MTIKILA ATAKA MAHAKAMA YA KADHI ISIJADILIWE

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ameiomba Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kutoa amri kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusitisha kujadili suala lolote linalohusu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Mtikila aliwasilisha maombi yake jana mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Richard Mziray, anayesaidiana na Jaji Lawrence Kaduri na Said Kihio.

Kesi ya msingi ambayo Mtikila anaomba Mahakama ya Kadhi isiruhusiwe nchini, ilipangwa kutajwa jana.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Gabriel Malata na Kasori Sarakikya, ulidai kuwa utawasilisha majibu ya maombi ya Mtikila leo.

Mtikila alidai kuwa anaomba kuwasilisha hati ya dharura mahakamani akitaka bunge hilo lisijadili wala kuzungumzia suala la Mahakama ya Kadhi.

"Ina maana suala hili baada ya kufunguliwa mahakamani linajadiliwa huko nje ya Mahakama?," alihoji Jaji Mziray na kuitikiwa na Mtikila.

Jopo hilo lilisema upande wa Jamhuri uwasilishe majibu ya maombi ya Mtikila kwa njia ya maandishi leo na kesho kesi hiyo itatajwa.

Mtikila alifungua kesi ya madai kupinga kitendo cha serikali kupeleka muswada bungeni wa kutunga sheria ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, kwamba kuanzishwa kwake ni kinyume cha Katiba ya nchi.


Mtikila ameiomba Mahakama itoe amri kwamba wale walio kwenye mamlaka ya serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano naUratibu), Mary Nagu; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na wenzao, watoe sababu kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka mitano ikiwa watashindwa kujieleza.

Pia, Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14 yamwaka huu, ameomba Mahakama itoe amri ya vigogo hao kufungwa kifungo hicho kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.

Katika hati yake, Mtikila pia anaiomba Mahakama itoe amri kwamba Mahakama ya Kadhi na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC), itangaze kuwa ni haramu kwenye ardhi ya Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Mtikila anadai kuwa suala la serikali kuandaa Muswada wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo cha Bunge kukubali zaidi ya kuukataa ni sawa na uhaini, kinachofanywa na waliopanga kuupeleka muswada huo bungeni.

Anaendelea kudai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo vya viongozi hao walivyoapa wakati wa kushika nafasiza uongozi wa umma na ni kinyume cha kifungu cha 19 cha Katiba ya nchi kinachoeleza kwamba masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kuongeza kuwa uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya nchi.

CHANZO: NIPASHE

MSHINDI WA URAIS KUTANGAZWA

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Nigeria INEC, Attahiru Jega, amesema kuna uwezekano wa kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa rais nchini humo ifikapo leo jioni kama zoezi la kuhesabu kura litamalizika mapema.

Jega amesema kuwa jumuiya ya kimataifa inaweza kuipongeza Nigeria jinsi ilivyoendesha uchaguzi mkuu.

"Tuna amini zoezi la kupiga kura limeenda vizuri ingawa kumekuwepo na changamoto mbalimbali lakini hatuwezi kuzipuuzia.
Ni hakika haukuwa muda kamilifu lakini tunaaminikwa ujumla tumefanya vizuri, japokuwa bado tunayo nafasi ya kuzidi kuboresha upigaji kura. Ndiyo maana tuliwaalika waangalizi vikiwemo vyombo vya habari na waangalizi wengine wa uchaguzi, ili kuweza kutangaza habari za uchaguzi na tunaweza kujifunza kutokana na ripoti zitakazotolewa na vyombo hivi pia tunaweza kuendelea kuboresha mchakato wa uchaguzi", amesema Jega.

Upigaji kura umeendelea kwa siku mbili kutokana na kutokea hitilafu katika kadi za kielektroniki na kuchelewesha usajili kwa baadhi ya wapiga kura.

Matokeo ya awali yamepangwa kutangazwa ndani ya saa 48 baada ya uchaguzi.

15 MBARONI JARIBIO LA KUMTOROSHA GWAJIMA

JESHI la Polisi linawashikilia na kuwahoji watu 15 kwa tuhuma za kutaka kumtorosha kutoka Hospitaliya TMJ Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo jijini, Dar es Salaam, Joseph Gwajima aliyelazwa hapo tangu usiku wa kuamkia juzi.

Gwajima amelazwa ikielezwa hali yake ilibadilika wakati akihojiwa na makachero wa Polisi waliokuwa wanamhoji baada ya kujisalimisha baada ya kutakiwa kufanya hivyo kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo.

Kukamatwa kwa watu hao, wakiwemo wachungaji sita, mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu chaDar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), Dar es Salaam kumethibitishwa na taarifa ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Katika taarifa yake, amesema watu hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama pamoja na kujaribu kumtorosha Askofu Gwajima ambaye amelazwa katika Hospitali ya TMJ kwa matibabu.

Alisema saa tisa na nusu usiku wa kuamkia jana, watu 15 walifika hospitalini hapo kwa lengo la kumuona mgonjwa huyo.

"Askari ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia mashaka watu hao hivyo waliwakatalia kuingia. Na hapo walijaribu kutumia nguvu, lakini walikamatwa," alisema.

Kova alisema baada ya kuwapekua, watu hao walikutwa na begi lenye bastola aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za Short gun na vitabu viwili vya hundi.

Alisema begi hilo pia lilikuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundicha Benki ya Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya Simu na Tablets, suti mbili na nguo za ndani.

Aliwataja waliokamatwa ni Chitama Mwakibambo (32), fundi seremala mkazi wa Gongo la Mboto, Mchungaji Edwin Audex (24) mkazi wa Kawe Maringo, Adam Mwaselele(29), mhandisi na mkazi wa Kawe Maringo, Frederick Fusi (25) mkazi wa Mbezi Beach.

Wengine mwanafunzi wa chuo cha IMTU, Frank Minja (24) mkazi wa Mbezi Beach, Emmanuel Ngwela (28) mkazi wa Keko juu ambaye ni mlinzi shirikishi, Geofrey William (30), Mhadhiri UDSM mkazi wa Survey Chuo Kikuu, Mchungaji Mathew Nyangusi (62) mkazi wa Mtoni Kijichi, mchungaji Boniface Nyakyoma (30) mkazi wa Kitunda.

Pia wametajwa Geofrey Andrew (31), dereva mkazi wa Kimara Baruti, Mchungaji David Mgongolo (24) mkazi wa Ubungo Makoka, Mfanyabiashara George Msava (45) mkazi wa Ilala Boma, Mchungaji Nicholaus Patrick (60) mkazi wa Mbagala Mission, George Kiwia (37) ambaye ni dalali wa magari na mkazi wa Tandale Uzuri na mchungaji Yekonia Bihagaze (39) mkazi wa Kimara Stop Over.

Kova alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni yakubaini sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote zilizotumika kutaka kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.


Pengo Asamehe

Wakati hayo yakiendelea, jana Pengo aliwatangazia waumini wake kumsamehe Gwajima na pia kuwataka waumini wake pia wamsamehe.

Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph ambako iliendeshwa misa ya Jumapili ya Matawi, alitoa msamaha kwa Gwajima na kusema kuwa hana chuki na mtu yeyote.

Aidha, Pengo alisema hawezi kuingilia hatua ya Polisi kumhoji kiongozi huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.

Gwajima: Niombeeni Aidha, katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Gwajima amewaomba waumini wake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili aweze kuendelea na kazi aliyotumwa na Mungu ya kuhubiri Injili.

Taarifa iliyotolewa na kusomwa kanisani kwake imedai kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri na afya yake imeanza kuimarika. Alisema waumini wake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili kuendelea na kazi aliyotumwa na Mungu ya kuhubiri injili.Kiongozi huyo bado amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na anaendelea kupatiwa matibabu ya karibu na madaktari kutokana na hali yake kubadilika mara kwa mara.

Hata hivyo, kwa taarifa iliyotolewa na daktari anayemtibu askofu Gwajima, Fortunatus Mazigo, alisema hali ya mgonjwa inaendelea vizuri japokuwa alikataa kusema ni nini tatizo linalomsumbua hadi akamilishe kukusanya taarifa ya vipimo vyote ambavyo vingine bado majibu yake hayajapatikana na huenda kila kitu kikawa hadharani leo.

Chanzo:Habari Leo

BABA AWABAKA MABINTI ZAKE

Mkazi mmoja wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani amekamatwa na polisi akituhumiwa kuwabaka watoto wake wawili wadogo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Habari zilizolifikia gazeti hili, zilisema kuwa katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na polisi na watoto wenyewe, baba huyo alianza kuwafanyia binti zake vitendo hivyo mwaka 2013 kwa siku ambazo mkewe ambaye nimama wa wasichana hao hakuwapo hadi usiku wa Machi 19, mwaka huu. Kwa sasa tunayahifadhi majina ya familia hiyo.

Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 15 anayesoma darasa la saba na mdogo wake mwenye umri wa miaka 11 aliyeanza kubakwa akiwa darasala tatu.

Kwa mujibu wa watoto hao, baba huyo alikuwa anamuita mmoja wa watoto wake chumbani kwake na kumtaka alale na mdogo wao wa kiume wakati huo akiwa na mwaka mmoja na binti akipitiwa na usingizi humvua nguo za ndani na kumwingilia huku akimtaka kukaa kimya na kuvumilia maumivu.

Mke wa mtuhumiwa huyo, ambaye amekuwa akizimia mara kwa mara kutokana na kulia baada ya kubaini mchezo huo, alisema aligundua watoto wake wanabakwa Ijumaa iliyopita baada ya mmoja wa mabinti zake hao kumweleza kuwa baba yake alikuwa amembaka Machi 19, mwaka huu.

Alisema kabla ya binti huyo kumweleza hivyo, alimwomba asimpige kwani kuna kitu anataka amweleze, japo ni kibaya lakini yeye amechoshwa na kimekuwa kikimuumiza kichwa.

"Alisema kila ninapokwenda katika biashara zangu, anatamani nisiwe ninawaacha hapo, nikamwahidi sitamfanya kitu ili mradi aseme ukweli tu," alisema mama huyo.

Baada ya kuhakikishiwa kulindwa, ndipo binti huyo aliposimulia jinsi ambavyo baba yake amekuwa akiwafanyia na kuwatishia wakipiga kelele atawaua.

"Niliposikia mwili ulisisimka na ghafla binti yangu mwingine naye akatokea akilia na kuniambia, 'hata mimi baba ananifanyiaga hivyohivyo kila siku unapokuwa umepeleka mboga sokoni Kariakoo," alisema mama huyo.

