AFRIKA MASHARIKI KUPELEKA VIJANA SENEGAL

Nasry Daudi Aziz wa Tanzania amechaguliwa kujiunga na kituo cha kukuza vipaji cha Aspire Football Dream kilichopo katika mji wa Dakar, Senegal, akijumuika na vijana wengine kutoka nchi mbalimbali za Afrika ya Mashariki na kwingineko waliowahi kupata nafasi hiyo.

Kuchaguliwa kwake kunafanya jumla ya vijana wa tatu wa Tanzania waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo.

Nchi za Afrika ya Mashariki zikiwemo Kenya na Uganda ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kupeleka vijana katika mafunzo hayo ya mpira wa miguu katika miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vingine vya habari, mwaka 2013, vijana wawili kutoka Kenya Humphrey Katasi (golikipa) na Abdulrizak Mohammed (kiungo) walichaguliwa wakati wa zoezi la kuchagua vijana kutoka nchi za Afrika ya Mashariki.

Vijana kutoka Uganda walikuwa Victor Matovu, na Bashir Kagiri (Uganda).

Wakenya wengine waliowahi kuchaguliwa walikuwa Festus Omukoto, Joseph Wanyonyi na Nelson Katana.

Mbali na Aziz, vijana Watanzania wengine wawili waliochaguliwa siku za nyuma ni Matine Taganzi na Orgenes Morrel ambaye aliitwa kwenye timu ya Taifa Stars maboresho na kocha Mart Nooj.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, mradi wa Aspire ulianza mchakato wa kusaka vijana nchini Tanzania mwezi Machi - Mei, 2014 ambapo vijana wengi walijitokeza na kuchaguliwa vijana 14 ambao walikwenda katika mchujo mwingine uliofanyika nchini Uganda uliowashirikisha vijana zaidi ya 50.

Kuchaguliwa kwa Nasry kunamfanya kuwa ni miongoni mwa wachezaji 17 waliochaguliwa kati ya vijana 34 walikuwepo nchini Senegal kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo kulikuwa na vijana wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika na Amerika ya Kusini.

Kituo cha Aspire kilichopo Dakar nchini Senegal ni miongoni mwa vituo viwili vinavyoongozwa na mtoto wa mfalme wa Qatar na timu ya Barcelona, kituo kingine kipo mjini Doha.

Aziz anatarajiwa kuondoka nchini Februari 28 mwaka huu kuelekea Dakar ambapo atakua kwenye kituo hicho kwa mkataba wa miaka mitano.