MTOTO ANYAKULIWA MGONGONI NA FISI

Watu wawili wamefariki dunia mkoani Simiyu katika matukio tofauti akiwamo mtoto wa miezi mitatu aliyenyakuliwa na fisi akiwa mgogoni mwa mama yake.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Simiyu, Gemin Mushy jana alisemakuwa mtoto Ng'wanza Samwel, akiwa amebebwa na mama yake alinyakuliwa na fisi Mei 25, majira ya saa 1;30 jioni katika kijiji cha Ngugunu, Tarafa ya Kisesa wilayani Meatu.

Alisema katika kufuatilia tukio hilo, mabaki ya mtoto huyo yalipatikana mita 200 tu fisi kutoka eneo alilonyakuliwa huku kichwa, kifua, tumbo, mikono na miguu ikiwa haipo.

Katika tukio jingine mpanda baiskeli aliyefahamika kwa jina la Magina Supa(20), mkazi wa Nyaumata mtaa wa Kisiwani wilayani Bariadi, aliuawa kwa kukatwa na kitu chenyencha kali shingoni na bega la kushoto na mtu aliyekuwa amempakiza kama abiria wake.

Akifafanua, Kamanda Mushy alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 26 majira saa 1;00 jioni katika mtaa wa Izunya, kata ya Somanda tarafa ya Ntuzu wilayani Bariadi kwa mtuhumiwa wa mauaji hayo anayedaiwa kuwa abiria wa mpanda baiskeli huyo aliyekuwa anajishughulisha na biashara ya daladala ya baiskeli.

Kamanda huyo alisema kuwa mara baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa ambaye hajafahamika na anasakwa baada uhalifu huo alitoroka. Chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

ATUPWA JELA MIAKA 30 KWA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 9

Mkazi wa Malampaka mkoani Simiyu, Benedictor Bulobo (30) , ametupwa gerezani atakakotumikia kifungo kwa miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka tisa.

Alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Maswa juzi na Hakimu Mwandamizi Mfawidhi Agatha Chigulu, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Akitoa hukumu hiyo hakimu huyo alisema kuwa anatoa adhabu hiyo ilikukomesha vitendo hivyo na kuwaonya wenye nia mbaya ya kutaka kutenda kosa kama hilo wajifunze na kuacha mwenendo huo.

Chigulu alieleza kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 131 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Awali mahakama iliambiwa na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Nassibu Swedy kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 23 mwaka jana saa 5:00 asubuhi.

Alimnajisi mtoto huyo maeneo ya nyumbani kwake baada ya kumkamata kwa nguvu binti huyo mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Malampaka na kumwingiza chumbani kwake alipombaka.

Alisema mtoto huyo alipata maumivu makali baada ya kuumizwa sehemu za siri, alipiga kelele kuomba msaada na watu walifika katika eneo la tukio, kumkamata na kumfikisha Bulobo katika kituo cha polisi Malampaka.

RAIS WA NIGERIA KUAPISHWA LEO NCHINI HUMO

Mshindi wa uchaguzi mkuu nchini Nigeria Muhamadu Buhari anaapishwa leo kama rais mpya wa nchi hiyo.

Bwana Buhari ambaye ni kiongozi wa zamani wa kijeshi anachukua uongozi kutoka kwa rais wa zamani Goodluck Jonathan ambaye amemtaka kuiunganisha nchi hiyo wakati inapokabiliana na tisho kutoka kundi la Boko Haram.

Buhari anasema kuwa lengo lake ni kupambana ufisadi ambao umekita mizizi katika taifa hilo lenye watu wengie zaidi barani afrika.


Lakini je Buhari ni nani ?

Muhammadu Buhari, ni Muisilamu, mzaliwa wa Jimbo la Katsina, Nigeria kaskazini.

Alizaliwa mwaka 1942, Buhari alikuwa kiongozi wa saba wa taifa la Nigeria, baina ya mwaka 1983-1985.

Ni jenerali mstaafu aliyepata mafunzo ya kijeshi katika Nigeria,Uingereza, India, na Marekani.

Na aliwahi pia kushika nyadhifa za ugavana, kamishna wa raslimali ya mafuta, mwenyekiti wa shirika la umma la mafuta, napia mwenyekiti wa Mfuko wa Amana ya Mafuta.

Anasemekana kuwa si m-kaishi, hakubali kushindwa.

Licha ya kushindwa mara katika chaguzi tatu, amerejea kushindania tena urais, dhidi ya rais alo-madarakani Goodluck Jonathan,Mkristo, anaye toka eneo la Niger Delta, kusini Nigeria, kwa mara ya pili, katika uchaguzi wa Machi. Unaonesha kuwa mchuano mkali.

Kuambatana na mandhari ya kisiasa, Buhari si limbukeni. Kushindwa mwaka 2003 na tena 2007, alitambia matokeo ya chaguzi hizo mahakamani bila mafanikio.

Ingawaje, Buhari anazingatiwa kuwa kiongozi mwenye ufuasi mkubwa na heshima nyumbani, hususan katika rubaa za kaskazini Nigeria.

Na hii inatokana na sera zake za kupambana na ufisadi na ukosefuwa nidhamu, wakati alipokuwa mtawala wa kijeshi.

Kimataifa, Buhari pia anasemekana kuheshimiwa.

Yajulikana kwamba ni yeye na marehemu Nelson Mandela tu ndio Wafrika binafsi waloalikwa na Ikulu ya White House, Marekani, kuhudhuria sherehe zakutawazwa Barack Obama.

Kampeni ya Jenerali Buhari, ilitilia mkazo mambo kadha, miongoni mwake utawala bora, kufufua uchumi, maendeleo ya miundombinu,umeme na nishati, kilimo, elimu,afya, ardhi na usafiri, kuwezeshwa wanawake, usalama,na ajira. Ingawaje, uwili wa nafsi yake bado unazusha masuala, je ni wa kijeshi au kidemomkrasi?

ASKARI POLISI APORWA SMG KWA PANGA

Matukio ya kuvamia askari wakiwa lindoni, vituo na vizuizi vya polisi nchini yameendelea kulitafuna Jeshila Polisi na safari hii, Askari wa Kikosi cha Tazara, Jijini Dar es Salaam, ameporwa SMG na kujeruhiwa vibaya.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku saa sita kwa watu wanaosadikiwa ni majambazi wakiwa na silaha za jadi kumvamia askari huyo akiwa kwenye lindo la Tazara na kupora silaha hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, watu wawili wakiwa na silaha za jadi, nyakati za saa sita usiku walivamia eneo hilo na kupora silaha hiyo na kutokomea nayo.

Taarifa hizo zinafafanua kuwa askarihuyo alijeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili na amelazwa hospitali kwa matibabu zaidi, ingawa jina lake halikutajwa wala hospitali aliyolazwa.

Kamanda wa Kikosi hicho, Kamanda Bieteo, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa hawezi kutoa ufafanuzi kwa simu bali kwa taarifa ya maandishi.

"Tukio lipo ni kweli wamemvamia askari akiwa lindoni kumjeruhi na kumpora silaha…siwezi kutoa ufafanuzi zaidi kwa simu, leo nitatoa taarifa kwa maandishi," alisema.

Alipotakiwa kueleza zaidi alijibu kwamfupi: "Nitafute kesho (leo), nitaandaa taarifa ya maandishi, sipotayari kueleza kwenye simu."

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa, alithibitisha, lakini akamuelekeza mwandishi kuwasiliana na Kamanda Bieteo.

Januari 21, mwaka huu, usiku huko kituo cha Polisi Ikwiriri - Rufiji majambazi wakiwa na bunduki walivamia kituo cha Polisi na kuwaua askari wawili na kupora bunduki aina ya SMG 2, SAR 2, Anti Riot gun moja, Shotgun moja na risasi 60.

Machi 30, mwaka huu barabara ya Kilwa kwenye kizuizi cha Polisi eneola Shule ya Sekondari St. Mathew Kongowe kata ya Vikindu Wilayani Mkuranga, majambazi wasiofahamika wakiwa na mapanga na silaha zingine za jadi walimuua askari mmoja kisha kupora bunduki moja aina ya SMG ikiwa na risasi 30.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema idadi ya matukio ya uvamiziwa vituo vya polisi imeongezeka kutoka sita kwa mwaka 2014 hadi nane kwa mwaka 2015.

Alisema katika matukio hayo jumla ya askari saba waliuawa kwa mchanganuo kwenye mabano Chamazi (2), Mkuranga (2) na Ushirombo (3)Bunduki zilizoporwa ni bunduki 22 na mchanganuo wake ni Chamazi (2), Mkuranga (1), Ushirombo (17) na Tanga (2).

CHANZO: NIPASHE

MAGUFULI ATANGAZA NIA YA URAIS

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza rasmi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kwa kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kwa wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini, ameona hana budi kutangaza rasmi azma yake.

Dk. Magufuli, mmoja wa mawaziri ambao kwa muda mrefu wamehusishwa kwenye kinyang'anyiro cha nafasi hiyo, alisema anaingia kwenye mchuano huo akiwa na sifa zote stahiki za kupiga na kupigiwa kura.

Alitangaza azma yake nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, muda mfupi baada yakumalizika kipindi cha maswali na majibu bungeni, jana asubuhi.

Baada ya kuulizwa kama ana mpango huo, mara moja alisema: "Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia."

Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza.

"Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi 'nitagombea urais'.Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi," alisema Dk. Magufuli.

Alisema siku ya kuchukua fomu ataitangaza baadaye pindi akishakamilisha taratibu za namna ya kuanika hadharani mambo anayokusudia kuyatekeleza endapo wana CCM watampa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho.

Kuingia kwake kwenye harakati za kuwania nafasi ya urais kunazidi kuufanya mchuano wauchaguzi wa nafasi hiyo ndani ya CCM kwa mwaka huu kuwa mkali zaidi.

Dk. Magufuli, amekuwa mbunge tangu mwaka 1995. Baada ya kushinda ubunge mwaka huo, alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi; Wizara iliyokuwa ikiongozwa na Anna Abdallah.

Anajulikana kama kipenzi cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa, ambayemara kadhaa hakusita kumsifu hadharani, akimtaja kama mmoja wa 'askari wa miavuli' katika baraza lake la mawaziri.

Aidha, uhusiano wake na Mkapa umejidhihirisha hadi kwenye masuala ya kifamilia, ambako mara kadhaa rais huyomstaafu ameweza kuhudhuria hafla na misiba mbalimbali nyumbani kwa Dk. Magufuli.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk. Magufuli alipewa fursa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM kusoma mafanikio ya chama hicho kwenye utekelezaji wa ilani yake upande wa barabara.

Uwezo wake wa kukariri takwimu mbalimbali, ulikuwa kivutio kwenye mkutano huo na sehemu nyingine kama bungeni ambako hutakiwa kueleza mafanikio ya wizara yake.

Hivi karibuni, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Ali Hassan Mwinyi, alimsifu kwa kumtaja kama 'simba wa kazi' kutokana na uchapaji kazi wake katika wizara mbalimbali ambazo ameziongoza.

Kwa upande wa wananchi, wengi wanamuona Dk. Magufuli kama mmoja wa mawaziri wachapakazi waliowahi kutokea katika historia ya taifa hili.