Mwanamke huyo ameomba sheria ichukue nafasi yake katika tukio hilo kwa kuwa ni la kinyama na pia wataalamu wa saikolojia wamsaidie binti yake mdogo wa darasa la tano kwani yeye ameathirika zaidi.

Daktari aliyewapima watoto hao, ameshauri binti huyo mdogo apate ushauri zaidi ili kurudisha akili yake katika hali ya kawaida.


Simulizi za watoto

Wakizungumza nyumbani kwao jana watoto hao, walisema babayao alikuwa akiwatishia kuwakatakata kwa panga au kuwakaba koo humohumo chumbani endapo wangethubutu kumweleza mtu yeyote kitendo wanachokifanya.

"Tulikuwa tumeingia kwetu kulala na wadogo zangu, nikasikia ananiita nikambembeleze mtoto eti anamsumbua, nilikwenda nikambembeleza akalala, wakati nashuka kitandani kurudichumbani kwetu baba akanivutakwake akanivua, akasema anachokifanya ni suna kwa hiyo hataki kelele, akisikia atanikaba nife."

"Niliumia sana na asubuhi mama alirudi nikajitahidi kweli asijue na hata shule sikwenda, jioni mama aliondoka tena baba hakuniita siku hiyo lakini baada ya siku tatu aliniita tena ikawa vilevile navumilia. Siku zilivyozidi unaweza kukuta kwa wiki naitwa hata mara nne siku ambazo mama hayupo nyumbani," alisema.

Watoto hao walieleza kuwa baadaye baba huyo alihamia kwa binti mdogo kwa staili ileilena kila mmoja alikuwa akiitwa kwa zamu na kwa vile kila mmoja alijua ni siri yake na baba. Kutonaka na woga wa kuuawa, hakuna aliyemweleza mwenzake hadi katikati ya mwaka jana mmoja wao alipomweleza mwenzake na baadaye kumweleza mama yao.

"Baba alikuwa anasema atatuua bila hata mtu kujua na tutaozea shambani, hata nikiwa katika siku zangu baba ananiingilia hivyohivyo, naugua kila mara UTI, mdogo wangu naye kila mara UTI, tukaamua liwalo na liwe kama kufa basi ila mama ajue," alisema mtoto huyo huku akibubujikwa na machozi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembe Saba, Hamis Shomari alisema kabla ya kupelekwa kituo cha polisi Kongowe Jumamosi iliyopita, watoto hao waliitwa shuleni hapo na kuhojiwa kila mmoja peke yake na wote walikiri kuanza kubakwa mwaka 2013 na baba yao na kwamba tabia hiyo iliendelea hadi Machi 19 usiku alipobakwa binti mdogo kwa mara ya mwisho na Machi 20 walipoamua kumweleza mama yao.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na kwamba wasichana hao wamefanyiwa vipimo mbalimbali na majibu ya daktari yamethibitisha kuwa wamebakwa na sehemu zao za siri zimeharibiwa, hivyo wanaendelea na matibabu.


Chanzo: Mwananchi

GWAJIMA ASAKWA NA POLISI KWA KUMKASHIFU PENGO

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya tuhuma za Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima za tuhuma za kumkashifu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Mwadhamana Polycarp Kardinali Pengo.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamandawa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ilisema Askofu huyo anatakiwa kujisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi, ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

"Tumepokea malalamiko ya kukashifiwa na kutukanwa hadharani kwa Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo ambaye ni kiongoziwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania," alidai Kamanda Kova na kuongeza kuwa kashfa na matusi hayo, yamefanyika kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Aidha, alidai kwamba kuna sauti iliyorekodiwa (audio) na picha za video (video clip) zikimuonesha Askofu Gwajima akimkashfu na kumtukana Kardinali Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.

Alidai taarifa ya kumtaka Askofu Gwajima ajisalimishe haraka, inatokana na juhudi za kawaida ili kumpata kushindikana.

"Ni muhimu kwa Askofu Josephat Gwajima kuripoti yeye mwenyewe badala ya kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii," ilisema taarifa ya Kamanda huyo.

MBARONI KWA KUKUTWA NA VIUNGO, MIFUPA YA ALBINO

WATU wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera kwa kosa la kukutwa na viungo mbalimbali vya mwili ikiwemo mifupa mitatu ya mtu mwenye ulemavu wa ngozi (albino).

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Henry Mwaibambe alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi katika kijijicha Kyota kata ya Kimwani wilayani Muleba mkoani humo baada ya jeshi hilo kuweka mtego kwa watuhumiwa hao ambao walikuwa wanatafuta wateja wa viungo hivyo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni James Rutozi (66) mkazi wa Kimwani ambaye ndiye aliyekuwa anahifadhi viungo hivyo na Emanueli Kaloli (50)ambaye pia ni mkazi wa Kimwani aliyekuwa anatafuta mteja wa viungo hivyo.

Alisema mara baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanauza viungo hivyo kwa Sh milioni 3 waliweka pesa za mitego na kujifanya wao ni wateja na ndipo walipowakamata watuhumiwa hao wawili ambao walikutwa na mfupa mmoja na walipowabana zaidi ndipo walitoa mifupa miwili.

Alisema mnamo mwaka 2006 katikakijiji cha Rushwa kata ya Mushabago wilayani Muleba, Zeulia Jestus akiwana miaka 24 mwenye ulemavu wa ngozi (albino) alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua na ndipo watuhumiwa hao walifukua kaburi hilo mwaka 2008 kwa maelekezo ya mganga wa jadi.

Alisema pia walipotaka kujiridhisha jeshi hilo liliomba kibali mahakamani ili kufukua kaburi hilo mnamo Machi 23, mwaka huu lilipofukuliwa liligundulika kuwa viungo hivyo vimetolewa katika mwili wa marehemu huyo.

Aidha, jeshi hilo linamtafuta mganga wa jadi aitwaye Mutalemwa Revocatus ambaye ametoroka kabla hajakamatwa ambaye ndiye aliyewashawishi wafukue hilo kaburina kuwapa dawa ya kinga ili wasidhurike wakati wanafukua.

Aliongeza kuwa mnamo mwaka 2008 wananchi wa kata hiyo ya Mushabago walitoa taarifa kwa Jeshila Polisi kuwa kaburi alilozikwa marehemu Zeulia lilifukuliwa na watu wasiojulikana baada ya kugundua tukio hilo.

CCM WAMUONYA TENA LOWASSA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema vitendo vinavyofanywa na Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa niukiukwaji wa Katiba na kanuni za chama hicho.

Aidha, kimesema vitendo vinavyofanywa na Lowassa ni kampeni za wazi za urais anazoendesha kabla ya muda kufikana hivyo kukiuka Katiba na kanuni za CCM na kuonya kuwa kama ataendelea na kampeni hizo haramu atapoteza sifa za kugombea nafasi ya urais.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitoa ufafanuzi huo baada ya waandishi wa habari waliopo katika msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinanakutaka ufafanuzi wa kinachoendelea mjini Dodoma kwa makundi tofauti kwenda kwa Lowassa kwa madai ya kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Nape akizungumzia suala hilo alisema, "Anachokifanya Lowasa ni kuvunja kanuni na kiburi, ni matendo ya wazi ya kampeni, bila shaka anajua adhabu yake. Matendohayo yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia CCM.

"Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa aliongeza kuwa Lowassa ni miongoni mwa wanaCCM ambao walipewa adhabu na CCM mwaka mmoja uliopita kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao. Nape alisisitiza kuwa matendo yanayoendelea hivi sasa ni dhahiri kuwa ni kiburi kisicho na maana dhidi ya CCM."

Lowasa anajua utaratibu wa Chama katika kuwapata wagombea wake kwa ngazi mbalimbali kuanzia udiwani mpaka urais hivyo kuendelea na matendo ambayo yanatafsiri ya wazi kuwa ni kampenini kiburi cha wazi. "Kwa matendo hayo ya Lowassa labda dhamira iwe ni kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya Urais kupitia chama kingine na si CCM."

Nape alisema ni vyema wagombea wa ngazi mbalimbali wakahakikisha wanazingatia Katiba na kanuni za chama hicho ili wasiingie kwenye kundi la kutokuwa na sifa ya kuomba ridhaa ya kugombea udiwani, ubunge na urais.

"Tunaendelea kukumbusha na kusisitiza kwamba wale wote wenyenia ya kugombea kupitia chama chetu kuheshimu kanuni na tararibu za kupata ridhaa kugombea kwa ngazi ya chama chetu," alisema Nape.

Lowassa amedaiwa kuwa amekuwa akitumia makundi mbalimbali kufanya kampeni ambapo alianza nakikundi cha wajasiriamali jimboni Monduli mkoani Arusha ambapo walienda nyumbani kwake kumuomba agombee.

Hatua hiyo ilifuatiwa na mashehe 50 kutoka wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambao nao walikwenda nyumbani kwa Lowassa Dodoma kwa lengo la kumshawishi agombee urais.

Baadaye walifuata wachungaji ambao nao walifunga safari hadi nyumbani kwa Lowassa Dodoma na kusema wameamua kumuomba Lowassa agombee urais kwa madai kuwa ana maono makubwa dhidi ya Tanzania.

Baadhi ya wachungaji hao walimwambia Lowassa wanaamini kuwa yeye ndio chaguo sahihi kwao na ndio maana wameamua kufunga safari na kumshawishi huku wakieleza kuwa kila mtu ametumia nauli yake kufika Dodoma.

Kwa upande wake Lowassa, akizungumza na wachungaji hao waliofika nyumbani kwake, alisema anafarijika kuona makundi mbalimbali yakifika nyumbani kwake kumshawishi agombee.

Alinukuliwa na vyombo vya habari juzi akisema pia kuwa hakuna kundi ambalo analituma au kulipa fedha kwa ajili ya harakati za kutaka kugombea urais.

Hata hivyo, tayari baadhi ya makadawa CCM ambao wamo kwenye orodha ya kutaka kugombea urais, wametoa malalamiko yao kuwa kinachofanywa na Lowassa si sahihi.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema kuwa kitendo chakuandaa watu kwa ajili ya kuanza kampeni si cha kiungwana na kwamba kila mgombea anaweza kufanya hivyo, lakini wanaheshimu kanuni na Katiba za chama chao.

January amenukuliwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii akieleza wazi kuwa anaweza kutengeneza makundi kwa ajili ya kuonesha Watanzania kuwa anahitajika, lakini akasema hizo ni propaganda ambazo hazina tija kwa Taifa.

"Kama mgombea anakubalika kwa Watanzania kwanini atumie fedha nyingi kutafuta makundi ili aonekane anakubalika? Alihoji January katika ujumbe wake aliousambaza katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

LOWASSA AMPUUZA JANUARY

Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa, amesema watu wanaosema anawalipa watu wanaomshawishi awanie nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, ni upuuzi na uongo na kwamba hawezi kuwajibu kwani kufanya hivyo ni kuwapa sifa wasizostahili.

Lowassa aliyasema hayo nyumbani kwake jana mjini hapa, kufuatia baadhi ya vyombo vya habari, kumnukuu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais, akisema baadhi ya watu wanatumia vibaya umaskini wa Watanzania kwa kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.

Akizungumza mbele ya wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya kuwagharimia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi na kwamba wengi wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.

"Najiunga na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis Mgeja) kusema leo (jana) kuna mtu kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo hovyo kidogo, ambaye nikimjibu nitakuwa nampa heshima kwa hiyo nampuuza, sina uwezo wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu," alisema.

Alisema makundi yanayomshawishi awanie nafasi hiyo wanafanya hivyo kwa utashi wao, mapenzi yao kwa taifa na Mungu wao na kwamba 'lugha nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo.

'Awali, Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa Lowassa wanalipwa, ni walioishiwa hoja, wamefilisika na sasa wanatapatapa na kwamba kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.

"Nimekaa muda mrefu kwenye siasa, wengine bado wanahitaji wapate muda wa kujifunza na katikasiasa hatuwajui ni wapi walipotokea,wakipata muda mzuri wajifunze, wawe na adabu, watulie kuliko kuzusha maneno ambayo huna uhakika nayo, ambayo ni dhambi kubwa sana," alisema Mgeja. Alisema wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alitoa rai kuomba wananchi na wana CCM wakiona mtu anayefaa kuwa kiongozi wamshawishi, hivyo wanachokifanya siyo makosa.

"Tusihukumiane kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika nyumbani kumshawishi, ndivyo tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo tumshawishi, mpeni nguvu, mjengeni suala hili ni kubwa linahitaji dua na maombi.
Kama viongozi tumeona kwa maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea kijiti na kutupeleka mbele,niungane na Watanzania wenzangu na mimi kusema tunaona kwamba hakuna mwingine zaidi ila Mheshimiwa Lowasa," alisema Mgeja.

Aidha, Lowassa alizungumzia ujio wa wachungaji hao nyumbani kwakejana, akieleza kuwa umeandika historia katika maisha yake kwani hakutegemea kupokea kundi kubwakama hilo la watumishi wa Mungu.

Alisema watu ambao wamemfuata kumshawishi amewaambia kuwa nafasi ya urais ni kubwa na inahitaji maombi.

"Ninachoomba wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige magoti mpaka yachubuke, hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu," alisema.

Mapema, Mratibu wa ujio wa Wachungaji hao, Mchungaji Benedickto Kamzee, kutoka Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi huo bila kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.

"Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu," alisema.

Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT, TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.

Maeneo hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi, Bukombe, Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke, Kinondoni, Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.

Wengine wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same, Masasi, Kibondo, Kilombero, Rungwe, Mwibara, Kisarawe, Nachingwea na Kilolo.


WANAFUNZI, WAFANYABIASHARA WANENA

Wakati huo huo, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara mjini hapa waliokwenda kwa Lowassa juzi kumshawishi agombee, wamesema kwa Lowassa hakukuwa na ubwabwa wala soda na kwamba kauli ya Makamba inaonyesha kuwa Lowassani kiongozi anayefaa ndio maana watu wanampinga.

Rais wa Kitivo cha Imformative katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Goodluck Philip, alisema wanafunzi walikwenda kwa Lowassa kwa utashi binafsi na bila shinikizo na kwamba kauli ya kuhongwa imewadhalilisha.

Alisema kauli hizo zinalenga kuwatisha watu wakati msingi wa kufanya hivyo ni wa kidemokrasia.

Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Dodoma, Norbati Pangaselo, alisema wapinzani wa Lowassa wanatakiwa kujenga hoja badala ya kuzusha uongo kwa nia ya kumchafua.


WAZAZI WAJA JUU

Mbio za uchaguzi wa urais zimeanza kukichanganya CCM, kufuatia Jumuiya ya Wazazi kutoa tamko kali la kutaka kuwachukulia hatua wenyeviti na makatibu wa mikoa wa jumuiya hiyo na wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya waliokwenda nyumbani kwa Lowassa kumshawishi agombee urais mwakahuu na kumpatia Sh. 600,000 wakidai ni kwa niaba ya baraza hilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, alisema CCM ina maadili na taratibu zake kwa wanachama wanaotaka kugombea urais mwaka huu.

"Viongozi 20 wa jumuiya waliokwenda kwa mgombea mmoja(Lowassa), wakae kwenye vyombo vya habari wakanushe hawakwenda kwa niaba ya Jumuiya ya Wazazi ndani ya mwezi huu na kwamba kukanusha huko hakuzii kuwahoji kwenye kikao cha maadili" alisema Bulembo.

Alisema vikao vya maadili vya jumuiya hiyo vitakaa kuwajadili na wakibainika kufanya makosa wanaweza kuchukuliwa hatua ambao ni pamoja na kufungiwa uanachama miezi sita, 12 na 18 au kufukuzwa kabisa uanachama.

Kwa mujibu wa kanuni ya Jumuiya ya Wazazi toleo la Mwaka 2008 kifungu cha 83 Ibara ndogo ya 11, Baraza la Wazazi Taifa litakuwa na uwezo wa kumfukuza au kumsimamisha uongozi kiongozi yeyote ambaye uongozi wake huteuliwa na Umoja wa Wazazi.

Bulembo alisema viongozi watakaojadiliwa na ikibainika wamekiuka kanuni watakumbwa na adhabu hiyo ni wenyeviti wa wazazi mkoa wa Kilimanjaro, Simiyu, Mwanza, Mbeya , Morogoro, Shinyanga, Kusini Unguja na Mkoa wa Mara.
Wajumbe wa Baraza Kuu watakaojadiliwa ni kutoka mkoa wa Tanga, Mbeya, Dodoma, Ruvuma namkoa wa Njombe wakati Makatibu wa Jumuiya wanatoka mikoa ya Kusini Unguja, Morogoro na Shinyanga.

Alisema siyo kosa kwa kiongozi au mwanachama yeyote kuonyesha mapenzi kwa mtu yeyote anayetaka kugombea urais, lakini taasisi ya chama haiwezi kuwa na mgombea wake itakuwa imekosa sifa.

"CCM ina jumuiya tatu, Jumuiya ya Vijana, Wazazi na Wanawake, jumuiya mojawapo inaposema ina muunga mkono mgombea fulani haifai kubaki tena katika CCM kwa sababu kazi ya jumuiya hizi ni kufanya kazi za chama kutegemeana na maelekezo," alisema.

Alisema unapozungumzia taasisi ambayo ni Jumuiya ya Wazazi yenye wanachama zaidi ya 2,300,000 Tanzania nzima, hivyo anapotokea kiongozi mmoja anasema anazungumza kwa niaba ya wanachama hao ni hatari na anavunja maadili ya chama ambacho hakiruhusu taasisi kujihusisha na mgombea yeyote.

Bulembo alisema CCM itatoa mgombea wake baada ya mkutano mkuu kwa kazingatia vikao vya chama, hivyo wale wote waliokwenda kwa Lowassa watachukuliwa hatua kwa kuitumia jumuiya kwa matakwa yao .

"Lakini hawa wagombea urais napenda niwaase, kama wanataka kugombea ndani ya CCM wafuate taratibu za chama na kusoma vitabu vinavyoelezea miiko ya chama, lakini unakuta mgombea anakusanya watu Mbeya na maeneo mbalimbali jamani anataka nini?" alihoji.


CHANZO: NIPASHE

AKAMATWA NA VIUNGO VYA BINADAMU NA NYARA ZA SERIKALI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limemkamata na linamshikilia Kulwa Rajabu (35) Mkazi wa Mtaa wa Kashaulili Wilayaya Mpanda kwa tuhuma za kumkamata na viungo vinavyosadikiwa kuwa ni vya Binadamu na nyara za Serikali Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Kamishina msaidizi mwandamizi Dhahiri Kidavashari mtuhumiwa huyo alikamatwa na viungo hivyo na nyara za Serikali hapo majira ya saa tatu usiku nyumbani kwake katika Mtaa wa Kashaulili mjini hapa.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kufuatia taarifa ambazo zilikuwa zimelifikia jeshi la Polisi kutoka kwa Raia wema ambao walitowa taarifa kwa polisi kuwa mtuhumiwa ameifadhi viungo vya binadamu na nyara za Serikali ndani ya nyumba yakeg

Alifafanua baada ya taarifa hizo kulifikia jeshi la polisi walianza kufanya uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo zilizokuwa zikimkabili Kulwa Rajabu.

Kamanda Kidavashari alieleza ndipo hapo jana Polisi walipokwenda nyumbani kwa mshitakiwa na walipofika nyumbani kwake walimfanyia upekuzi huku wakiwa na viongozi wa Mtaa huo.

Alisema katika upekuzi huo Polisi walifanikiwa kumkamata mshitakiwa akiwa amehifadhi ndani ya nyumba yake mifupa mitatu ,mshipa mmoja wa chini ya kinena unaodhaniwa ni wa mtu mwanaume na meno mawili viungo hivyo vinadhaniwa ni vya Binadamu

Kidavashari alisema mbali ya mtuhumiwa kukamatwa na viungo hivyo pia mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa amehifadhi ndani ya nyumba yake nyara za Serikali

Alizitaja nyara alizokamatwa nazo mtuhumiwa Kulwa Rajabu kuwa ni kipande cha ngozi ya Kalungu yeye na singa mbili za Tembo.

Kamanda Kidavashari alisema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa Mahakamani ili akajibu mashitaka mawili ya kupatikana na viungo vinavyosadikiwa kuwa ni vya Binadamu na kupatikana na nyara za Serikali.

MWANAFUNZI AUAWA NA BABA YAKE BAADA YA KIPIGO

Mwanafunzi aliyefahamika kwa jina la Alson Kibona (17) mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Nsemlwa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi ameuwawa baada ya kupigwa kichwani na mpini wa koleo na sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi kwa kosa la kutokwenda shuleni.

