APANDISHWA KIZIMBANI KWA KUMLAWITI MTOTO WAKE

MKAZI wa mtaa wa Migongo kata ya Migongo Halmashauri ya Mji wa Masasi mkoani Mtwara, Hajili Mpili(52) amepandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Masasi kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa.

Mtuhumiwa alifikishwa mahakamani hapo mwishoni mwa wiki na kusomewa shitaka na mwendesha mashtaka Suleimani Omari mbele ya hakimu Halfani Ulaya.

Mbele ya Hakimu Halfani Ulaya, Mwendesha Mashtaka Suleimani Omari alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo la kumlawiti mtoto wake Februari 5 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku akiwa nyumbani kwake huko katika mtaa wa Migongo.

Alidai kuwa mshtakiwa alimlawiti mtoto wake aliyekuwa anaishi nayenyumbani hapo baada ya mama wamtoto huyo kufariki dunia miaka mitatu iliyopita na kwamba tangu hapo mzee huyo hajawahi kuoa tena.

Suleimani alidai kuwa mtuhumiwa huyo kwa nyakati tofauti amekuwa akimlawiti mtoto huyo huku akimpa vitisho vya kwamba endapo angethubutu kutoa taarifa hizo kwa majirani, basi angeweza kuondoa maisha yake ili aweze kuepukana na aibu hiyo.

Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo alirudi nyumbani usiku akiwa amelewa na ndipo alipomvamia mtoto huyo na kuanza kumlawiti na ndipo mtoto huyo alianza kupiga makelele ya kuomba msaada lakini kwa bahati mbaya hakuna jirani hata mmoja aliyeweza kusikia sauti za mtoto huyo na alifanikiwa kukimbia na kulala vichakani.

Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa asubuhi mtoto huyo aliyekuwa ameumizwa usoni pamoja na mgongoni kutokana na kipigo alichokuwa amekipata usiku na kwamba alipoulizwa na watoto wenzake kwa nini ana majeraha aliwaeleza amepigwa usiku na baba yake alipokuwa akijaribu kujiokoa wakati akimlawiti.

Chanzo: Habari Leo