Hata hivyo, waziri huyo amekuwa akikosolewa kwa uamuzi wake wa uuzaji nyumba za Serikali kwa watumishi na hata wasio watumishi wa umma.

Pamoja na dosari hiyo, watetezi wake wanaamini kilichofanywa wakati huo wa utawala wa awamu ya tatu kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Baraza la Mawaziri, na si uamuzi wa Dk. Magufuli mwenyewe.

Chanzo: Mtanzania

RAIS KENYATTA AKWAMA KWENDA NIGERIA

Rais Uhuru Kenyatta alisitisha ziara yake ya kwenda Nigeria siku ya Alhamisi masaa kumi na moja baada ya kuibuliwa maswali dhidi ya idadi kubwa ya maafisa ambao aliungana nao kwenye safari hiyo.

Badala yake, Kenyatta alimtuma makamu wa rais William Ruto kumuwakilisha katika kuapishwa kwa rais mpya wa Nigeria, Jenerali Muhammadu Buhari, leo.

Safari ya rais ilisitishwa siku moja baada ya maafisa 84 wa serikali ambao waliungana naye kuvujishwa kwenye vyombo vya habari. Maswali yaliulizwa kuhusu ukubwa wa ujumbe huo.

Hii ni mara ya pili kwa Kenyatta kusitishiwa safari zake, mwezi uliopita, ndege yake iligeuka angani katika hali ya kushangaza wakati akielekea Marekani baada ya kuhitajika kuitisha mkutano wa biashara nchini kwake.

Taarifa za kugeuka kwa ndege yake hazikuelezwa kwa kina japo inadaiwa kuwa ndege hiyoiligeuka ikiwa anga la Ethiopia.

IDADI YA WALIOKUFA KUTOKANA NA JOTO YAONGEZEKA INDIA

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ongezeko la joto nchini India imefikia 1,412 huku joto likifikia takriban nyuzi joto 47.

Watu 550 walikufa katika miji ya Andhra na Pradesh huku wengine zaidi ya 215 wakishindwa kukabiliana na joto hilo mjini Telangana.

Msimamizi shughuli za majanga nchini humo Saada Bhargavi amesema kuwa vifo katika jimbo la Telangana vimefika watu 215 tangu kuanza kwa joto hilo kali hapo Mei 15.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini India ilitangaza kuwa hali ya joto katika majimbo ya Telangana na Andhra Pradesh inategemewa kuwa nyuzi joto 29 na 41 kwa siku zijazo.

Mji mkuu wa India, New Delhi umefikisha nyuzi joto 45.5 mpaka sasa.

MGOMBEA URAIS CCM KUJULIKANA JULY 12

Chama cha Mapinduzi(CCM) kimetoaratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku ikionyesha mgombea urais atapatikana Julai 12, mwaka huu baada ya kupitishwa na mkutano mkuu.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar mgombea urais anatarajiwa kupatikana Julai 10, mwaka huu baada ya kupitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, alisema mchakato wa uchukuaji na urudishaji fomu katika nafasi ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajia kuanza Juni 3 hadi Julai 2,mwaka huu saa 10 jioni.

Alisema ndani ya tarehe hizo mgombea atatakiwa kutafuta wadhamini 450 kwenye mikoa 15, mitatu ya Zanzibar na mmoja wapo uwe kati ya Unguja na Pemba, huku Tanzania Bara ikiwa mikoa 12.

Akifafanua zaidi, alisema ongezeko la wadhamini kwa mgombea wa urais kutoka 250 miaka ya nyuma hadi 450 linatokana na ongezeko la mikoa pamoja na wanachama wa CCM.

Aidha, Nape alisema vikao vya mchujo vinatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 8, mwaka huu, ambapo itakaa Kamati ya Usalama na Maadili ikifuatiwa na Kamati Kuu Julai 9 wakati NEC ikitarajiwa kuwa Julai 10, huku Mkutano Mkuu utafanyika Julai 11 hadi 12 mwaka huu.


MASHARTI YA UGOMBEA URAIS
Kuhusu masharti kwa wagombea wa Urais upande wa Tanzania, alisema yameongezeka ikiwa ni pamoja kutafuta wadhamini 450 kwa mwaka huu badala ya 250 kama ilivyokuwa kwa chaguzi zilizopita za mwaka 2005 na 2010.

Alisema mgombea wa urais hatatakiwa kudhaminiwa na mjumbe yeyote wa mkutano mkuu kwa sababu wanashiriki katika mchakato wa kuteua mgombea.

Aliongeza kuwa mwanachama mmoja hataruhusiwa kudhamini zaidi ya mgombea mmoja, pia fomuhiyo itathibitishwa na katibu wa wilaya kama waliodhamini fomu hiyo ni wanachama.

"Hayo ni masharti matatu ya kwanza ya msingi wanatakiwa kuyajua…wajumbe wa mkutano mkuu ni marufuku kumdhamini mgombea, adhaminiwe na wanachama wa kawaida au viongozi ambao hawaingii katika huo mchakato," alisema.

Kwa upande wa Zanzibar, Nape alisema fomu za urais zinatarajiwa kuanza kuchukuliwa Juni 3 na kurudishwa Julai 2, mwaka huu saa 10 jioni.

Alisema ndani siku hizo, mgombea atatakiwa kutafuta wadhamini 250 kwenye mikoa mitatu ya Zanzibar na mmoja uwe Unguja au Pemba.

Alisema vikao vya mchujo wa wagombea vinatarajiwa kuanza Julai 4, mwaka huu kwa Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar ikifuatiwa na Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Zanzibar itakayokaa Julai 5, mwaka huu, Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa itafanyika Julai 8, mwaka huu, wakati Kamati Kuu ikikaa Julai 9, mwaka huu na NEC ikikaa Julai 10, mwaka huu.

Alisema CCM inategemea kupata mgombea wa urais wa Zanzibar Julai 10, mwaka huu kwa utaratibu ambao mgombea huyo anapatikana kwa kupitia NEC na si Mkutano Mkuu kama ilivyo kwa mgombea waUrais wa Jamhuri wa Muungono wa Tanzania.


MASHARTI YA UGOMBEA URAIS ZNZ
Nape alitaja masharti ya mgombea wa urais wa Zanzibar kuwa anatakiwa kuwa na wadhamini 250 sharti ambalo lilikuwapo na halijabadilika.

Alisema wajumbe wote wa NEC ambao ndiyo watakaofanya uamuzi hawaruhusiwi kumdhamini mgombea wa urais.

UBUNGE
Kuhusu wagombea ubunge alisema wanatarajiwa kuchukua fomu Julai 15, mwaka huu na kurudisha Julai 19, mwaka huu.

Nape alisema wagombea wa ubunge watafanya mikutano ya kampeni ya kujinadi kwa wanachama kuanzia Julai 20 hadi 31, mwaka huu.

"Ratiba itapangwa kwenye matawi namna ya kuyajumuisha matawi kama ilivyofanyika mwaka 2010, wagombea wataenda kwa wanachama watakuta mkutano umeandaliwa kwa ajili ya kuomba kura," alisema.

Aidha, alisema Agosti Mosi itakuwa ni siku ya kupiga kura ya maoni kwanchi nzima kwa ajili ya kuwapata wagombea ubunge wa CCM, baada ya hapo kutakuwa na vikao vya mchujo kwa ajili ya kuwapata wagombea watakaopambana na wagombea wa vyama vingine.

Hata hivyo, alisema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, uchukuaji fomu na urejeshwaji itakuwa kama michakato ya kwenye ubunge.


VITI MAALUM na WAWAKILISHI

VITI MAALUM
Alisema uchukuaji na urudishaji wa fomu utakuwa kama kwenye ubunge isipokuwa mchakato wa kuwachuja utapitia kwenye vikao vya Jumuiya ya Wanawake (UWT).

UDIWANI
Alisema kwa upande wa udiwani ratiba itakuwa kama ya ubunge.

"Tofauti ni kwamba Tanzania Bara kutakuwa na masanduku mawili yaani ya ubunge na udiwani na Zanzibar kutakuwa na masunduku matatu yaani ubunge, wawakilishi na udiwani," alisema.

Kuhusu Viti Maalum kupitia vijana, Nape alisema utaratibu wa mwisho wa kutoa majina utafanywa na UWT Taifa badala ya Baraza la Umoja wa Vijana.

Pia, alisema Jumuiya ya Wazazi imepewa viti viwili vya ubunge na mchakato wake utapitia Baraza la UWT.

Aidha, alisema daftari la wanachama wa CCM litafungwa Julai 15, mwaka huu na pia zipo hatua zitazochukuliwa kudhibiti wanachama feki.

Alisema viwango vya uchukuaji fomu vipo kwenye kanuni kama ilivyo katika vipindi vya uchaguzi vilivyopita. Hata hivyo, aliwataka wagombea kuzingatia kanuni na taratibu za chama hicho ikiwa ni pamoja na kuzisoma na kuzielewa kanuni hizo ili wasifanye kinyume na taratibu.

"Tusingependa kuona wale wanaokuja kuchukua fomu na kurudisha wanakuja kwa mbwembwe na hatutaki sherehe wala madoido, safari hii kosa moja goli moja," alisema.

Kuhusu upigaji kura, alisema mwanachama anatakiwa awe na kadi mbili, yaani kadi ya uanachamana kadi kupiga kura kwa ajili ya utambulisho wake.

Baadhi ya wajumbe wa Nec, wamesema hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, juzi imewafanya wanachama wa chama hicho kuwa wamoja na kutambua dhamira ya mwenyekiti wao ndani ya chama na Taifa kwa ujumla.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Makao Makuu ya chama hicho maarufu 'White House', walisema hotuba hiyo imedhihirisha kuwa Rais Kikwete hana mgombea na hatakuwa tayari kukiacha chama kikienda ovyo wakati yupo.

Pia wameeleza kuwa hotuba yake imeleta matumaini mapya ya kuwaunganisha wanachama kuwa wamoja.

BALOZI KARUME
Mmoja wa wajumbe wa NEC kutoka Zanzibar, Balozi Ali Karume, alisema hotuba hiyo ni kama darasa kwa wanachama wa chama hicho."Nimefurahishwa na hotuba ya Rais Kikwete kwani ameonyesha ukomavu wake kwenye medani ya siasa ndani ya chama," alisema.

Balozi Karume alisema hotuba ya Rais Kikwete itatumika kuivusha CCM katika uchaguzi mkuu na chaguzi nyingine zinazotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

"Naamini hata nukuu zake zitakuwa dira ya kukiongoza chama chetu wakati kutakapokuwa na viongozi wengine," alisema.

Alisema Rais Kikwete amezungumza mambo ya msingi na wazi, amedhihirisha anatanguliza maslahiya chama chake na si marafiki zake kwani ameweka wazi kwenye suala la kuchagua kiongozi kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama hakuna sababu ya kutanguliza urafiki.

"Mwenyekiti wetu wakati anazungumza alinukuu baadhi ya meneno yaliyokuwa yakizungumzwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, lakini naamini hotuba ya Rais aliyoitoa leo(juzi) itakumbukwa na kizazi cha sasa na kijacho".