Kaimu kamanda wa jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi Rahid Mohamed alimtaja mzazi anayetuhumiwa kumuuwa mwanae kwa kumpiga na mpini wa koleo kuwa ni John Kibona(35) mkazi wa mtaa wa Nsemulwa Mjini hapa Alisema tukio hilo la mauwaji ya mwanafunzi lilitokea hapo juzi majira ya saa tisa usiku nyumbani kwa mtuhumiwa katika mtaa wa Nsemulwa

Kwa mujibu wa Rashid Mohamed Siku hiyo ya tukio marehemu Alson alikuwa amelala chumbani mwake ndipo baba yake alipomwamsha na kuanza kumuoji kwanini amekuwa na tabia ya utoro wa mara kwa mara wa kutokwenda shuleni.

Mohamed alisema ndipo mtuhumiwa alianza kumpiga marehemu kwa kutumia mpini wa koleo kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake huku akiwa akimkanya kwa maneno kuwa aache tabia ya utoro wa shuleni.

Alisema marehemu baada ya kuona kipigo kimemzidia alianza kupiga mayowe ya kuomba msaada hata hivyo mtuhumiwa hakujali aliendelea kwa kumpa kichapo mwanae huyo.

Siku iliyofuata marehemu aliamka huku akiwa na maumivu makali katika sehemu mbalimbali za mwili wake hari ambayo ilimlazimu ashindwe hata kwenda shule na mtuhumiwa hakujali wala kumpeleka kwenye matibabu Kaimu Kamanda Rashid Mohamed alieleza siku hiyo ilipotimia majira ya saa sita marehemu alikwenda kisimani kuteka maji ya kuoga ambapo alipoinama ili achote maji damu zilianza kumtoka mdomoni na puani na kisha kuanguka chini pembezoni mwa kisima hicho.

Alisema majirani waliokuwa karibu na eneo hilo walimchukua marehemu na kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa ajiri ya kupatiwa matibabu.

Alifafanua wakati akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali hiyo alifariki Dunia kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata kutokana na kipigo alichokuwa amekuwa amekipata Baada ya mtuhumiwa kupata taarifa kuwa mwanae amepelekwa Hospitali na wakati akiwa anapatiwa matibabu amefariki Dunia aliamua kutoweka na kukimbilia sehemu kusiko julikana

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu na uongozi wa mtaa linamsaka mtuhumiwa ili kumkamata na awezekujibu tuhuma inayomkabili.

Aidha kaimu kamanda wa jeshi la Polisi wa Mkoa wa Katavi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kutumia nguvu kwa kuwapiga watoto wao na badala yake wawaelimishe na kuwaeleza umuhimu wa elimu ili kuepuka matukio mbaya ya nanma hii ndani ya jamii.

WATANO WAFARIKI KUTOKANA NA MVUA DAR

HALI ni tete katika jiji la Dar es Salaam, kutokana na mvua ya masika iliyonyeshwa kwa siku tatu na kusababisha vifo vya watu watano, huku nyumba nyingi zikiwa zimezingirwa na maji.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Buguruni kwa Mnyamani na eneo la Jangwani katika Manispaa ya Ilala, ambako nyumba nyingi na barabara zimeathirika.

Sehemu nyingine za jiji zimezingirwa na maji kutokana na kuziba kwa mitaro na mifereji, ikiwa ni athari ya utupaji taka ovyo na pia miundombinu duni.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), mvua kubwa zaidi zinatarajia kuendelea kunyesha mpaka Jumatano.

Kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, Mkuu wa Mko wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki (pichani) jana aliongoza kikosicha uokoaji katika eneo la Buguruni kwa Mnyamani, ambako nyumba 250 zilizingirwa na maji, jambo ambalo vikosi vya uokoaji vililazimika kufanya kazi ya kuwanasua watu waliokuwa wamekwama katika nyumba zao.

Uokoaji huo ambao mpaka jana jioni ulikuwa ukiendelea, ulisaidiwa na wafanyakazi wa kampuni ya China Railway Jianchang Engineering(CRJE), inayojenga Daraja la Kigamboni, kwa kutoa vifaa na kushiriki katika uokoaji wa watu hao.

Sadiki alisema mpaka jana mvua hizo zimesababisha vifo vya watu watano, akiwemo mtu mmoja aliyesombwa na maji, mwingine aliyeangukiwa na ukuta na watatu ambao wamenaswa na umeme baada ya nguzo ya umeme kuanguka Mbagala Mzambarauni katika Manispaa ya Temeke.

"Wananchi wanatakiwa kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo katika maeneo ya mitaro, kwani ndiyo yaliyochangia maji kuleta madhara, na walio mabondeni bado nawasihi kuondoka maeneo hayo," alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema mtu mmoja ambaye hajatambuliwa mwenye umri kati ya miaka 45 hadi 50, anasadikiwa kusombwa na maji katika mto Goba.

Aidha, alisema katika eneo la Mwananyamala, mlemavu wa viungo Edward Warioba (22) aliangukiwa na ukuta usiku wa kuamkia jana akiwa amelala katika nyumba iliyokuwa imeingia maji na kulowanisha kuta zake.

Wambura alitaka wananchi kuchukua tahadhari kwa watoto waona wahakikishe wanakwenda na kurudi kutoka shule wakiwa salama.

Eneo la Jangwani, kati ya Magomeni na Faya (Kariakoo), pia nyumba kadhaa zilizingirwa na maji huku baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wakihamia barabarani ili kujinusuru.

Lakini eneo la Jangwani, karibu na klabu ya Yanga, walionesha kutokuwa na wasiwasi na mvua zinazoendelea kwa madai kuwa hazijafikia kiwango cha kuwa na athari kwao.

"Kipimo chetu ni hiki hapa, (wanaonesha alama) maji yakifika kimo hiki tunajua wakati wa kuhama nyumba zetu umewadia lakini kwa sasa maji haya hayana madhara yoyote," alisema mkazi wa eneo hilo, Huseni Juma.

Akizungumza jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi alisema mvua kubwa zaidi ya milimita 50 ambazo zimenyesha sasa, zinatarajia kuendelea kunyesha ndani ya saa 24 zijazo huku mvua hizo kuendelea kunyesha hadi Machi 25, mwaka huu.

"Utabiri unaonesha kuwa mvua kubwa za zaidi ya milimita 50 zitaendelea kunyesha siku tatu zijazo. Hivyo ni vema wananchi wakaendelea kuangalia utabiri unaotolewa na mamlaka kila siku ili kujiepusha na madhara," alisema.

Awali, TMA ilitoa mwelekeo wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi, Aprili na Mei na kuwa kipindi hicho mvua zilitarajiwa kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.

RAIS KIKWETE NA UHURU WAMALIZA TOFAUTI

RAIS Jakaya Kikwete na Uhuru Kenyatta wa Kenya wameingilia kati mgogoro uliopo baina ya mataifa hayo mawili kuhusu masuala ya usafirishaji na utalii.

Makubaliano yaliyofanywa na marais hao ni pamoja na Kenya kuruhusu magari ya Tanzania, yanayofanya safari za kupeleka wageni na watalii, maarufu kama 'Shuttle' kuingia kupeleka na kuchukua watalii katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKNIA).

Makubaliano mengine ni kwa Tanzania kupitia Mamlaka ya Usafiriwa Anga (TCAA), kurudisha safari za ndege ya Shirika la Kenya (KQ) kutoka siku 14 za sasa hadi 42 za awali.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kikao kilichowakutanisha marais hao wawili jijini Windhoek, Namibia.

"Kuanzia saa 10:00 leo hii (jana) magari yote ya Tanzania yana ruksa ya kuingia Kenya kuchukua na kupeleka watalii katika uwanja wa Jomo Kenyatta na ndege za Kenya kuanzia leo zitaruhusiwa kurusha ndege zake kama kawaida kwa siku 42 badala ya 14," alisema Waziri Membe.

Aidha, Membe alisema katika kikao hicho, walizungumzia mambo mawili muhimu ambayo ni sekta ya usafirishaji na utalii, ambapo pia walikubaliana ndani ya wiki nne, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo waitishe mkutano utakaowajumuisha Mawaziri wa Usafirishaji, Utalii na Maofisa kutoka katika ofisi za Marais.

Alisema kabla ya kutoa taarifa hiyo, waliwasiliana na Mawaziri wa Uchukuzi na Utalii ambapo pia taarifa hiyo imetangazwa kwa wakati mmoja hapa nchini na Kenya.

Waziri Membe alisema mkutano wakwanza utafanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam, ambapo alisema katika mkutano huo ndipo kiini cha mgogoro huo kitabainika.

"Tanzania na Kenya ni ndugu, ni majirani tusikubali kuchonganishwa wala kuonesha tofauti zetu waziwazi, kama zipo ni vizuri tukaitana na kuzimaliza kimya kimya," alisema.

Rais Kikwete na Kenyatta wamekutana jijini Windhoek ambako walikwenda kuhudhuria sherehe za miaka 25 ya uhuru wa nchi hiyo na kuapishwa kwa rais wa tatu wa nchi hiyo, Dk Hage Geingob.

Hatua ya mgogoro huo inatokana na serikali ya Kenya kupiga marufuku magari ya Tanzania kuingia nchini humo, kupeleka na kuchukua watalii.

Hata hivyo hivi karibuni Mamlaka yaUsafiri wa Anga (TCAA) ilipunguza idadi ya safari za ndege za shirika la nchi hiyo kutoka 42 kwa wiki hadi 14.

Mgogoro huo umekuwa na madhara kiuchumi na maisha ya wananchi wa nchi hizi mbili.

CCM NA CHADEMA WAKOSOA TAARIFA YA CAG

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema wamekosoa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupatahati zenye mashaka na kueleza kuwa hesabu za vyama vyao zipo sahihi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye na Mkurugenzi wa Fedha wa Chadema, Anthony Komu walidai taarifa ya CAG ndiyo yenye upungufu.

Nape katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari yaliyorushwa moja kwa moja na kituo cha Radio 5 Arusha alisema, kuna tatizo la kutokubaliana kutokana na ukaguzi wa CAG.

Alisema mahesabu ya CCM yanayotokana na fedha za ruzuku kutoka serikalini yapo sahihi lakini wana mgogoro na CAG ambaye anataka mahesabu juu ya mali zote za CCM.

