vitendo hivyo vilisha sahaulika mkoani hapa.
"Tulitarajia wahusika wangekamatwa ndani ya muda mfupi, lakini wapi, Polisi hapa Tanga imeshindwa kabisa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo hadi Kamishna Chagonja alipokuja na kuzungumzia tukio la juzi", alisema.
Aidha, Mrisho Mashaka mkazi wa Kwaminchi alisema licha ya Chagonja kuwataka wakazi wa jiji la Tanga kutulia, kwakuwa hali ya usalama imeimarishwa, bado baadhi ya wananchi wanayo shaka na hofu kubwa kuhusu tamko hilo.
"Kinachoendelea kutupa hofu ni mgongano wa kauli za polisi kama tulivyosikia kwenye vyombo vya habari kwamba waliarifiwa kwamba silaha za moto zikiwemo walizoporwa askari Januari 26 zimefichwa ndani ya mapango, lakini kilichokutwa ni silaha za jadi yakiwemo mapanga, pinde na mishale na vifaa vya kutengeneza milipuko", alidai.
Alisema vifaa vilivyotajwa kukutwa kwenye eneo la tukio ni tofauti na madhara waliyopata askari, waliokuwa kwenye operesheni hiyo ya kusaka silaha hizo, ambayo yamesababisha kifo na majeraha makubwa kwa baadhi yao, ambao sasa wamelazwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Bombo.
"Binafsi bado napata kigugumizi kuelewa taarifa hii kwasababu bado inayo maswali mengi ya kujiuliza, jehao ni watu wa namna gani ambao wamefanikiwa kujeruhi vibaya askari na kisha kutoroka na silaha zilizokuwa zikitafutwa, wameelekea wapi? Je sisi tuko salama?", alihoji.
Walidai vipo viashiria vinavyoonesha kwamba hali ya ulinzi na usalama mkoani hapa, haijatengemaa kutokana na hali ya mazingira iliyobainisha kwamba wahalifu hao waliweka makazi ndani ya mapango hayo bila kubainika mapema.
Mbali ya silaha za jadi, vitu vingine vilivyokutwa ndani ya mapango hayo ni pikipiki mbili, baiskeli tatu, mavazi ya aina mbalimbali na vyakula, ambavyo ni dhahiri vinaashiria kwamba watu hao walikuwa wakijipenyeza ndani ya jamii kutafuta huduma muhimu bila kufahamika kwamba ni wahalifu.
Aidha, walisema ripoti ya hivi karibuni ya hali ya uhalifu mkoani Tanga, ambayo ilitolewa na Kamanda mwishoni mwa mwaka jana ilibainisha kuongezeka kwa makosa ya uhalifu, yanayofanywa dhidi ya binadamu kwa asilimia 2.11, ikilinganishwa na takwimu za makosa kama hayo yaliyoripotiwa mwaka 2013.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai alibainisha hayo wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hali ya ulinzi na usalama mkoani humo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Desemba mwaka jana. Kamanda alisema kwamba mwaka 2014, makosa 7, 970 ndiyo yaliripotiwa kwenye vituo mbalimbali vya Polisi wilayani, ikilinganishwa na makosa 7,805 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2013.
Wakazi hao wa Tanga walidai wanaamini kwamba takwimu hizo nikiashiria tosha kwamba mambo hayako sawa, licha ya Kamishna Chagonja kujitahidi kutoa matumaini.
Kutokana na mambo kama hayo, walisema kuna umuhimu mkubwa kwa jeshi hilo kujipanga kimkakati ili kuondoa tatizo hilo haraka kwa sababu kila siku matukio mapya yanaibuka na watuhumiwa hawapatikani.
Chanzo: Habari Leo