"Hotuba hii ya Rais itatumika kama nukuu kwa ajili ya chaguzi na namnaya kukiendesha chama.
Nimekaa nje ya nchi kwa muda mrefu, lakini alichozungumza Rais amedhihirisha kiwango chake kwenye siasa ni cha hali ya juu na amekomaa katika demokrasia. Amekuwa kwenye chama muda mrefu kwa hotuba yake hii anakwenda kupumzika akiwa ameacha historia iliyotukuka," alisema Balozi Karume.

Alisema moja ya mambo yanayoharibu chama ni pamoja na kuingiza urafiki kwenye masuala ya uongozi.

"Na hilo Rais Kikwete amezungumza kwa ufasaha na ameonyesha kutokuwa tayari kuchagua kiongozi kisa urafiki au kujuana kwa maslahi binafsi," aliongeza.

Balozi Karume alisema Rais Kikweteamezungumza na wajumbe wa NEC lakini hakuonyesha anataka nani achaguliwe kwani hakuwa upande wowote zaidi ya kuzungumzia hali halisi ya chama hicho na wakati uliopo.

"Ingekuwa wengine hapa tungeanza kupata maelekezo ya Rais kuhusu nani anataka awe Rais baada ya kumaliza muda wake, lakini yeye hana chaguo lake, hivyo ametaka sifa, kanuni na maadili ya chama iwe dira ya kupata viongozi wake."

ABDALLAH BULEMBO
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, alisema mgombea wa CCM lazima awe msafi na asiyekuwa na kashfa chafu.

Alisema mgombea wa CCM anayetaka kugombea uongozi si yule mwenye mbwembwe na madoido mengi, bali ni mtu mwenye kujitambua na kujiamini.

KHAMISI MGEJA
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, alisema hotuba ya Rais Kikwete ni darasa tosha kwa wanachama wa CCM hasa kipindi hiki kwa kuwa suala la kuchagua viongozi ni la muhimu.

Aliwataka wajumbe wa Nec na wanaCCM kwa ujumla kuisikiliza kwa umakini hotuba hiyo ili kufahamu misingi ya chama hicho.

"Lazima wanachama wasome alama za nyakati kwa kuchagua viongozi si utashi wa viongozi, bali kwa utashi wa wananchi ambao ndiyo wanaopiga kura"."Nimesikiliza vizuri hotuba ya Mwenyekiti wetu, amezungumza mambo ya msingi ambayo kwetu sisi ni darasa tosha. Lazima tusome alama za nyakati.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka jana tumeshuhudia baadhi ya mitaa imekwenda upinzani kwa sababu ya viongozi kuwa na watu wao na si wale wanaotakiwa na wananchi," alisema na kuongeza:"Hivyo lazima tuchague viongozi kwa kuangalia wananchi wanamtaka nani na si kiongozi anataka nani awekiongozi."Mjumbe wa Nec kutoka Wilaya ya Musoma, Vedastus Mathayo, alisema hotuba hiyo imetoa mwelekeo kwa chama hicho na njia madhubuti kuelekea katika uchaguzi mkuu.


MWIGULU AJIUZULU
Wakati huohuo, Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba, amejiuzulu wadhifa huo.

Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha anatajwa kuwa miongoni mwa makada wa CCM wenye nia ya kuwania kupitishwa nachama hicho kuwania urais uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

CHANZO: NIPASHE

WATU WATATU WAFARIKI BASI LATUMBUKIA MTONI

Watu watatu wamekufa papo hapo na wengine 28 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Super Feo walilokuwa wakisafiria kutoka jijini Mbeya kwenda Songea kupinduka na kutumbukia mtoni katika kijiji cha Shamwanga Kata ya Inyara, Mbeya.

Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa12:50 asubuhi muda mfupi tu baadaya basi hilo kuanza safari.

Mashuhuda walisema basi hilo likiwa kwenye mwendo mkali lilitaka kulipita lori lililokuwa mbelena wakati likiwa limeingia upande wa kulia wa barabara, lilitokea lori lingine la kusafirisha mafuta kwa mbele na hivyo magari hayo yakataka kugongana uso kwa uso.

Gasper Alfred, mkazi wa kijiji cha Shamwengo, alisema baada ya basi hilo kumshinda dereva na kutumbukia mtoni, abiria waliokuwamo walitoka wakiwa wameumia, huku watatu baadhi yao wakionekana kupoteza maisha.

"Nililiona basi hili likijaribu kulipita lori la mbele, lakini kwa upande wa pili likatokea lori lenye tenki la mafuta ndipo dereva wa basi akaamua kulikwepa ili wasigongane uso kwa uso, lakini dereva alipotakakurudi barabarani gari lilimshinda na kutumbukia mtoni, nimeona watu wengi wametolewa wakiwa wameumia na watatu wakiwa wamekufa," alisema Alfred.

Alisema kuwa miongoni mwa watu alioshuhudia wakitolewa kwenye gari wakiwa wamekufa, mmoja wao ni mzungu wa jinsia ya kiume na wengine wawili ni Watanzania, mmoja akiwa mwanaume na mwingine mwanamke.

Daktari wa zamu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Lathan Mwakyusa,alithibitisha kupokea miili ya marehemu watatu pamoja na majeruhi 28 hospitalini hapo.

Dk. Mwakyusa alisema miongoni mwa majeruhi hao 28, kati yao 24 walitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku wengine wanne wakilazimika kulazwa hospitalini hapo kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo pamoja na maeneo wanayoishi kwenye mabano kuwa ni Patric Mwakasege (Uyole), Erasto Nyoni (Iyunga), Ester Nyange (Kilosa), Agness Mwambosyo (Kiwira), OmaryAlly (Jacalanda), Fatma Nyambi (Loleza), Tabia Sward (Kyela), Maua Ngonyani (Songwe), Catheline Mbula (Dar es Salaam), Edson Omary (Chunya), Asukenye Mwandanege (Tukuyu), Veronica Emmanuel (Kilosa), Emmanuel Mwandanege (Tukuyu).

Wengine ni Charles Lwambano (Mbeya), Baraka Abiah (Airport) Patrick Mlimbilwa (Songea), Mwangaza Shaibu (Airport), Felicia Mwalongo (Songea), Francis Abel (Songea), Adam Raphael (Mbinga), Anuary Hemed (Njombe), Canoe Ho(Rudewa), Petili Mbema (Songea), Fatma Abdallah (Airport), Ginny Warley (Njombe), Cecilia Rengina (Njombe) na Ashraf Abiah (Airport).

KIONGOZI WA UPINZANI BURUNDI AUWAWA

Kiongozi wa chama kidogo cha upinzani nchini Burundi ameuawa kwa kupigwa risasi.

Mwili wa Zedi Feruzi pamoja na wa mlinzi wake ulipatikana nje yanyumba yake kwenye mji mkuu Bujumbura.

Mauaji ya mwanasiasa huyo yanafanyika wakati wanaharakati wa upinzani nchini humo wamesitisha kwa siku mbili maandamano yao dhidi ya rais Pierre Nkurunziza kupinga uamuzi wake wa kuwania urais muhula wa tatu.

Uamuzi huo ambao wengine wanasema kuwa unaenda kinyume na sheria umesababisha kuwepo kwa jaribio la kumpindua, maandamano ya wiki kadha na kuhama kwa zaidi ya watu 100,000 kutoka nchini humo.

WANANDOA WACHINJWA KAMA KUKU

Watu wawili, mke na mume wakazi wa Makambo, wilayani Mlele, wameuawa kikatili kwa kuchinjwa nakutenganishwa kichwa na kiwiliwili wakati wakiwa wamelala.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, aliwataja wanandoa hao kuwa ni Seth Mwakalimbwa (65) na Yakoba Kalulu (48).

Kidavashari aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Mei 21, usiku nyumbani kwa wanandoa hao ambao baada ya kuuawa miili yao iliachwa kitandani.

Alisema marehemu hao wakati wa uhai wao walikuwa wakiishi kwenye nyumba yao peke yao kwa muda mrefu.

Alisema, balozi wa eneo hilo, Wilbroad Mahenge, ndiye aliyegundua vifo hivyo baada ya kutowaona wanandoa hao kwa siku mbili mfululizo na kuingiwa na wasiwasi.

Kamanda Kidavashari alisema balozihuyo aliamua kwenda kwenye nyumba ya wanandoa hao ili kujua hali zao na alipofika alikuta milango ikiwa wazi hali iliyosababisha apate mashaka.

Alisema alijaribu kuwaita kwa majina yao lakini hakuna aliyeitika na aliamua kuingia ndani na kuwakuta wakiwa wamelazwa kitandani huku wakiwa wamefariki dunia kwa kuchinjwa shingo zao na kutenganishwa kiwiliwili na kichwa.

Alisema, balozi Wilbroad alikwenda kutoa taarifa kwenye uongozi wa serikali ya kitongoji ambao nao walitoa taarifa polisi.

Kamanda alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina.

Aidha, alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Alisema polisi kwa kushirikiana na uongozi na wanakijiji wa Makambo, wanaendelea na msako ili kuwabaini watu waliohusika katika mauaji hayo.

WATU WENYE ULEMAVU WAFUNGA BARABARA KUPINGA KUVUNJIWA MEZA ZAO

Walemavu wanaofanya biashara katika soko la Karume Mchikichini wamelazimika kulala katika makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya masaa sita wakilalamikia kuvunjiwa meza zao za biashara na halmashauri ya manispaa za Ilala, hali iliyosabaisha baadhi ya barabara kushindwa kupitika kutokana na kuwepo kwa msongamano mkubwa wa magari.

ITV imeshuhudia walemavu hao wakiwa wamekaa katikati ya makutano ya barabara ya Kawawa na Uhuru bila woga, huku wakifukuza watu ovyo kwamba hawahusiki katika kuwasidia, ambapo katika mahojino na baadhi yao wamesema wamesikitishwa na kitendo cha serikali ya wilaya ya Ilala kuwavujia meza zao na kusababisha upotevu wa baadhi ya mali zao na kuongeza kuwa iwapo serikali haitaingilia kati sakata lao watalala hapo barabarani.

Licha ya barabara mbalimbali kushindwa kupitika kutokana na sakata hilo ambalo limevuta hisia za watu wengi, baadhi ya madereva wamelalamikia kusimama katika msongamano kwa masaa mengi
Huku wakidai kuwa kuendelea kwa sakata hilo inasababisha shughuli mbalimbali muhimu ikiwemo shughuli za maendeleo kusimama.

Kutokana na hasira za kuvunjiwa meza zao majira ya usiku bila taarifa, baadhi ya viongozi waliofika katika eneo hilo ili kuzungumza nao walijikuta katika wakati mgumu huku askari wa polisi wakitumia hekima ya kutowatawanya watu hao kwani kwa kufanya hivyo wengi wao wangeumia.

Majira ya saa kumi jioni huku msongamano wa magari ikiendelea kutesa watu, baadhi ya watu walionekana kutembelea kwa mguu katika baadhi ya barabara kwa kukosa usafiri huku mkuu wa wilaya ya Ilala Reymond Mushi akikubali kuwepo kwa maelezo ya maaandishi kuwa wafanyabiashara hao watarudi katika maeneo yao huku uchunguzi ukianza mara moja ili kubaini madhara ya vunjavunja hiyo pamoja na suala la fidia.

CHANZO:ITV

RAIS WA BURUNDI AONEKANA HADHARANI, AL SHABAAB WAKANUSHA TAARIFA

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza Jumapili mwishoni mwa juma hili lililopita tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi Jumatano Mei 13 mwaka 2015.