"CCM ina miradi mingi kwa mfano hapa Arusha tuna uwanja wa Sheikh Amri Abeid awali uwanjahuu, ulikuwa unasimamiwa na Mkoa wa Arusha pekee, sasa mkoa umegawanywa siyo rahisi kuwa na mahesabu yote," alisema.

Alisema kwa maagizo ya CAG, kuandaa hesabu na taarifa za mali zote za CCM, inahitaji kutumika kwa zaidi ya Sh1 bilioni jambo ambalo ni gumu.

"Sisi tunadhani CAG anapaswa kukagua mahesabu ya fedha za ruzuku tunazopewa na Serikali lakini siyo mahesabu ya mali zote za CCM," alisema.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, ameainisha vigezo saba tofauti vilivyosababisha hesabu za CCM kupata hati yenye mashaka na kueleza kuwa CCM imekosa uhalali wa kisheria kumiliki baadhi ya mali ilizonazo.

Ukaguzi huo wa CAG umefanyika kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992ya Vyama vya Siasa, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria namba 7 ya mwaka 2009, inayompa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya siasa.

Ilibainisha vigezo vingine vya hati yenye mashaka kuwa ni CCM kutowasilisha taarifa ya mapato yake ya fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali zilizofikia Sh1,526,536,802, huku CAG pia akishindwa kupata nyaraka za kuthibitisha matumizi na malipo yaliyofanywa na chama hicho yanayofikia Sh6,045,438,052.

Kwa upande wa Chadema, Komu alisema ripoti ya CAG inaupungufu kwani, inataka chama hicho kuandaa taarifa za mahesabu na uthamini wa mali hadi mikoani.

"Mapungufu (upungufu) ambayo alianisha ya kutofanya uthaminiwa mali zetu kutokuwa na mahesabu ya benki katika ngazi mbalimbali na vitabu vya risiti kwa baadhi ya maeneo ni mambo ambayo huwezi kuyakamilisha kutokana na mfumo wa vyama vyetu," alisema.

Alikiri kuwa chama kuwa na akaunti nyingi kwa madai kuwa kila mkoa, wilaya na jimbo wana akauti yao.

Ripoti ya CAG ilibaini kwamba Chadema ina zaidi ya akaunti 200 katika benki mbalimbali nchini lakini fedha zilizotajwa kuwapo katika taarifa zake kwa mwaka ulioishia Juni 2013 ni Sh224,824.750.56 kati ya hizo Sh221,060,446.41 zikiwa ni salio katika akaunti zake sita na kuacha salio la Sh3,764,304.15 kwa akaunti zaidi ya 194 zilizosalia.

Magari 10 yalinunuliwa kwa Sh 559,031,330 bila kuidhinishwa Sh 27,500,000 zilitumika kukodi jenereta bila kuwa na nyaraka.

Chanzo: Mwananchi

UHUSIANO TETE KENYA TANZANIA WAFUKUTA

Mgogoro unaofukuta kati ya Tanzania na Kenya umefikia hatua mbaya baada ya juzi usiku kikao cha makatibu wakuu wa Wizara za Maliasili na Utalii, Wizara za Afrika Mashariki za pande zote mbili kuvunjika.

Kikao hicho kilikuwa kikitafuta suluhu ya pande hizo mbili baada ya Serikali ya Kenya kuzuia magari ya Tanzania kuchukua watalii Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta(JKIA).

Kutokana na kuvunjika kwa kikao hicho, jana Waziri wa Utalii wa Kenya, Phyllis Kandie alisusia kikao cha kutafuta suluhu na waziri mwenzake wa Tanzania, Lazaro Nyalandu.

Akizungumzia kuvunjika sakata hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Adelhelm Meru alisema kikao kilivunjika baada ya wajumbe wa Kenya kutaka kufumuliwa Mkataba wa Ushirikiano wa Utalii uliosainiwa mwaka 1985.

Alisema wajumbe wa Kenya wakiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii, Dk Ibrahim Mohamed na wa Wizara ya Afrika ya Mashariki, John Konchellah walisema suala la kuzuiwa magari ni dogo, lakini wanataka kufumuliwa kwa mkataba wote.

"Sisi Watanzania tulipinga kwa kuwa ajenda yetu ilikuwa ni moja, kwa nini magari ya Tanzania yamezuiwa kuingia JKIA na kama kuna matatizo basi ielezwe," alisema.

Alisema kutokana na mvutano huo, walishindwa kuelewana na hivyo kikao kuvunjika bila kufikia maridhiano.

Kuvunjia kwa kikao hicho kumekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) kupunguza safari za ndege kutoka Kenya kuingia Tanzania kutoka 42 hadi 14 kwa wiki.

Suala hilo limeibua hisia tofauti nchini na baadhi ya wadau wa uchumi wamesema Serikali haikutafakari kabla ya kufikia hatua hiyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema hakuna nchi inayonufaika na uamuzi huo, hivyo aliishauri Serikali kukaa meza moja na Kenya na kufikia suluhisho mapema.

Mchumi kutoka Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Abel Maganga alisema uamuzi huo utakuwa na changamoto kwa kipindi kifupi kwa watalii ambao tayari walishalipia tiketi za safari kuja nchini.

Pia, alisema endapo hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu, itakuwa na athari kwa Tanzania kwa kuwa sekta ya utalii ndiyo inayoliingizia taifa fedha nyingi za kigeni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana kuhusu waziri mwenzake kutokuhudhuria mkutano wa majadiliano, Waziri Nyalandu alisema walikubaliana kikao hicho kiwe na ajenda moja ya sababu za Serikali ya Kenya, kuzuia magari ya Tanzania.

Alisema kuzuia magari ya Tanzania kuingia JKIA ni kukiuka mkataba huo wa 1985 ambao unatoa ruhusa magari ya kila nchi kuingia nchi nyingine kuleta watalii.

"Tulikubaliana magari ya Kenya, yanaweza kuingia Tanzania, katika miji ya Arusha, Moshi, Tanga na Musoma kuleta watalii, hivyo hivyo magari ya Tanzania kuingia Kenya lakini tunashangaa wenzetu wameweka zuio la magari yetu na yao yanaingia nchini," alisema.

Nyalandu alisema baada ya kushindikana vikao hivyo, msimamo wa Tanzania ni kuwataka mawakala wa kampuni za utalii na watalii kuwa wavumilivu wakati mgogoro huo unafanyiwa kazi.

AZAM WANUNUA LIGU YA KENYA

Baada ya kuzinunua Lligi Kuu za Tanzania Bara (VPL) na Uganda (UPL), Kampuni ya Azam Media, Jana Ijumaa imenunua rasmi haki za matangazo ya televisheni ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKLPremier League).

Imetangazwa rasmi Jana kuwa Azam TV inayorusha matangazo kwa satelaiti kutoka Tanzania, itakuwa inarusha moja kwa moja 'live' matangazo ya mechiza ligi ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) baada ya pande zote mbili kusaini makubaliano hayo kwenye Hoteli ya Intercontinental jijini Nairobi, Kenya jana Ijumaa 20 Machi.

Udhamini huo wa miaka mitatu utazifanya mechi za FKF PL zionekana moja kwa moja kwa dau la dola za Marekani mil 2.25 (Kshs mil 2o5.75) ikiwa ni sawa na US$ 750,000 kwa kila msimu.

Imethibitisha na Mwenyekiti wa FKF, Sam Nyamweya, kwamba kila timu inayoshiriki ligi hiyo itapata fungu la Kshs mil 1 kila mwezi huku akitamba kuwa misaada mingi ya kiuchumi inakuja kutoka kwa wadhamini wengine.

Hata hivyo, imeriptiwa na mitandao ya michezo ya Kenya kwamba suala la mgawo wa fedha za klabu bado halijakaa sawa kutokana na kutokamilika kwa mipango ya bajeti ya udhamini.

"Sitaki niseme sana kuhusu ugawo wa klabu, tutajadili kama shirikisho pamoja na wadau na kuangalia bajeti tuliyonayo kabla ya kuliweka wazi suala hilo kwa umma," amesema.

Alipoulizwa kuhusu ruhusa kwa TV za Kenya kujiunga na Azam TV kuonyesha matangazo ya ligi hiyo, Nyamweya alisema suala hilo pia bado linajadiliwa.

MASHEKHE WAMCHANGIA LOWASSA LAKI 7 ACHUKUE FOMU YA KUGOMBEA URAIS

Masheikh zaidi ya 50 kutoka Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, leo wamemkabidhi kiasi cha shilingi 700,000/-za kuongezea kuchukua fomu ya kuwania urais 2015.

Mashekhe hao wakiongozwa na Yusuf Surulu na Alli Mtumwa wamemkabidhi fedha hizo nyumbani kwake mjini Dodoma na kushuhudiwa na Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof Juma Kapuya.

Wamesema kuwa wameona mtu pekee anayefaa kushika wadhifa huo ni yeye hivyo wanamsihi atangaze nia na achukue fomu ya kugombea na wapo nyuma yake katika dua.

Lowassa amewaambia viongozi hao wa dini kuwa makundi mbalimbali ya jamii yamekuwa yakimuomba kugombea Urais lakini wao wamemfanya ashawishike sasa kufanya hivyo wakati ukifika.

TCRA: KUFUNGIA MITANDAO YA KIJAMII,RADIO, TV ZINAZOKIUKA MAADILI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema iko mbioni kuifungia mitandao ya kijamii, redio na televisheni inayokiuka maadili ya Mtanzania.

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Innocent Mungy, alisema kuwa mitandao hiyo ni pamoja na facebook, whatsapp na instagram.

Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo kutokana na kuwapo kwa watumiaji wengi wa mitandao hiyo katika kuelekea Siku ya Mawasiliano duniani inayofanyika Machi 15, kila mwaka.

Mungy alisema kuwa Mamlaka hiyo inafanya utafiti ili kubaini mitandao inayoongoza kwa kulalamikiwa na wateja ili hatua zichukuliwe.

"Tangu TCRA iwezeshe kuwa na wingi wa simu na kuwezesha kuwepo kwa mitandao mingi ya kijamii changamoto zimeongezeka, maadili yameporomoka tofauti na miaka ya nyuma wakati kuna redio moja tu maadili yalizingazitiwa, kwasasa utasikia lugha za matusi kwenye radio ikiwa ni pamoja na vipindi visivyofuata maadili na kanuni za habari, tuna mpango wakuifungia mitandao hiyo na vyombo vya habari visivyokidhi mahitaji," alisema.

