Maandamano hayo yaliyokuwa yafanyike leo, yalikuwa yaanzie Buguruni hadi Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ajili ya kufikisha madhumuni yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema, kutokana na mazingira yaliyojitokeza katika taarifa ya JUVICUF ni dhahiri kwamba lengo lao ni kuvunja amani.
Alisema kutokana na hatua hiyo polisi watalazimika kutumia uwezo wao kwa misingi ya sheria ili kudhibiti maandamano hayo ambayo hayana nia nzuri.
Madhumuni ya malengo hayo ni kutaka kwenda NEC kuomba siku za uandikishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ziongezwe kutoka saba hadi 14 na kulaani ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na polisi.
"Haya maandamano hayana mantiki yoyote, tuliwaita viongozi wao ambao ni Maulid Said Naibu Katibu na Masoud Said Masoud ili waongozane na Mkuu wa Upeleleziwa Kanda Maalumu kwenda NEC kupata ufumbuzi wa maoni yao. "Hakuna mantiki kufanya maandamano, tuliwashauri waende viongozi wachache kuwasilisha maoni yao na hayo masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu ni la kisheria na linashughulikiwa kwa mujibu wa sheria," alisema.
Kova alisema wamegundua maandamano hayo yatasababisha msongamano mkubwa kutokana nakuwa leo ni siku ya kazi. Barabara ambazo zingetumiwa na waandamaji hao ni Buguruni kupitia Shule ya Uhuru, Mnazi Mmoja na kuingia barabara ya Ohio hadi NEC na wizarani.
Alisema viongozi hao wa Juvicuf walikataa kwenda kwa Waziri kukata rufaa kama sheria inavyoelekeza kwa madai kuwa ni kupoteza muda. Kova alitumia fursa hiyo kuasa vijana wasijitokeze katika maandamano hayo pia wakumbuke hakuna mbadala wa amani.