Kuonekana hadharani kwa Pierre Nkurunziza kumesitisha uvumi kwamba rais huyo hajarejea nchini Burundi.

Pierre Nkurunziza amewapokea wanahabari nyumbani kwake na kusema kwamba Burundi inakabiliwa na vitisho vya wanamgambo wa kiislamu wa Kisomalia wa Al Shabab.

"Tuko hapa kuwaambia kwamba tunapaswa kuwa makini na tishio la Al Shabab na tutachukua hatua muhimu za kukabiliana na mashambulizi ya wanamgambo wa kundi la Al Shebab", amesema rais Pierre Nkurunziza.

Kundi la Al Shabab kupitia msemaji wake amekanusha madai hayo ya rais Nkurunziza ya kushambulia nchiyake. Al Shabab imesema huo ni mpango wa Pierre Nkurunziza na serikali yake wa kutaka kuwakandamiza waandamanaji ili wasiendelei kuandamana dhidi ya muhula wake wa tatu.

Awali rais Pierre Nkurunziza hakupendelea kuzungumza na wanahabari, lakini imeonekana kuwa alishinikizwa na washirika wake wa karibu ili aweze kuondoa uvumi uliyokua ukizagaa tangu Ijumaa juma lililopita kwamba rais huyo hayupo nchini Burundi, na huenda picha na sauti yake viliyorushwa hewani kwenye redio na runinga vya taifa vilirikodiwa nje ya nchi alipokua, baada jaribio la mapinduzi.

Hata hivyo rais huyo hakueleza kuhusu jaribio la mapinduzi na kupingwa kwa muhula wake wa watatu. Wakati huo huo mshauri wake mkuu anayeshusika na masuala ya mawasiliano Willy Nyamitwe, ameeleza kwamba kuna uwezekano wa kuahirisha kwa wiki kadhaa uchaguzi wa madiwani na wawabunge uliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Mei.

Hayo yakijiri, vyama vya kiraia pamoja na vyama vya kisiasa vya upinzani ikiwa ni pamoja na baadhi ya wafuasi wa chama tawala cha Cndd-Fdd wamesema wataendelea na maandamano Jumatatu wiki hii, wakibaini kwamba jaribio la mapinduzi lilioendeshwa Jumatano wiki iliyopita lilikua ni mpango wa serikali wa kutaka kuzima maandamano, vyama vya kiraia pamoja na kusitisha matangazo ya vituo vya redio na televisheni vya kibinafsi.

Itafahamika kwamba vituo vine vya redio za kibinafsi ikiwa ni pamoja na redio Isanganiro, Bonesha Fm, RPA na redio na televisheni Rennaissance Fm, vilishambuliwa kwa roketi. Polisi inanyooshewa kidole kuhusika na mashambulizi hayo.

FOMU ZA URAIS BEI JUU

Wagombea wa nafasi ya urais, ubunge na udiwani watalazimika 'kutoboka mifuko' zaidi kutokana na gharama za fomu kwa vyama husika kuwa juu.

Wiki iliyopita, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walitangaza kuwa fomu kwa wagombea urais zitatolewa kwaSh1 milioni, ubunge Sh250,000 na udiwani Sh50,000.

Kwa upande wa Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema mgombea wa urais, atalazimika kulipa Sh1 milioni kwa nafasi hiyo.

Naibu Katibu Mkuu-Bara, John Nyambabe alisema jana kwamba fedha zitakazopatikana kwa gharama za fomu zitatumika kusaidia shughuli za chama.

"Tayari tumeshatoa fomu kwa mtu mmoja kwa upande wa urais ambaye ni Dk George Kahangwa, lakini bado fomu zipo na chama kinakaribisha wengine," alisema Nyambabe.

Alisema gharama za fomu za ubunge ni Sh50,000 na udiwani Sh20,000.

Chama cha Wananchi (CUF), kimesema mgombea urais atalazimika kulipia fomu Sh500,000.

Ofisa Uchaguzi wa CUF, Lugoni Abdulrahaman alisema tayari wabunge wamesharejesha fomu na kura za maoni zinaanza Mei 20, mwaka huu.

Alisema wagombea hao walichukua fomu kwa Sh50,000, huku za udiwani zikiwa ni Sh20,000.

"Wagombea wa ubunge na udiwani tayari wamesharejesha fomu mchakato wa kura za maoni unaanza na kwa kuanza tunaanzia Zanzibar," alisema Lugoni.

Vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ambavyo vimekubaliana kumteua mgombea mmoja wa urais.

Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 22 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 23 na 24 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za uchaguzi ikiwamo kutoa fomu.

BINTI APAMBANA NA MAMBA NUSU SAA KUMUOKOA MAMA YAKE

MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka tisa ameonesha ujasiri wa kipekee kwa kumwokoa mama yakemzazi, Magreth Ibrahim (50) kuuawa na mamba baada ya kupambana na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.

Mama huyo mkazi wa kijiji cha Karema, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda, kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini Mpanda kwa matibabu baada ya mkono wake kunyofolewa na mamba aliyemshambulia wakati akifua kando ya Mto Ikola.

Akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyemtembelea hospitalini hapo masaibu yaliyomsibu, alisema anamshukuru sana binti yake mwenye umri wa miaka tisa aliyeweza kuokoa maisha yake licha ya kuwa amenyofolewa mkono na mamba huyo.

Akisimulia mkasa huo, Magreth alieleza kuwa juzi akiwa anafua kando ya mto Ikola ghafla mnyama huyo aliibuka majini na kumpiga usoni na mkia wake.

"Mamba huyo aliibuka ghafla mtoni na kunichapa usoni na mkia wake nami nikaangukia majini ndipo aliponidaka mkono wangu na kunivutia mtoni ….binti yangu aliyekuwa jirani yangu alipoona nikokaribu kuliwa na mamba kwa ujasiri aliweza kukabiliana naye … Alinishika mkono mwingine na kunivutia nje huku akipiga kelele kumtisha mnyama huyo ili aniachie hatimaye akaunyofoa mkono wanguna kutokomea nao mtoni …." alieleza.

Aliongeza kuwa watu waliokuwa wakifua mtoni hapo wengi wao wakiwa wanawake walifika eneo la tukio ambapo wakiwa na binti yangu walimvuta na kumtoa nje na baadae wakamkimbiza hospitalini mjini Mpanda kwa matibabu.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa amethibitisha kuwa hali yamama huyo inaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.

ALIYEKUWA RAISI WA MISRI AHUKUMIWA KUNYONGWA

Mahakama moja nchini Misri imetoa amri ya kunyongwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Mohammed Morsi.

Mahakama hiyo ilimpata na hatia aliyekuwa rais wa Misri Mohammed Morsi kufuatia kuvunjwa kwa magereza mwaka wa 2011.

Kauli hii ni msumari katika kidonda cha Morsi ambaye alikuwa tayari anatumikia kifungocha miaka 20 jela kwa kuamrisha kukamatwa kwa waandamanaji waliopinga utawala wake.

Morsi aling'olewa mamlakani na jeshi mwezi Julai mwaka wa 2013 kufuatia kipindi kirefu cha maandamano dhidi ya utawala wake.

Kuanzia hapo chama chake cha the Muslim Brotherhood kimepigwa marufuku huku mamia ya maelfu ya wafuasi wake kukamatwa na vyombo vya dola.

Kufuatia uamuzi huo wa kifo , sasa kauli nzima na ruhusa itapatikana tu baada ya uamuzi kutumwa kwa kadhi mkuu nchini humo ambaye sasa ndiye atakayetoa uamuzi wa mwisho iwapo Morsi ataonja mauti au la.

Sheria za nchi hiyo hata hivyo zinamruhusu Morsi kukata rufaa licha ya uamuzi wa kadhi mkuu.

Morsi na wafuasi wake wamekuwa wakishikilia kukutu kuwa mashtaka dhidi yake yamechochewa na uhasma wa kisiasa baina yake na uongozi ulioko sasa.

Morsi amekataa katakata uhalali wa mahakama iliopo sasa.

Morsi aliweka rekodi ya kuwa kiongozi wa kwanza kuchaguliwa katika uchaguzi wa haki na huru.

Hata hivyo utawala wake ulikumbwa na wimbi la maandamano baada ya kujilimbikizia madaraka akiwa amehudumu kwa mwaka mmoja tu ya kuwa ofisini.

WATU WAWILI WAUAWA KWA BOMU KABUL

Watu wawili wameripotiwa kufa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya mlipuko kutokea kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege katika mji mkuu wa Afganistan Kabul.

Walioshuhudia wanasema kuwa mlipuaji wa kujitolea mhanga alikuwa amelenga wanajeshi wa kimataifa nje ya lango kuu la uwanja huo wa ndege.

Haijabainika iwapo walikwepa shambulizi hilo au la.

Lango hilo hutumika na maafisa wa kijeshi wa kigeni pekee yao.

Msemaji wa polisi nchini humo amaiambia BBC kuwa shambulizi hilo lilifanyika karibu na afisi za halmashauri za safari za ndege nchini humo zilizoko nje ya uwanja wa ndege.

Mtu aliyeshuhudia alilitaja shambulizi hilo kuwa la kujitoa mhanga.

Shambulizi hilo linafanyika siku tatu baada ya mwanamgambo mmoja kuwaua watu 14 wakiwemo raia 9 wa kigeni mjini humo.

MTOTO ANAHITAJI MSAADA WA UPASUAJI NJIA YA HAJA KUBWA

FATIMA Msuya mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita wa wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma anahitaji kusaidiwa Sh milioni 2.5 ili afanyiwe upasuaji utakaowezesha kupata njia ya haja kubwa.

Mama wa mtoto huyo, Paulina Titus (48) alisema Fatima alizaliwa bila sehemu ya haja kubwa kabla ya kufanyiwa upasuaji kwa mara yakwanza katika Hospital ya Peramiho ambapo aliwekewa njia ya haja kubwa tumboni.

Paulina alisema hata baada ya kufanyiwa upasuaji huo, mtoto huyo hajaweza kujisaidia katika njia hiyo mpaka atakaporudi tena KCMC kwa upasuaji mwingine.

Aidha mama huyo alisema, kwa yeyote aliyeguswa na ambaye yupo tayari kumsaidia, atume msaada wake wa fedha kwa namba 0767 710113.

RAIA WAPYA WA KIRUNDI WAKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI

POLISI mkoani Katavi imewakamata raia wapya watatu waliokuwa wakimbizi kutoka Burundi kwa kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo.

Watu hao walikamatwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 1.2.

Nyara hizo za Serikali ni vipande vitatu vya meno ya tembo vikiwa sawa na jino moja la mnyama huyo vikiwa tayari kusafirishwa kwenda mjini Tabora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari amewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Frank Hamis (18) , Steven Jonas (22) na Jackson Erasto ambao karibuni wamepewa uraia wa Tanzania.

Kidavashari alibainisha kuwa watuhumiwa hao walikutwa juzi saa 3:00 asubuhi katika chumba alichopanga mwanafunzi wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari Katumba, Ernest John (19) katika eneo la Mnyasi kijijini Katumba wilayani Mlele."