Alisema kuwa Mamlaka hiyo lengo lake ni kuwezesha Watanzania kwenda na wakati na kuelewa mambo mengi kwa wakati mmoja ikiwa ni pamoja na kupata habari ndani na nje ya nchi na kuongeza ajira kwa Watanzania kama ilivyo kwenye makampuni ya simu.

Aliwataka wamiliki wa mitandao kufuata maadili ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, wazazi, kuwafundisha wananchi na waumini wao kuwa na maadili ili kuondoa upotofu huo ambao unaweza kugeuza kizazi kisichofuata maadili na wengine kukosa ajira kutokana na kutumia mitandao vibaya.

Aidha, alifafanua kuwa utumiaji wa simu kwa Tanzania ulianza mwaka 1962 zikiwa ni simu zenye uzito wa kilo tatu na mwaka 1990 ndipo zilipoingia simu za ujumbe mfupi nazo hazikuwa na matatizo ya kuporomoka kwa maadili.

Alisema utafiti uliofanyika kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii unaonyesha watumiaji wanaingia bila kusoma masharti yakuingia ambapo mitandao hiyo inatoa onyo la kutokurusha picha chafu au za mtoto chini ya miaka mitano.

Alisema watumiaji wa simu wanafikia milioni 32,000,000 wakati vyombo vya utangazaji vimeongezeka na kufikia 123 ikiwa ni pamoja na televiasheni 28 na redio 95.

Changamoto ni kwa watumiaji kutumia mitandao kwa njia salama ikiwa ni pamoja na kujali afya za watumiaji na kuondoa uhalifu.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

LIPUMBA AKUBALI TAMKO LA MAASKOFU

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba ameunga mkono tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kupinga Katiba Inayopendekezwa, akisema hoja zao ni za msingi kwa kuwa kuna mambo mengi yanayopingwa na wananchi.

Kauli ya Profesa Lipumba ni mwendelezo wa kauli tofauti zilizotolewa na watu mbalimbali kuhusu tamko la jukwaa hilo, wakiwamo wasomi, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasiasa kuhusu hatima ya Kura ya Maoni na muswada wa Makahama ya Kadhi.
Alhamisi iliyopita, jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) liliwataka waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, kushiriki kikamilifu katika elimu ya Kura ya Maoni, na kisha kuipigia kura ya “hapana” Katiba Inayopendekezwa.
Pia, tamko hilo lililotiwa saini na maaskofu Dk Alex Malasusa wa (CCT), Tracisius Ngalalekumtwa (TEC) na Daniel Awet wa CPCT, lilishauri mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuihusisha serikali wala waumini wa dini nyingine.
Jana gazeti hili lilimnukuu makamu mwenyekiti wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi akisema tayari tamko hilo limeshasambazwa katika majimbo yote ya kanisa katoliki nchini.
Kauli ya Lipumba
Akizungumzia tamko hilo, Profesa Lipumba alisema ni sahihi kuipinga Katiba hiyo kwa sababu wananchi walilalamikia mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya baada ya kubaini kuwa mambo mengi waliyoyapendekeza yaliondolewa wakati wa Bunge Maalumu la Katiba.
“Wananchi walitaka kuwepo na ukomo wa wabunge wao, viongozi wasifungue akaunti nje ya nchi na mambo mengine yote hayamo kwenye Katiba Inayopendekezwa. Hoja yao (maaskofu) ni ya msingi,” alisema Profesa Lipumba aliyeongoza wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya Bunge la Katiba na kususia mchakato huo moja kwa moja.
Alisema Serikali imeonyesha kutokuwa na uaminifu kwa wananchi ndio maana haikujali hisia zao, badala yake iliamua kuendelea na mchakato huo licha ya baadhi ya wajumbe kuususia.
Profesa Lipumba, ambaye ni mtaalamu wa uchumi, aliongeza kuwa wananchi walitaka kuwepo na utaratibu maalumu kuhusu viongozi wao kupewa zawadi wawapo madarakani, lakini Katiba Inayopendekezwa ililitupa nje suala hilo.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi, Profesa Lipumba alisema pia Serikali isitishe uamuzi wake wa kupeleka Muswada ya Mahakama ya Kadhi katika Bunge lijalo kwa kuwa bado yapo mambo mengi yanayotakiwa kuwekwa sawa.

Profesa Lipumba alisema pamoja na mahakama hiyo kutokuwa ngeni hapa nchini kwa kuwa ilikuwapo Tanzania Bara wakati wa ukoloni na Zanzibar, bado inaendelea kufanya kazi bila tatizo, mfumo unaotaka kutumiwa na Serikali kuianzisha hivi sasa unapingwa na baadhi ya Waislamu na Wakristo hivyo kusababisha mgawanyiko.
Alisema hali hiyo imefikia hapo kutokana na CCM kuliingiza suala hilo kwenye ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005, hivyo njia bora ya kuondoa sintofahamu iliyopo ni kwa kutumia muda mrefu zaidi katika kutafuta muafaka.
“Ni bora tungetumia muda mrefu zaidi kutafuta muafaka, Serikali isiendelee na muswada huo,” alisema Profesa Lipumba.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, likiwamo suala la Mahakama ya Kadhi, utawasilishwa katika bunge lijalo ukiwa na maudhui ya kuangalia namna ya kuendesha masuala ya imani ya dini ya Kiislamu.
Nyambabe aunga mkono
Katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema anaunga mkono uamuzi uliofikiwa na maaskofu hao kwa kuwa haiwezekani nchi ikapiga Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa wakati wananchi wamegawanyika.
“Msimamo wa maaskofu ni kama wa Ukawa. Bila kuchukua hatua mmomonyoko wa maadili hautaisha,” alisema Nyambabe.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Nyambabe alisema: “Hakuna mtu anayepinga kuwepo kwa mahakama hiyo, lakini isiwe chini ya serikali moja kwa moja, iwe huru.”
Kauli za wachungaji
Baadhi ya wachungaji waliunga mkono uamuzi wa Jukwaa la Kikristo kwa maelezo kwamba jambo hilo limeamuliwa na viongozi wao wa juu, lazima litekelezwe.
“Kwa kuwa wameshaamua, naamini tutapata hiyo barua haraka tu, lakini mpaka sasa hatujasikia jambo lolote,” alisema Mchungaji Emmanuel Owoya wa Usharika wa Nkwatira, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Hai.
Naye, Mchungaji Jackson Mwaisabile wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God (PAG) mkoani Iringa, alisema bado hajauona waraka unaosambazwa na Jukwaa la Maaskofu na kwamba utakapowafikia watajua nini cha kufanya.

Mzee wa Kanisa la Nguvu ya Uponyaji wa Ukombozi (LHPM) la Dar es Salaam, Ayubu Luchenje alisema masuala la Katiba Inayopendekezwa na Mahakama ya Kadhi yanahitaji kuyafahamu vyema kabla mtu hajatoa uamuzi wake.
Luchenje alisema suala la Mahakama ya Kadhi linakiuka misingi ya Taifa kwa kuwa Katiba iliyopo inaitambua nchi isiyo na dini. Alisema kwa msingi huo jambo hilo linafanywa kisiasa kwa malengo ya kutaka kulifurahisha kundi fulani katika jamii.
“Waziri Mkuu Mizengo Pinda anachofanya ni kutaka kuwafurahisha watu fulani tu, jambo hilo haliwezekani ufanye kitu kisichokubaliwa na Katiba,” alisema Luchenje.


CHANZO: MWANANCHI

MART NOOJ ATAJA KIKOSI KITAKACHOIVAA MALAWI

Kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars ) Mart Nooj, ametangaza kikosi cha wachezaji 27 watakaoingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi utakaofanyika uwanja wa CCM Kirumba jijin Mwanza Machi 29, 2015.

Taifa Stars inayotarajia kucheza na The Flames mwishoni mwa mwezi huu, itaingia kambini machi 22 machi katika hotel ya Tansoma kujiandaa na mchezo huo kabla ya kuelekea jijini Mwanza machi 24 kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo.Wachezaji walioitwa kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo ni; Magolikipa, Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula na Mwadini Ali (Azam FC).

Walinzi ni Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris (Azam FC), Mwinyi Haji (KMKM), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani, Nadir Haroub, Oscar Joshua (Yanga), Abdi Banda na Hassan Isihaka (Simba SC).

Viungo ni Frank Domayo, Salum Abubakar, Amri Kiemba, Mcha Khamis (Azam FC), Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United).

Washambuliaji Mwinyi Kazimoto (Al Markhiry - Qatar), Saimon Msuva , Mrisho Ngasa (Yanga), Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta (Tp Mazembe - Congo DR), John Bocco (Azam FC), na Juma Luizio (Zesco United - Zambia)

Timu ya Taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili jijini Mwanza machi 27, 2015 ikiwa na kikosi kamili, wakiwemo wachezaji nane wanaocheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, Msumbuji, Congo DR na Zimbambwe.

Malawi inashika nafasi ya 91 katika viwango vipya vya FIFA Duniani vilivyotolewa mwezi huu, huku Tanzania ikipanda kwa nafasi saba na kushika nafasi ya 100.

VIONGOZI WATATU CHADEMA WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Viongozi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Diwani wa kataya Ubungo, Boniface Jacob, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili la kushambulia na kumteka mlinzi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilibrod Slaa.

Wengine ni Afisa Usalama wa Chadema, Hemed Sabula (48), mkazi wa Tandale kwa Tumbo na Afisa Utawala Chadema Benson Mramba (30), Mkazi wa Tabata Kisukuru.

Watuhumiwa wote walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, na upande wa mashtaka ukiongozwana wakili wa serikali Janet Kitale.

Akisoma shitaka la kwanza, Kitale alieleza kuwa Machi 7, mwaka huu kwa pamoja wakiwa kwenye ofisi ya Chadema Makao Makuu walimshambulia Khalid Kagenzi katika maeneo mbalimbali ya mwiliwake.Kitale alidai katika shitaka la pili ambalo lilitokea Machi 7, wakiwa katika eneo hilo kwa pamoja walimteka Kagenzi na kumpeleka kwenye hotel ya River View iliyopo Sinza na kukusudia kumtisha na kumuweka mafichoni.

Watuhumiwa hao walikana mashtaka hayo na kupewa masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa na wadhamini wawilina kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10. Viongozi hao walirudishwa rumande na kesi hiyo itatajwa Machi 26, mwaka huu na upelelezi haujakamilika.