Mwanafunzi huyo ana uhusiano nao wa kindugu hivyo aliwakaribisha kulala chumbani kwake alimokuwa amepanga katika nyumba ambayo ni mali ya Felix Gado iliyopo eneo la Mnyasi kijijini Katumba.

MGAHAWA WAUZA NYAMA YA BINADAMU NIGERIA

Mgahawa mmoja nchini Nigeria katika jimbo la Anambra umefungwa kufuatia viongozi wenye mamlaka nchini humo kung'amua kwamba moja ya vyakula vinavyouzwa mgahawani humo ni nyama ya binadamu.

Polisi walipoitwa mgahawani hapo waliona vichwa viwili vya binadamu vipya vyenye kuchuruza damu wakati walipokuwa wakiwakamata watu kumi na mmoja kutoka mgahawani hapo akiwemo mmiliki wa mgahawa huo,pia walikamatwa wanawake sita na wanaume wane, baada ya wasamaria wema kutoa taarifa hizo za kustaajabisha!
Damu zilizokuwa zikivuja kwenye vichwa hivyo vya wanaadamu,vilikuwa vimefungwa kwenye mifuko ya Rambo.

Polisi pia wamekamata bunduki aina ya AK-47 na silaha nyinginezo,seti ya magurunedi nasimu kadhaa za kila aina wakati walipokuwa wakiwakamata watu hao.

Kila wakati nilipokuwa nikienda sokoni,na sababu kubwa hasa hoteli hiyo iko karibu na sokoni,nimekuwa nikishuhudia harakati za ajabu za watu kuingia na kutoka hotelini humo,watu wachafu na uchafu wao mwilini niule usioeleweka,hivyo siku shangazwa polisi walipogundua biashara hiyo haramu mapema wiki hii, anasema mkaazi wa eneo hilo.

Mchungaji mmoja akiwa katika mshtuko mkubwa baada ya kugundua kuwa alikuwa amekula nyama ya binaadamu,aliamua kwenda polisi kupeleka malalamiko yake.

Aliwaambia kuwa alikwenda kwenye mgahawa wa hoteli hiyo asubuhi na mapema,baada ya kupata staftahi,akaambiwa kwamba pande la nyama alilokula gharama yake ni naira 700 sawa na paundi mbili unusu alistaajabu mno.

Sikufahamu kuwa nimeuziwa nyama ya binadamu nikaila na kwamba ilikuwa ghali sana.

Taarifa za watu nchini Nigeria kula nyama za watu zimekuwa ni uvumi wa muda mreefu, lakini hii ni mara ya kwanza mgahawa kuamua kuuza nyama za binaadamu tu.

MVUA YAUA WATANO DAR

Mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo tangu juzi imesababisha vifo vya watu watano huku mamia wakikosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.

Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.

Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30."Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita." Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.

Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa "hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu".

"Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari," alisema Dk Kijazi.


Watano wafa

Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.

"Mtoto mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo Machimbo ya Makangarawe na mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua kunyesha na kujaa ndani ya nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado hajapatikana alisombwa na mafuriko pia," alisema Sadick.

Hata hivyo, habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73) mkazi wa Manzese.


Maeneo mengine

Katika eneo la Mbezi Luis, Mto Mbezi ulifurika, hali iliyosababisha nyumba zilizojengwa kandokando ya daraja hilo kufunikwa na maji.

Mkazi wa eneo hilo, John David alisema hali ilikuwa mbaya zaidijana asubuhi kwani maji yalifurika na kujaa barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji.

Alisema wakazi walio karibu na mto huo walichukua tahadhari tangu juzi na kuhama makazi yao.

"Haikuwa rahisi kwa wao kuendelea kukaa hapa wakati wanafahamu hali kama hii ingetokea. Tangu jana jioni familia zinazoishi huko ziliondoka, lakini vitu vyao vimesombwa na maji na nyumba moja imesombwa pia,"alisema David.

Maeneo ya Boko Basihaya, zaidiya nyumba 20 zilikuwa zimezingirwa na maji huku familia kadhaa zikilazimika kukimbia nyumba zao na kutafuta makazi ya muda kuanzia juzi usiku hadi jana.

Timu ya waandishi wa Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kushuhudia maji yakiwa yamejaa kwenye nyumba zilizojengwa kandokando ya bwawa linalotiririsha maji kuelekea baharini.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Dionise Swai alisema baada ya maji kujaa nyumbani kwake, alilazimika kuyanyonya kwa kutumia pampu ili kunusuru mali zake.

"Niliyawahi kwa hiyo hayakuingia. Wanafamilia wengine wameondoka nimebaki mwenyewe," alisema.

Mkazi wa mwingine eneo hilo, Frank Shuma alizitupia lawama mamlaka kwa kushindwa kujenga mifereji ya kutiririsha maji kwenda baharini.

Hali kama hiyo pia ilitokea eneo la Kinondoni Hananasif ambako maji yalijaa na kufunika baadhi ya nyumba.

Katika daraja la Kawe, wananchi walikuwa kwenye harakati za kuokoa mali zao zilizosombwa na maji, yakiwamo magodoro, vyombo na nguo.

Maji yalijaa kwenye barabara na kusababisha vyombo vya moto na watembea kwa miguu kupitakwa shida huku magari mengine yakilazimika kusimama pembeni.

Barabara ya Haile Selassie, upande wa baharini karibu na Hoteli ya Sea Cliff, eneo hilo lilifunikwa na maji na kusababisha usumbufu kwa vyombo vya moto na madereva kulazimika kuendesha kwa mwendo wa taratibu na kusababisha foleni.

Watumiaji wa barabara ya Mwai Kibaki walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi walionekana wakiwa wamevua viatu au kutafuta njia mbadala kukwepa maji yaliyokuwa yamejaa barabarani.

Mkazi wa Ubungo Kibangu, Julieth Kibakaya alisema hofu imetanda kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na athari zinazosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha hasa mafuriko.

"Huku kwetu hali ni mbaya. Mafuriko yamebomoa nyumba mbili hadi sasa. Hivi sasa wanafamilia hao hawana makazi tena imebidi wapewe hifadhi ya muda na majirani zao na hali ikiendelea hivi tunahofia wakazi wengi wa eneo hili watapoteza nyumba zao," alisema Kibakaya.

Chanzo: MWANANCHI

MARTIN NOOIJ ATAJA KIKOSI KUJIANDAA NA MICHUANO YA COSAFA

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mart Nooij leo ametangaza kikosi cha wachezaji 28.

Kikosi hicho kitaingia kambini katika hoteli ya Tansoma iliyo eneo la Gerezani jijini Dar es salaam, kujiandaa na michuano ya kombe la COSAFA na kuwania kufuzu kwa AFCON na CHAN mwezi Juni mwaka huu.

Katika orodha hiyo ya wachezaji 28 watakao ripoti kambini jumatatu mchana, watapimwa afya zao na madakatari wa timu ya Taifa, na kisha watakaokuwa fit atachagua wachezaji 20 watakao kwenda kwenye michuano ya COSAFA nchini Afrika kusini.

Wachezaji walioitwa ni magolikipa: Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula, Mwadini Ali (Azam),

Walinzi: Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Nadir Haroub, Oscar Joshua, Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda, Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Haji Mwinyi (KMKM).

Wengine ni viungo: Amri Kiemba,Salum Abubakar, Frank Domayo (Azam), Said Juma, Salum Telela, Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United) na Mwinyi Kazimoto (Al Markhira).

Washambuliaji ni Ibrahim Ajib (Simba), Mrisho Ngasa, Saimon Msuva (Yanga), John Bocco, Kelvin Friday (Azam) na Juma Luizio (Zeco United).

Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini siku ya jumatano, Mei 13 saa 1 jioni kwa shirika la ndege la Fastjet kuelekea nchini Afrika Kusini katika mji wa Rusterburg - North West Province ambapo ndipo michuano ya COSAFA CUP itafanyika kuanzia Mei 17 mpaka Mei 31 mwaka huu.

WAHAMIAJI WATIKISA SOKA ITALIA

*Timu ya weusi tupu yapanda daraja

Timu ya soka nchini Italia inayoundwa na Waafrika wahamiaji tupu imepanda kutoka daraja la chini kabisa nchini humo.

Timu hiyo, Koa Bosco, ilishinda kwenye mechi ya mtoano Jumapili na hivyo kuwa juu kabisa ya msimamo wa ligi katika Jimbo la Calabria Kusini. Maana ya jina la timu hiyo ni Watumishi wa Madhabahu.

Shirikisho la Soka la Italia lina mfumo wenye ngazi tisa, kuanzia Serie A ambayo ni Ligi Kuu hadi ile ya mwisho, Terza Categoria, ambayo ni ya ridhaa na ambako Koa Bosco wanaondoka.

Wanaounda timu hii ni wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi mbalimbali, zikiwamo Senegal, Ivory Coastna Burkina Faso. Jimbo waliloweka makazi ni moja ya maeneo masikini zaidi nchini Italia.

Wengi wa wachezaji wa timu hii huishi kwenye mahema au makontena katika kambi inayoendeshwa na Serikali ya Italia ikaribu na mji wa Rosarno, kusini mwa nchi.

Timu hiyo iliundwa na Padre wa Kanisa Katoliki, Roberto Meduri na inaendeshwa na kufundishwa na Wataliano wa eneo hilo.

"Si rahisi kuendesha mradi wa aina hii, kuna magumu mengi. Vijana hawa wamepiga hatua kubwa, ni ushindi na ni wazi kwao kwamba maisha ya kila siku yanasonga mbele," Mkurugenzi wa Koa Bosco, Domenico Bagala ananukuliwa na jarida la Il Calcio akisema.

Anaeleza kwamba kuanzia asubuhi hadi alasiri wahamiaji hao hufanya kazi kwenye mashamba yaliyo jiranina pia kwenye bustani za machungwa.

Haikuwa rahisi kwa timu hii kupanda daraja, kwani wachezaji walikuwa wakikashifiwa kwa sababu ya rangi yao, kwa mfano Machi mwaka huu wakicheza ugenini zilitokea fujo na wachezaji wao wakatupiwa mawe kutoka majukwaani.

Mechi hiyo ilivunjwa na baadaye timu zote zikaadhibiwa, ambapo wenyeji, Vigor Paravati waliambiwa kwamba hawakuonesha kitendo cha kimichezo.

Hata hivyo, tangu kupanda kwao daraja watu kutoka maeneo mbalimbali wamekuwa wakiwatumia salamu za pongezi na sifa.

Kocha wao, Domenico Mammoliti, amekuwa akitundika mtandaoni baadhi ya salamu hizo, akieleza mwenyewe kufarijika na kwamba huu ni mwanzo wataendelea kupanda madaraja.

Tayari timu hiyo imeanza kuwa na mvuto kwa klabu kubwa kamaJuventus, ambapo Mkurugenzi wa Juve, Pavel Nevded majuzi alialika kikosi chote na viongozi kwenye Makumbusho ya Juventus.

Hapo walikutana na wachezaji wa Juventus na wakabadilishana jezi kama kutakiana heri na pia kuwapongeza Koa Bosco kwa hatua waliyopiga.

Padre Meduri anasema awali alipounda timu hiyo alikuwa na nia ya kuwachanganya wageni katika jamii, kujenga urafiki na kusitisha hali mbaya iliyokuwapo, ambapo fujo zilipata kuua watu 53 kujeruhiwa baada ya Waafrika wawili kupigwa risasi 2010.