Wakati huo huo, Kamishina wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuwa jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu malalamiko ya Dk. Slaa ambayo yaliwafikia Machi 8, mwaka huu.

Alisema tuhuma hizo ziliwasilishwa na wakili wa Chadema, John Mallya, ambapo walipokea maelezo yake pamoja na mtuhumiwa Kagenzi (48)ambaye ni mlinzi wa Dk. Slaa.

Alisema kuwa wakili Mallya alidai kuwa uongozi wa Chadema pamoja na kamati ya ulinzi na usalama wa chama hicho ulichukua hatua mbalimbali za kujiridhisha kwamba Kagenzi ana tuhuma za kuhatarisha maisha ya Dk. Slaa kwa kutumia mbinu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kumwekea sumu.

Alisema ndiyo maana alitumwa kumpeleka kituo cha polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Kamanda Kova alisema polisi ilipomhoji mlinzi huyo alidai kuwa ana majeraha mwilini yaliyotokana na mateso aliyofanyiwa akiwa chini ya ulinzi wamaafisa wa usalama wa Chadema ambao walikaa naye na kumhoji kuanzia saa 5 asubuhi ya Machi 7, saa 11 jioni ya Machi 8, mwaka huu akiwa chini ya ulinzi mkali.

Alisema katika suala hilo kuna mashauri mawili ambayo yanachunguzwa likiwamo la awali la DK. Slaa na la pili dhidi ya watuhumiwa wanaodaiwa kumtesa kwa kumshambulia Kagenzi na kumsababishia majeraha mwilini.Juzi Dk. Slaa alihojiwa kwa zaidi ya saa sita na jeshi la polisi kuhusiana na malalamiko aliyoyatoa mlinzi huyo ya kupanga mikakati ya kutakakumuua.


CHANZO: NIPASHE

WATANZANIA WAHUSISHWA NA MAUAJI YA ALBINO MALAWI

Mauaji ya watu wenye ulemavuwa ngozi (Albino) yameendelea kuharibu taswira ya ya nchi na jumuiya ya kimataifa baada ya taarifa kudai kwamba wahalifu wa Tanzania wanahusishwa na unyama huo nchini Malawi.

Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa wiki iliyopita kwenye Nyasa Times, gazeti la Malawi likiwa na kichwa cha habari Albino "wanawindwa kama wanyama" kwa viungo vya mwili nchini Malawi, mwanaharakati alikaririwa kwenye habari hiyo akisema, baada ya Tanzania kuanza jitihada za kupambana na vitendo hivyo, wahalifu hao wamehamia Malawi sasa.

Shirika la Watu wenye Ulemavu wa Ngozi nchini Malawi (APAM) lilikaririwa katika habari hiyo ya gazeti hilowakisema, watu wanaojihusishana uuzaji wa viungo vya albino wamepata soko Malawi baada ya kuona ugumu wa biashara hiyo nchini Tanzania.

"Wale ambao wako katika biashara ya kuuza viungo vya albino… wameanzisha soko nchini Malawi, kwa sababu imekuwa vigumu kufanya biashara nchini Tanzania," Boniface Massah aliliambia gazeti hilo.

"Tunawinda kama wanyama, huna uhakika kuwa unaweza kuwaamini marafiki au ndugu,"alisema rais wa APAM Massah, ambaye anapiga kampeni za haki za albino Malawi.

Kwa mujibu wa takwimu nchini Malawi, kulikuwa na mauaji ya albino wawili mwaka 2014 na moja 2013.
Gazeti hilo limeeleza kuwa Malawi na watu wapatao 10,000 wenye ulemavu wa ngozi.

KOCHA SYLVESTER MARSH AFARIKI DUNIA

Aliyekuwa kocha Msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Sylvester Marsh amefariki dunia Alfajiri ya leo katika hospitali ya Muhimbili alipokuwa amelazwa.

Taarifa zinasema Marsh alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya maradhi ya saratani ya koo yanayomsumbua na ghafla hali yake ilibadilika juzi hadi kufariki dunia.

Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj Abdallah Athumani Seif 'King Kibadeni' kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa, akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Jan Poulsen na Kim Poulsen.

Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kuingia madarakani Oktoba mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Stars na Marsh akaondoka pamoja na Kim Poulsen.

Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.

Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.

Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.

Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

MTOTO ANAEFANANA NA ALBINO ATEKWA NA KUUAWA

Loveness Maliaki (11), mtoto wa darasa la nne shule ya msingi Osunyai Sombetini, anayedaiwa kufanana na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), ametekwana kuuawa na kunyofolewa viungo vyake vya siri, pua na macho kutobolewa.

Mama wa marehemu, Mary Kilongo (37), alisema walimpata mtoto huyo akiwa amefichwa chini ya uvungu, kwenye nyumba mbovu ya udongo inayomilikiwa na Henry Ally (58) ambaye wakati wa tukio hilo inadaiwa hakuwapo.

"Wakati wakitoka shule jioni akiwa ameongozana na wenzake huyo kijana (anamtaja mtuhumiwa) Tunamfahamu, aliwafuata watoto akiwa anaendesha baiskeli yake akawaambia kuwa kuna hela yangu imetumwa kwa M-Pesa kwenye simu yake,"

alieleza na kuongeza: "Akawataka wamfuate wakaichukue, alimkatalia basi akaamua kumchukua marehemu kwa nguvu na kumpandisha kwenye baiskeli yake na kuondoka naye, hivyo wale waliobaki wakaja kunieleza."

Mjomba wa marehemu, Mohamedi Kilongo, alisema alipouangalia mwili wa marehemu ulionekana kama alinyogwa shingo, kwani alikuwa na alama

Chanzo:East Africa Radio!

ALBINO MWINGINE AKATWA KIGANJA

LICHA ya Serikali, jamii na jumuiya ya kimataifa kukemea ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), bado kuna wanaoendelea kung'ang'ania mila potofu za kuamini kwamba bila ya ushirikina unaohusishwa na matumizi ya viungo vya albino, hawawezi kufanikiwa kimaisha, iwe katika kisiasa au kibiashara.
Hayo yanathibitishwa na kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya ukatili dhidi ya albino, ambapo usiku wa kuamkia jana, watu wasiojulikana walimshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kishakutokomea nacho kusikojulikana.

Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban.  ukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda.

Alisema tukio hilo ni la saa 8 usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo. Akielezea zaidi, Kamanda Mwaruanda alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada yakukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.

"Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya … "Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana," alibainisha.

Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.

Kwa mujibu wa Mwaruanda, mtoto huyo amelazwa katika katika Kituo cha Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja na mama yake mzazi.

"Watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo hicho cha kiganja cha mkono wa mtoto Baraka," alisisitiza Kamanda.


Mchango wa CRDB

Wakati huo huo, Lucy Lyatuu anaripoti kuwa katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Benki ya CRDB ilikabidhi hundi ya Sh milioni 20 kwa mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda kwa ajili ya mapambano dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk Charles Kimei alikabidhi hundi hizo jana ambapo Sh milioni 10 zilitolewa kupitia akaunti ya Malkia. Akizungumza, Dk Kimei alisema benki hiyo inatambua mchango mkubwa ambao amekuwa akiuonesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kupigania haki na uhai wa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, huku akipinga mauaji yanayowakumba.

"Kutokana na hali hiyo, tunamkabidhi mke wake kiasi hiki cha fedha ili kisadie mapambano dhidi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini," alisema Dk Kimei na kuongeza kuwa akaunti ya Malkia imeona umuhimu wa kulinda uhai wa kundi hilo, ambalo linatokana na uzao wa matumbo ya wanawake.

Alisema katika fedha hizo, akaunti ya Malkia ambayo kwa kiwango kikubwa ni kwa ajili ya wanawake, imetoa Sh milioni 10 huku benki ikiona umuhimu wa mapambano hayo na kuongeza kiwango kingine cha Sh milioni 10 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya mapambano hayo.

Kuhusu Siku ya Wanawake, Dk Kimei alisema ili mwanamke aweze kufanikiwa ni lazima yeye mwenyewe kuwa na utayari wa kujiwezesha kwa kujiongezea elimu, kupata mafunzo mapya na vilevile kuchangamkia fursa mbalimbali zipatikanazo.

Tunu alisema ni wazi kuwa juhudi za kumkomboa mwanamke, hazitafanikiwa kama hawatapata ukombozi wa kiuchumi. "Wanawake wengi wanashindwa kupiga hatua katika maisha yao kutokana na kuwa ni wategemezi kiuchumi na mara nyingi pia wanakandamizwa ili wasichukue hatua za kujikomboa," alisema Pinda.

Kikwete na viongozi wa albino Alhamisi wiki iliyopita, 

Rais Jakaya Kikwete alikutana na viongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest Kimaya, Ikulu jijini Dar es Salaam. Katika kikao hicho, Rais Kikwete alisema Serikali ya Tanzania inasikitishwa na kufedheheshwa namauaji ya albino nchini na itafanya kila linalowezekana kukomesha mauaji hayo.

"Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo" alisema Rais.

Katika kikao hicho, viongozi hao waalbino nchini walisoma risala ambayo ilitoa kilio chao na mapendekezo yao kwa serikali na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda Kamati ya Pamoja, ambayo itajumuisha Serikali, viongozi wa watu wenye albino, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu na mkakati wa pamoja, ambao hatimaye mauaji hayo kukomeshwa nchini.

Rais alisema Kamati ya Pamoja inatarajiwa kukamilika wiki hii na alisisitiza kuwa kamati hiyo ya pamoja, itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya watu wenye albino.

Aidha, katika hotuba yake kwa Taifa ya mwisho wa mwezi Februari mwaka huu, Rais Kikwete alisema anaungana na Chama cha Albino Tanzania, kulaani ukatili dhidi ya albino na kutaka watu wote wanaojihusisha na ukatili huo wasakwe, wakamatwe, wafikishwe mahakamani na kupewa adhabu kali.

MWAKYEMBE ATAJWA KASHFA TRL

Kuna kila dalili kwamba uhamisho wa Waziri Dk. Harrison Mwakyembe kutoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki, akibadilishana nafasi na Samuel Sitta, ni sehemu ya kumwepusha na kadhia ya kashfaya mabehewa feki ambayo hadi sasa imegundulika kuwa ni kashfa nyingine inayoitafuna Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Uchunguzi huru umegundua kuwa hatua ambazo zilianza kuchukuliwa na Sitta katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA), nako TRL zimeanza kutikisa baada ya kubainika kwamba mabehewa ambayo yaliingizwa nchini kutoka China na kupokelewa na Dk. Mwakyembe kwa mbwembwe zote kisha kubainika hayana viwango, wakubwa wa kampuni hiyo walijua hilo, lakini wakafunika kombe kwa kuwa wakubwa walipeana zabuni kwa njia ya kujuana.