Ni mara chache Koa Bosco hupata ufadhili wa kifedha, lakini kwa kupanda daraja na kuanza kujulikana sehemu nyingi, wanatarajia mambo mazuri baadaye.

Hata hivyo, watu wa maeneo ya jirani wamekuwa wakikusanya na kutoa msaada wa mablangeti na mavazi ya kuwatia joto wachezaji.

Eneo wanaloishi lina ukosefu wa ajira na nahodha wa timu hiyo anayetoka Ivory Coast,Yaya Diallo, anaamini ni vyema Waafrika wengine wakabaki nyumbani ambako wanaweza kufanikiwa kuliko hatari ya kusafiri kwenda Italia.

Italia huwa na wahamiaji wengi ambao husafiri kwa boti kutoka Afrika wakipitia pwani ya Libya, na wengi hufia baharini katika kile wanachosema ni kwenda kutafuta maisha Ulaya.

PACQUIAO ASHUTUMIWA KWA UDANGANYIFU

Manny Pacquiao ameshutumiwa kwa kudanganya kuwa alikuwa akiumwa bega kabla ya pambano dhidi ya Floyd Mayweather. Pambano hilo lilipigwa Las Vegas,Marekani.

Iwapo Mfilipino huyo atakutwa na hatia, adhabu atakayopata kwa mujibu wa sheria itakuwa kifungo jela cha kati ya mwaka mmoja na miaka minne, na faini ya kufikia dola za Kimarekani $5,000 (£3,305).

Tume ya Michezo ya Nevada, NAC, imesema Pacquiao, mwenye umri wa miaka 36, hakutangaza kuwa majeruhi katika fomu ya maelezo kabla ya pambano.

Lakini Pacquiao anasema alikuwa muwazi na mpango wa matibabu ulikuwa umekubaliwa.

Pacquiao alisema kupigwa kwake kumetokana na maumivu - akidai kuwa alishindwa kutumia mkono wake wa kulia katika pambano hilo- lakini taarifa ya pamoja iliyotolewa na Team Pacquiao na mapromota wake Top Rank imesema Shirika la Marekani la Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kuongeza Nguvu Michezoni, Usada, lilijulishwa juu ya sula hilowakati wa kambi ya mazoezi ya mwana masumbwi huyo na pia katika usiku wa pambano.

Wamesema daktari mmoja wa Usada alizuia matumizi ya dawa moja ya kuzuia maumivu usiku wa pambano, lakini NAC haikuruhusu kutolewa kwa sababu hawakujua kuhusu kuumia bega.

Taarifa hiyo imesema: "Hii inakatisha tamaa kutokana na ukweli kwamba Team Pacquiao ilieleza kuhusu Pacquia kuumia bega na matibabu kwa Usada, ambao waliidhinisha matibabu na Manny aliorodhesha dawa katika fomu yake ya kabla ya pambano."

NAC imesema kambi ya Pacquiao haikulazimika kueleza kuhusu kuumia kwa bondia wake, lakini mkurugenzi mtendaji wao Bob Bennett amesema: "si tu kwamba hakujaza fomu kikamilifu,ni kwamba hakuwa mwaminifu. "Saa mbili kabla ya pambano walitaka dawa ya kutuliza maumivu. Suala hilo lilituweka katika mazingira magumu sana."

DANGOTE ATAKA KUINUNUA ARSENAL

Mtu tajiri barani Afrika Aliko Dangote amesema kuwa bado anataka kuinunua kilabu ya Arsenal licha ya kushindwa kufanya hivyo mwaka 2010 alipotaka kununua hisa za kilabu hiyo.

Bilionea huyo kutoka Nigeria ni tajiri mara nane ya alivyokuwa wakati alipojaribu kununua hisa za klabu hiyo na kwamba shabiki huyo wa Arsenal bado hajatupilia mbali ndoto yake ya kutaka kuinunua kilabu hiyo ya London Kaskazini.

''Bado nina matumaini kwamba siku moja nitainunua timu hiyo',' alisema Dangote mwenye umri wa miaka 58.

''Naweza kuinunua bei ambayo wamiliki wake itakua vigumu kukataa'', huku akiongezea kuwa ''najua mpango wangu''.

La kushangaza ni kwamba Dangote ametaja hadharani kwamba Arsene Wenger anafaa kubadilisha mbinu yake akisema kuwa timu hiyo inahitaji mwelekeo mpya.

Dangote ambaye ana thamani ya dola bilioni 15 ni tajiri zaidi ya Stan Kroenke ambaye anamiliki hisa nyingi katika kilabu hiyo na Bilionea raia wa Uzbek Alisher Usmanov ambao wamekuwa wakipigania udhibiti wa kilabu hiyo katika miaka ya hivi karibuni.

WAKIMBIZI TOKA BURUNDI WALIOINGIA NCHINI WAFIKI 1852

Idadi ya watu wanaoingia nchini kutoka Burundi kukimbia machafuko ya kisiasa kupitia mkoani Kigoma, imezidi kuongezeka kutoka 1,645 hadi kufikia 1,852.

Kati ya hao, 1,252 tayari wameshasajiliwa kama wakimbizi rasmi na kupelekwa katika kambi yaNyarugusu, wilayani Kasulu.

Hayo yalibainishwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, wakati wa mahojiano na NIPASHE.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo juzi, hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, mkoa huo ulikuwa umeshapokea idadi ya watu 500 walioingia kupitia vijiji sita vya Kibuye, Kagunga, Kosovo, Kakonko, Sekeeye na Kigaye.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, haliya usalama katika maeneo ya mipakani, imeimarishwa na kutoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo kutoa taarifa kwa uongozi wa vijiji iwapo kuna mgeni asiyefahamika kufika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Afisa wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, MauriceDavid, alisema hadi juzi jioni idadi ya wakimbizi walioingia mkoani humo ilifikia 1,645.

David alisema wakimbizi kutoka Burundi walianza kuingia mkoani humo Aprili 26, mwaka huu kupitia wilaya za mkoa huo na idadi kwenye mabano kuwa ni Buhigwe (156), Kigoma Vijijini (1,155), Kibondo (260, Kasulu (195) na Nyarugusu (64) ambao walikwenda moja kwa moja katika kambi hiyo bila kupitia katika vituo vya Uhamiaji.

Hata hivyo, aliongeza kuwa idadi ya wakimbizi waliofika kabla ya kuzuka upya kwa vurugu hizo nchini humo ilikuwa 46, lakini hadi jana mkoa mzima ulikuwa umepokea jumla ya wakimbizi takribani I, 852.

Burundi imekumbwa na vurugu kutokana na maandamano yanayofanyika kwenye mji mkuu wanchi hiyo Bujumbura, kwa wananchikupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutaka kugombea tena urais kwa muhula wa tatu kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

Katiba ya Burundi inataja muda wa urais kuwa ni vipindi viwili, lakini Rais Nkurunziza anadai kusimamia makubaliano ya Mkataba wa Arusha kwamba kipindi chake kilianza pale mkataba huo uliposainiwa, hivyo muda aliokuwa madarakani kabla ya kusainiwa usihesabiwe.

Chanzo: NIPASHE

CHENGE ATINGA KORTINI NA MAWAKILI 10

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, amefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na maazimio ya Bunge kuhusiana na malalamiko ya ukiukaji wa maadili ya uongozi.

Chenge, anatuhumiwa kupokea fedha kutoka kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd Sh. bilioni 1.6.

Chenge aliitwa katika Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo ambazo ni kinyume cha maadili. Hata hivyo, alipinga akisema kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kumhoji kwa kuwa liko katika Mahakama ambayo ina mamlaka kuliko baraza, na kueleza kuwa atafungua kesi ya kupinga mahakamani.

Katika maombi yake, lililowasilishwa masjala kuu ya Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Chenge ameorodhesha sababu 13 za kupinga mwenendo wa baraza na mapendekezo yaliyowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na shauri hilo.

Kwa mujibu wa hati yake ya maombi, anadai kwamba mwenendo wa Baraza na maazimio ya Bunge ya Novemba 29, mwaka 2014, yalikuwa ni kinyume cha amri iliyotolewa Novemba 25, mwaka 2014 ikisimamisha kwa muda kuwasilishwa na majadiliano ripoti iliyohusiana na uhamishaji wa fedhaza akaunti ya Tegeta Escrow.

Kesi hiyo imepangwa mbele ya jopola majaji watatu likiongozwa na Stella Mugasha, Augustine Mwarija na Dk. Fauz Twaib.

Majaji wamewaelekeza walalamikiwa ambao ni Tume ya Maadili ya Baraza la Maadili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha majibu yao Mei 8 na Mei 21, mwaka huu kesi hiyo itasikilizwa.

Jopo la mawakili 10 linalomwakilisha Chenge katika kesi hiyo linawajumuisha Deogratias Ringia, Wilson Ogunde, Jamhuri Johnson, Michael Ngalo, Respicius Didace, Okare Emesu, Cuthbert Tenga, Dosca Mutabuzi, John Nyange na Stephano Kamala.

Katika maombi yake, Chenge anaiomba mahakama kutoa amri yakudumu ya kuizuia Tume na Baraza kuendelea au kutafakari kuanzisha malalamiko yoyote dhidi yake kuhusiana na ripoti za CAG na PAC.

Kadhalika, anaiomba mahakama kutoa azimio kwamba malalamiko yaliyoanzishwa na tume kupitia baraza lake ni batili kutokana na ukiukaji wa taratibu na kwamba majadiliano ya Bunge na maazimio yake hayakuwa sahihi, hayakuwa ya kisheria, na kwa hiyo yalikuwa batili.

MGOMO WATIKISA TENA

Takribani siku 22 zikiwa zimepita tangu madereva wagome kutoa huduma za usafiri nchi nzima, leo wametangaza mgomo mwingine kutokana na ukimya dhidi ya madaiyao kwa serikali.

Madereva hao jana walitoa tamko lakuwapo kwa mgomo huo kupitia vyama vyao, huku wakikanusha kwamba watagoma sambamba na kuandamana.

Walisema leo watakuwa kwenye ofisi zao za muungano wao zilizopo Ubungo, jijini Dar es Salaam na hawatatoa huduma za usafiri.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Umoja wa Madereva na Chama cha Malori, Rashid Salehe, alisema, mgomo upo pale pale kwa madai kuwa bado kuna mambo ambayo yameendelea kuwa kikwazo kwao.

Alisema iwapo serikali haitatoa majibu ya kuridhisha, leo hawataingia barabarani kutoa huduma za usafiri.

Alisema jana walifanya mkutano wa madereva jijini Dar es Salaam huku ajenda kubwa ikihusu mgomo huo.

Alitaja baadhi ya sababu zinazowafanya wagome kwa mara nyingine kuwa ni serikali kutotekeleza madai yao likiwamo lakupewa ajira rasmi na waajiri wao.

"Msimamo wetu upo palepale kwamba kesho (leo) hatutaendesha magari..madereva wanaambiwa wezi, tunataka mikataba iboreshwe…tutakaa hapa hata ndani ya siku saba hadi serikali ije na kutoa majibu yanayoridhisha. Tunataka tupatiwe mikataba inayoeleweka na waajiri wetu mbele ya serikali," alisema na kuongeza:"Tumekaa katika kikao cha leo (jana)kwa ajili ya kuangalia maazimio ya kikao tulichokaa Aprili 29, mwaka huu…katika kikao hicho zaidi ya madereva 40 walisema hawana hela."


TABOA WAIPAANGALIZO SERIKALI

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu, alisema walipata taarifa zotekuhusu mgomo huo na kueleza kwamba wanaotangaza mgomo huo siyo madereva walioajiriwa.

Kwa mujibu wa Mrutu, madereva hao ndiyo waliosababisha magari yao kutoingia barabarani Aprili 11, mwaka huu na kuitaka serikali kuingilia kati suala hilo, vinginevyo leo magari hayataweza kuingia barabarani.


DARCOBOA: MGOMOUWE WA HIARI

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, alisema chama hicho kina taarifa kuhusu mgomo huo, lakini akaeleza kusikitishwa kwake kwa namna madereva wa vyombo vya usafiri wanavyowahusisha wao akisema hawahusiki.

Kutokana na hilo, Mabrouk aliomba mgomo huo usiwe wa lazima bali wa hiyari kwani si vyema kuwahusisha wao wanaohusika na daladala tena ndani ya mkoa na kupewa vitisho vya kupigwa mawe endapo gari lolote litakaidi agizo hilo.

"Serikali iangalie suala hili, kama kuna jambo lipo nyuma ya pazia basi liwekwe wazi….kama ni wa mikoani kwa nini wanatuhusisha sisi, tusitafute kuwasumubua wananchi," alisema mwenyekiti huyo wa Tarcoboa.

SUMATRA: WANANCHI WATASUMBULIWA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Gilliard Ngewe, alisema, suala hilo lipo katika wizara husika na kwamba kufanyika kwa mgomo huo kutaathiri wananchi kutokana na kukosa huduma za usafiri.

Hata hivyo, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (pichani), bila mafanikio kutokana na simu yake kutopatikana, huku Naibu wake, Charles Tizeba, akisema: "Naomba mnitafute kesho..nipo msibani."NIPASHE pia lilimtafuta Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu wake, Makongoro Mahanga, lakini simu zao hazikuwa hewani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alikaririwa na vyombo vya habari juzi akisema amepokea ujumbe mfupi wa simu kwamba leo kuna mgomo.

Tishio la mgomo wa leo ni mwendelezo wa mgomo mwingine mkubwa ambao ulidumu kwa takribani saa saba kwa mabasi kutokuruhusiwa kutoka katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo, Aprili 11, mwaka huu.

Madai ya mgomo huo ambao uliletaadha kubwa kwa wananchi yalikuwa ni kupinga ucheleweshwaji wa malori kwenye mipaka hususani ya Tunduma ambako hukaa kwa zaidi ya siku 26 licha ya kulipiwa kila kitu bandarini.

Mengine ni kupinga sheria namba G 31 ya mwaka 2015 ambayo inazungumzia faini ya Sh. 300,000 au kifungo cha miezi 21 kwa madereva wanapofanya makosa barabarani. Pia kupinga madereva kutakiwa kwenda Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kila baada ya miaka mitatu kwa ajili ya kujinoa.

Madai mengine yalikuwa ni wamiliki wa magari kutowashirikisha madereva katika mikataba yao ya kazi.

Hata hivyo, mgomo huo ulisitishwa baada ya serikali kupitia kwa Waziri Kabaka kufuta sharti la kwenda chuoni kila baada ya miaka mitatu.

Pia aliahidi kulipatia ufumbuzi sualala mikataba yao katika kikao kilichotarajiwa kufanyika wiki iliyofuata.


CHANZO: NIPASHE

RAIA 800 WA BURUNDI WAINGIA TANZANIA WAKIKIMBIA MACHAFUKO NCHINI KWAO

Idadi ya watu wanaokimbilia nchini kutafuta hifadhi kutokea Burundi imezidi kuongezeka huku Serikali ya Tanzania ikithibitisha kuwa jumla ya watu 800 wameingia na kuorodheshwa.

Raia hao wanakimbia machafuko ya kisiasa nchini humo yaliyoanza hivi karibuni.

Aidha, kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, watu 51 waliongia nchini wiki iliyopita kupitia mkoani, Kagera wamerudishwa makwao kutokana na kukiuka sheria na taratibu za uhamiaji.

Nantanga alisema wakimbizi hao walirudishwa Burundi kwa sababu kabla ya kuingia nchini walitokea Rwanda na huku akisisitiza kuwa sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa (UN) haziwahesabu kama wakimbizi kamili.

"Watu 51 waliongia nchini wiki iliyopita kutokea Burundi na kuingia mkoani Kagera wamerudishwa kwao kutokana na kuingia nchini kupitia Rwanda tofauti na sheria za Uhamiaji zinavyoelekeza," alisema Nantanga.

Aliongeza kuwa kati ya wakimbizi 800 waliongia nchini kupitia mkoaniKigoma, 720 tayari wamepelekwa katika kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoaoni humo.

Nantanga alisema mpaka Aprili 30, mwaka huu katika mkoa wa Kigoma watu 500 waliingia kupitia vijiji sita ambavyo ni vya Kibuye, Kagunga, Kosovo, Kakonko, Sekeeye na Kigaye.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, John Mongella, jana alithibitisha kuwa kuna raia wa Burundi wanaoingia mkoani humo, lakini alisema kutokana na kutokuwapo kwa kambiya wakimbizi, wamekuwa wakipelekwa mkoani Kigoma ambako kuna kambi ya kuwahifadhi.

"Wapo baadhi wanakamatwa na kurudishwa nchini mwao, lakini wengine tunawakabidhi mkoa wa Kigoma ambao kwa sasa una kambi kwa ajili ya kuwahifadhi, hata tukisema wakae hapa hatuna mahala pa kuwahifadhi," alisema Mongella.

Alisema kwa sasa mkoa wa Kagera hauna mpango wa kufungua kambi kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi hao, na kutumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutowapokea nakuwahifadhi watu hao na badala yake watoe taarifa wakati watakapoona wameingia katika maeneo yao.

"Waharifu nao wanaweza kutumia fursa hiyo kuingia, ninachowaomba wananchi wasijiingize katika masuala ya kupokea watu na kuwahifadhi, badala yake wawakabidhi kwa wenyeviti au maafisa watendaji walioko katika maeneo yao," alisema Mongella.

Burundi imekumbwa na vurugu kutokana na maandamano yanayofanyika kwenye mji mkuu wanchi hiyo Bujumbura, wakipinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutaka kugombea tena urais kwa muhula wa tatu, baada ya kumaliza muda wake wa mihula miwili.

Katiba ya Burundi inataja muda wa urais kuwa ni vipindi viwili, lakini Rais Nkurunziza anasema kwa mujibu wa makubaliano ya Mkataba wa Arusha, kipindi chake kinaanza pale mkataba huo uliposainiwa, hivyo muda aliokuwa madarakani kabla ya kusainiwa usihesabiwe.

Anasema kuwa, muhula huu ndio utakuwa kipindi chake cha pili na cha mwisho.

Hata hivyo, upinzani unapinga na yamekuwepo maandamano kuanzia Jumamosi ya kupinga hatua hiyo, natayari watu kadhaa wametiwa nguvuni na baadhi wanadaiwa kupoteza maisha.

CHANZO: NIPASHE

VIKONGWE WAKAMATWA NA MAGOBOLE

JESHI la Polisi mkoani Katavi linawashikilia watu tisa wakiwemo vikongwe wa miaka 80 na 70 baada ya kukamatwa wakiwa na bunduki tatu za kienyeji aina magobole, risasi zake 15, mtambo wa kutengenezea silaha, baruti na sare za Jeshi la Wananchi la Ulinzi na Usalama (JWTZ).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ,Dhahiri Kidavashari alitaja vitu vingine vilivyokamatwa kufuatia msako mkali unaoendelea wilayani Mlele ni vipande tisa vya nondo, vyuma vya kutengenezea risasi na mafuta ya kiboko yaliyohifadhiwa kwenye chupa.

"Mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri kati Jeshi la Polisi, askari wa Tanapa na raia wema ambapo wamekuwa wakiendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kufanikisha katika ukamataji," alieleza.

Alidai kuwa silaha hizo zilikuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria na zilikuwa zikitumika katika visa vya kijangili na uhalifu mwingine wilayani Mlele.

Akizungumza kwa njia ya simu, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Lazaro Zakaria (63) aliyekamatwa akimiliki gobole bila kuwa na kibali, Shaaban Mussa (52) gobole bila kuwa na kibali na Robert Kaumba (80).

Wengine ni Hamisi Rehani (70) alikamatwa akiwa na mtambo wa kutengenezea silaha aina ya gobole bila kuwa na kibali, Benedict Simon (52) akiwa na risasi 15 za gobole, vipande tisa vya nondo, vipande vyamiti, mtutu mmoja na baruti ndani ya chupa na Shaaban Mussa (52) alikamatwa akiwa na risasi moja ya gobole bila kibali.

Kwa mujibu wa Kidavashari, katika msako huo pia jeshi hilo lilimtia mbaroni Esther John (21) akiwa na sare ya JWTZ na vyuma viwili vya kutengenezea risasi na Mashaka George (32), alikamatwa akiwa na mafuta ya kiboko aliyoyahifadhi kwenye chupa.

Alieleza kuwa watuhumiwa wote, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa upelelezi na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

WATU WAWILI WAUAWA KWA RISASI MJINI TEXAS

Polisi mjini Texas wanasema kuwa wamewapiga risasi na kuwaua watu wawili waliokuwa nasilaha, waliowashambulia walinda usalama kwa risasi, walipofika katika eneo la hafla moja yenye utata ya uchoraji wa vibonzo vya kuwakejeli waislamu na mtume Mohammed.

Duru za habari zasema kuwa kisa cha ushambuliaji wa risasi kimefanyika katika sherehe moja, iliyokuwa ikifanyika mjini Dallas, mahala ambapo waandalizi walikuwa wakiendesha onyesho hilo.

Hafla za Sherehe hiyo iliyoandaliwa na kundi moja la kisiasa la kihafidhina, ambalo limekuwa likikejeli Uislamu, lilikuwa litoe zawadi nono ya dola milioni kumi kwa mchoraji kibonzo mahiri zaidi, atakayeibuka mshindi kwa kumchora mtume Mohamed.

Mwanasiasa kutoka Uholanzi Geert Wilders -- ambaye anafahamika kwa matamshi yake dhidi ya kuwadunisha waislamu, alikuwa msemaji mkuu katika hafla hiyo.

Aliyeshuhudia ameiambia BBC kuwa, aliwaona maafisa wa polisi wakimtia mbaroni mshukiwa wa tatu, ambaye alionekana kuwa hana silaha.

Kikosi cha kutegua mabomu pamoja na ndege za helikopta za polisi zimefika mahali hapo kwa sasa.

MKUU WA MAJESHI BURUNDI AWAONYA WANASIASA

Mkuu wa majeshi nchini Burundi Meja Jenerali Prime Niyongabo ametoa wito kwa wanasiasa kutotumia jeshi la taifa kwa manufaa yao ya kisiasa.

Jenerali Niyongabo amekariri tangazo lililotolewa na waziri wa ulinzi Jumamosi kuwa jeshi la nchi hiyo litahakikisha kuwa mkataba wa Arusha umetekelezwa kikamilifu na kuwa jeshi hilo halitumiwi na mtu au chama chochote cha kisiasa.

Kuhusiana na maandamano yanayoendelea, mkuu huyo wa jeshi amesema kuwa maandamano hayo sio halali na wanaichi wanapaswa kutumia mbinu za sheria zilizopo kutatua mizozo yao.

Wakati huo huo Meja Jenerali Niyongabo amesema jeshi hilo litasalia kuwa lenye nidhamu ya hali ya juu na tiifu kwa taifa la Burundi na wala sio kwa mwanasiasa yeyote.

Ameongeza kusema kufikia sasa jeshi limefanya kazi nzuri kuhakikisha kuwepo kwa usalama nchini Burundi na katika mataifa mengine wanakohudumu katika vikosi vya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika.

Mkuu huyo wa majeshi amesema wanajeshi wataendelea kushirikiana na polisi kushika doria ili kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo nchini Burundi.

Huku hayo yakijitokeza muungano wa upinzani umesema kuwa maandamano yataendelea siku ya Jumatatu baada ya mapunziko ya siku mbili.

Upinzani umepinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu kama rais.

Viongozi wa upinzani wanasema kuwa Rais Nkurunziza ni sharti atekeleze mkataba wa Arusha ambao ulimaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi.

Lakini chama tawala cha CNDD FDD kimepinga madai hayo na kusema kuwa Rais Nkurunziza anatumikia muhula wake wa kwanza kwa sababu, miaka mitano ya kwanza ilikuwa kipindi cha mpito na hakuchaguliwa na raia kama inavyohitajika kisheria.

Wakaazi wa mji mkuu wa Bujumbura wameshuhudia uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu kama vile petroli, na kadi za simuza muda wa mazungumzo huku kukiwa na misururu mirefu katika vituo vya kununua mafuta.

Idadi kubwa ya raia wa Burundi wamekimbilia nchi jirani kwa hofu ya kuzuka mapigano zaidi.

MATEKA WASIMULIA MATESO YA BOKO HARAM

Wanawake na watoto waliokuwa wakishikiliwa mateka na kikundi cha Kiislam cha Boko Haram kaskazini mwa Nigeria wamesema baadhi yao waliuawa kwa kupigwa mawe na wapiganaji wa Boko Haram wakati jeshi lilipokaribia kuwaokoa.

Walikuwa wakizungumza siku moja baada ya karibu mateka mia tatu kuokolewa kutoka msituwa Sambisa na kuwapeleka katika kambi ya serikali.

Mwanamke mmoja ambaye alijifungua akiwa mateka ameelezea namna wapiganaji hao walivyomkata koo mumewe wake mbele yake, kabla mwanamke huyo kutenganishwa na watoto wake wengine watatu.

Mwandishi wa Associated Press ambaye aliotembelea kambi hiyoamesema wengi wa watoto waliokolewa walikuwa wanaugua utapiamlo mkali.

Jeshi la Nigeria limesema limewaokoa zaidi ya watu mia saba katika kipindi cha wiki moja iliyopita wakati wa mapigano makali yanayoendelea dhidi ya Boko Haram.

MELI YA TANZANIA YAKAMATWA NA TANI 3 ZA COCAINE UINGEREZA

Kwa mara nyingine, Jina la nchi limeendelea kuchafuka baada ya Meli ya MV Hamal iliyosajiliwa Tanzania kukamatwa barani Ulaya ikiwa imebeba shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine yenye uzito wa tani tatu.

Kama dawa hizo haramu zingeuzwa mitaani nchini Uingereza, zingekuwa na thamani ya Sh1.5 trilioni, kiasi ambacho nchi wafadhili zinatarajiwa kuichangia Tanzania kwenye bajeti ya mwaka 2015/16.

Matukio mengine yaliyoichafua nchi ni la meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Tanzania ambayo ilikamatwa Septemba 2013, jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterranian nchini Italia wakati ikielekea Uturuki ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni 50 milioni za Uingereza (sawa na Sh125 bilioni). Tukio jingine ni lile la Watanzania wawili kukamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya Sh6 bilioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.

Kiwango hicho cha dawa zilizokamatwa kimeweka rekodiya ukubwa wa mzigo wa dawa hizo haramu nchini Uingereza. Awali shehena ya cocaine iliyokuwa kubwa ilikamatwa Septemba mwaka jana ikiwa na mzigo wenye thamani ya Sh 450 bilioni.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, meli ya MV Hamal ilikamatwa kwenye Bahari ya Kaskazini na baada ya kupekuliwa kwenye bandari ya Arberdeen nchini Scotland, ilikutwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya cocaine.

Meli hiyo yenye urefu wa mita 32 na uwezo wa kubeba tani 422, ilikamatwa na askari wa kikosi cha majini cha Royal Navy waliokuwa kwenye meli ya HMS Somerset pamoja na askari wa uhamiaji wa Border Force waliokuwa kwenye meli ya Valiant, karibu kilomita 160 mashariki mwa mji wa Aberdeen Alhamisi baada ya kupewa taarifa na kitengo cha makosa ya jinai, NCA.

Baadaye, meli hiyo ilipelekwa bandari ya Aberdeen, ambako maofisa wa Border Force wenye stadi maalumu ya upekuzi, waliipekua meli hiyo kwa kusaidiana na polisi wa Scotland.

John McGowan – afisa mwandamizi wa uchunguzi wa NCA, alisema: "Upekuzi wa meliulikuwa mrefu na unaosababisha maumivu, na uliofanywa na watu wenye utalaamu mkubwa wa kufanya kazi kwenye mazingira magumu.

"Matokeo yake ni ugunduzi huu mkubwa – unaoaminika kuwa mkubwa kuwahi kutokea kwenye rekodi nchini Uingerezana ambao unaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya fedha."

Hata hivyo, rekodi za mtandao wa shughuli za baharini unaonyesha kuwa katikati ya Februari, meli hiyo ilikuwa Uturuki na wiki mbili zilizopita ilianza safari kutoka visiwa vya Tenerife nchini Hispania na ilipokamatwa ilikuwa inaelekea Hamburg, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ujerumani ikitazamiwa kufika jana usiku.

Meli hiyo imekutwa na watu tisa wenye umri kati ya miaka 26 na 63 wote raia wa Uturuki na wameshitakiwa kwa kukutwa na dawa za kulevya. Washitakiwa wote hawakusema lolote waliposomewa mashtaka yao. Washitakiwa hao ni Mustafa Ceviz, 54, Ibrahim Dag,47, Mumin Sahin, 45, Muhammet Seckin, 26, Umit Colakel, 38, Kayacan Dalgakiran,63 na Emin Ozmen, 50, wote wanatoka jiji la Istanbul. Wengine ni Abdulkadir Cirik, 31, anayetoka Mersin na Mustafa Guven, 47, kutoka Yozgat, nchini Uturuki. Walifikishwa mahakamani Jumatatu.

MIKOPO YA WANAFUNZI HESLB YAIVA

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), jana imetoa mwongozo kwa wanafunzi wahitaji wanaotarajia kuomba mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2015/2016 unaotarajiwa kuanza miezi michache ijayo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, ambao unapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz), waombaji wamepewa miezi miwili kuwasilisha maombi yao kuanzia Jumatatu (Mei 4) hadi Jumanne (Juni 30, 2015).

Mwongozo huo uliotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatega, unasema wanafunzi wote wahitaji wa mkopo na ruzuku wanapaswa kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum kupitia mtandao unaojulikana kama"Online Loans Application and Management System" ulioanzishwa na HESLB kwa ajili ya kupokea maombi hayo.

Mfumo huo unapatikana kupitia tovuvi ya Bodi au kwa kufungua kiunganishi chake (http://olas.heslb.go.tz).Mwongozo huo pamoja na mambo mengine, unafafanua kuwa waombaji wa mara ya kwanza wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Sh. 30,000 na kisha kutumia namba ya muamala na kuingia katika mtandao na kuanza kujaza fomu za maombi.

"Waombaji wa mara ya kwanza wanapaswa kulipa ada ya maombi ya Sh. 30,000 ambayo inalipwa mara moja tu na haitarudishwa kwa njia ya M-Pesa," inasisitiza sehemu ya mwongozo huo.

Aidha, imesisitizwa kuwa wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea namasomo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu, hawapaswi kuwasilisha maombi tena.

Kwa mujibu wa Nyatega, Bodi imewasihi waombaji na wadau wengine kuusoma na kuuzingatia mwongozo huo wakati wote wanapofanya na kuwasilisha maombi.

HESLB ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu.

Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.

WATU WATATU WAUAWA SHAMBULIZI LA BOMU BURUNDI

Watu watatu wameuawa katika shambulizi la bomu lililowalenga askari polisi nchini Burundi ambapo zaidi yawatu mia sita wametiwa mbaroni wakati wa maandamano na ghasia za kupinga raisi wa taifa hilo Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu wa kiti cha urais.

Mkuu wa Polisi nchini humo Generali Andre Ndayambaje amesema kuwa maafisa wawili wa polisi waliuawa na mmoja kujeruhiwa katika wilaya ya Kamenge ya mji mkuu wa Bujumbura.

Shambulizi kama hilo linatajwa kutekelezwa katikati mwa jiji hilo ambapo maafisa watatu walijeruhiwa.

Afisa mmoja wa polisi ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema kuwa ni wazi kuwa waandamanaji wameanzisha mashambulizi ya ghafla na ameongeza kuwa ikiwa raia hao wanataka vita watakiona cha mtema kuni.

UKAWA WATOA TAMKO JUU YA NJAMA ZA KUAHIRISHA UCHAGUZI

Vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA vimetoa msimamo wao juu ya njama za kuahirisha uchaguzi mkuu unaotakiwa kufanyika OCTOBA mwaka huu na kwamba hawako tayari serikali iliyopo madarakani iongezewe muda,huku ukiitaka tume kutoka hadharani na mpango maalum na ratiba nzima ya maandalizi ya uchaguzi mkuu badala ya kuishia kusema kuwa uchaguzi uko pale pale.

Akielezea msimamo huo jijini dar es salaam mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI Mh. James Mbatia amesema endapo tume ya uchaguzi itaendelea na utaratibu uliotumika mkoani njombe itatumia zaidi ya miaka 10 kuandikisha na kuongeza kuwa kwa sasa suala la kura ya maoni liwekwe pembeni na serikali isitishe mambo yote yasiyokuwa ya msingi ielekeze nguvu zake kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura ili limalizike kwa wakati.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chadema Mh Freeman Mbowe amesema hakuna mgawanyiko ndani ya ukawa licha ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale na kwamba tayari wameshafanya mgawanyo wa majimbo kwa asilimia 95 ambayo wamekubaliana isipokuwa majimbo 12 ambayo bado wanavutana lakini bado wako kwenye masahauriano.

Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahimu Lipumba amesisitiza kuwa UKAWA haiungi mkono jaribio lolote la kufanya marekebisho ya katiba ya sasa kwa lengo la kuongeza muda wa utawala uliopo madarakani kwani kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba ya nchi na ukiukwaji wa sheria huku akiitadharisha serikali kutokuipeleka nchi kwenye machafuko yanayotokea burundi hivi sasa.