Habari zinasema kamati iliyoundwana Sitta kuchunguza kashfa ya uingizaji mabehewa hayo kutoka India, tayari imeibua mambo mazito ambayo yanaongeza orodha ya kashfa za ulaji na ufujaji wa fedha za umma uliosimamiwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakitumia madaraka yao vibaya.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka TRL, uingizaji wa mabehewa hayo ulifanywa na Kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited ya India kwa kushirikiana na mfanyabiashara mmoja nchini ambaye kwa miaka mingi amehusika katika kadhia nyingi za kujipatia fedha kwa mikataba laghai dhidi ya serikali na mashirika yake.

Vyanzo vyetu ndani ya TRL vinasema kuwa kamati iliyoundwa kuchunguza kashfa hiyo ya ufisadi wa mabilioni ya fedha, inatarajia kukamilisha taarifa yake ya uchunguzi hivi karibuni na kuikabidhi kwa Waziri Sitta, lakini tayari imegundua madudu mengi ikiwamo wakubwa kupokea mabehewa yenye hitilafu wakati wakijua.

Waziri Sitta amesema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia jambo lolote hadi atakapokabidhiwa ripoti ya uchunguzi. "Suala la mabehewa feki nimelikutana kuna tume (kamati) iliundwa kuchunguza na inatarajia kukamilisha ripoti yake hivi karibini, nadhani kwa sasa tungevuta subira ila niwahakikishie wananchi sitaogopa kuchukua hatua bila kujali kashfa hiyo inamhusu mtu au kiongozi wa namna gani," alisema. Kashfa ya uingizaji wa mabewa feki iligundulika mwishoni mwa mwaka jana, ikidaiwa kuwa kuna ufisadi mkubwa umefanyika ndani ya TRL katika utoaji wa zabuniya ununuzi wa mabehewa mapya.

Baadhi ya mafundi wa TRL wanasema kuwa mabehewa hayo ni mabovu na hayaendani na vipimo vya reli ya kati.Udhaifu wa mabehewa hayo uligundulika baada ya kufanyiwa majaribio, kufuatia mengi ya yale mapya 25 aliyopokea Dk. Mwakyembe kupata ajali katika mazingira ya kutatanisha, huku ikidaiwa kuwa hayana 'stability' yakiwa juu ya reli.

"Unajua hata yale ya mizigo mengi yalianguka sana. Sasa ikaonekana hebu na haya ya abiria yachekiwe vizuri, nakuambia matokeo yake ni balaa kama yangeachwa kusafirisha abiria. Ingekuwa ni kilio nchi nzima," alisema mtaalam mmoja wa masuala ya reli kwa sharti la kutokutajwa jina gazetini.

Mabehewa hayo tangu yapokelewe takribani miezi tisa sasa, hayajawahi kusafirisha abiria. Mtaalam huyo aliongeza kuwa kilichofanyika ni uongozi wa TRL wakishirikiana na wakubwa wizarani kuengua jopo la mafundi wa TRL na kuingiza mabehewa hayo kwa kuwa tayari wakubwa walikuwa na mtu wao katika tenda hiyo.

Dk. Mwakyembe alizindua mabehewa mapya 25 ya kubebea kokoto aina ya 'Ballist Hopper Bogie' (BHB), kutoka kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industrial Limited yenye thamani ya Sh. bilioni 4.316 kwa ajili ya uimarishaji wa Reli ya Kati.

Upokeaji wa mabehewa ya mizigo ulifuatiwa na tukio jingi la kushuhudia upokeaji wa mabehewa mengine ya abiria Julai 24, mwaka jana Dk. Mwakyembe akiwa mmoja wa mashuhuda.

Alipoulizwa na NIPASHE kwa njia yasimu jana kuhusiana na kashfa ya mabehewa feki TRL, Mwakyembe alisema: "Hivi sasa niko nje ya nchi... vyombo vya habari vimesharipoti sana suala hili. Watu tayari walishachukuliwa hatua, inawezekana wewe (mwandishi) hujui, wenzako wameandika sana kuhusu suala hili, na watu walishachukuliwa hatua."

Katika hafla ya upokeaji na ushushaji wa mabehewa hayo katikaBandari ya Dar es Salaam, Dk. Mwakyembe alisema ununuzi wake ni sehemu ya utekelezaji wa makakati wa 'Matokeo Makubwa Sasa' (BRN), ambao umelenga kuhakikisha usafirishaji wa reli unaimarika kwa ajili ya kuhimili usafirishaji wa abiria na mizigo, hivyo kusaidia utunzaji wa barabara za lami zinazojengwa kila kona nchini kwa sasa.

Vyanzo vya habari kutoka TRL vinasema kuwa uhamisho wa Dk. Mwakyembe kutoka Uchukuzi, ni mkakati wa kumwepusha na kadhia yoyote ambayo inaweza kulipuka wakati wowote kutokana na zabuni hiyo ambayo inaonekana kama aina nyingine wa wizi wa wazi.

Mbali na Dk. Mwakyembe, menejimenti ya TRL nayo iko kikaangoni tangu Sitta aunde kamatiya kuchunguza kashfa hiyo.


CHANZO: NIPASHE

MIPANGO YA KUMDHURU DK. SLAA YAFICHUKA

Mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Khalid Kangezi, anahojiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa tuhuma za kushiriki katika mipango ya kukihujumu chama hicho na kutaka kumdhuru Dk. Slaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Camillius Wambura, alithibitisha jana Kangezi kufikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay na kwamba, hadi jana jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa.

Taarifa za awali zilizotolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar esSalaam jana, zilieleza kuwa Kangezi amekuwa akitumiwa na maofisa 22 wa vyombo vya usalama katika miaka miwili iliyopita kufanya mipango hiyo dhidi ya chama hicho.

Alidai Kangezi amekuwa akitumiwa na maofisa usalama wa vyombo hivyo kupata taarifa nyingi za Chadema na kuwasilishwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Marando alidai mipango hiyo imegunduliwa na kitengo cha usalama cha Chadema kupitia simu za Kangezi na kwamba, ililenga kuiumiza Chadema kisiasa. Alidai katika hujuma hizo, Kangezi amekuwa akiwasiliana na mmoja wavigogo wa ngazi ya taifa wa CCM.

Marando alidai kuanzia Desemba, mwaka jana hadi wiki iliyopita, Kangezi alikuwa amekwishafadhiliwa Sh. milioni saba kwa ajili ya matumizi ya mawasiliano ya simu kufanikisha upatikanaji wa taarifa za Chadema kupitia vikao vyake mbalimbali, ikiwamo kamati kuu.

Alidai alipohojiwa na chama, Kangezi aliwapa kitabu chake cha kutunza kumbukumbu, ambacho kinaonyesha mawasiliano kati yake na baadhi ya maofisa wa vyombo vya usalama, aliowataja kwa majina na namba za simu zao za mikononi.

"Huyu kijana ilibidi atuandikie statement (andishi) kwa mkono wake mwenyewe. Na pamoja na mambo mengine juu ya mheshimiwa (kigogo wa CCM-anamtaja jina). 'Mzee (anamtaja jina) mwenye simu namba (anaitaja) mimi nilimpigia mara tatu, amenitumia fedha za vocha mara mbili kiasi cha Sh. 50,000 siku ya Jumatatu tarehe 14/7/2014 na pia 150,000 tarehe 4 Desemba, 2014 siku ya Alhamisi kwa madhumuni ya kunishawishi kumpatia taarifa za siri za chama napia kumpigia simu katika vikao mbalimbali," alidai Marando.

Alidai kuwa wataalamu wa Chademawamefanikiwa kuingia katika simu mbili zinazomilikiwa na Kangezi na kugundua mawasiliano aliyoongea kwa zaidi ya saa mbili au tatu katika siku, ambazo rekodi zinaonyesha kuwa zilikuwa ni za vikao vya chama.Marando alidai wataalamu hao waligundua kuwa aliyekuwa akipigiwa simu na Kangezi kumpa taarifa za chama ni mmoja wa vigogo wa moja ya vyombo vya usalama katika wilaya ya Kinondoni,jijini Dar es Salaam.

Alidai kigogo huyo wa usalama alionekana kuwa na mawasiliano ya karibu na vigogo wawili CCM ngazi ya taifa. "Sasa kilichotushtua zaidi, huyu kijana ametuambia katika hili andishi lake kwamba, katika siku za karibuni amekuwa akielekezwa hatauwezekano wa kutoa maisha ya Katibu Mkuu wa chama chetu, Dk. Willibrod Slaa," alidai Marando.

Kutokana na hali hiyo, Marando alilaani suala hilo na kusema chamakilitarajia kumpeleka Kangezi polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Alipoulizwa jana na NIPASHE, Kamanda Wambura alisema Kangezialifikishwa katika kituo cha polisi Oysterbay saa 8.14 mchana na kwamba, muda huo watu waliompeleka walikuwa wakiendelea kuandika maelezo kituoni.Alisema Kangezi alipelekwa katika kituo hicho cha polisi na mmoja wa mawakili wa Chadema.

Kangezi alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia tuhuma hizo, hakupatikana na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.

Hadi tunakwenda mitamboni,Wambura alisema Kangezi alikuwa akiendelea kuhojiwa katika kituo hicho.


CHANZO: NIPASHE

WATOTO 17 WAKUTWA KATIKA NYUMBA YA MFANYABIASHARA MJINI MOSHI

Hali ya taharuki imetanda katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha baada ya kugundulika mahali walipofichwa watoto17 wakiwamo watatu wa familia moja wanaodaiwa kupotea tangu mwezi Februari mwaka jana kwa madai ya kufundishwa maadili ya imani ya dini ya kiislamu.
Umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Moshi wamejitokeza katika kata ya pasua mjini Moshi kushuhudia tukio la watoto hao wenye umri wa kuanzia miaka miwili hadi 13 ambao walikuwa wanaishi kwa Bw.Abdelnasir Abrahamani ambaye ni mfanyabiashara wa nguo nchini Kenya.

Akizungumza katika eneo la tukio mkuu wa wilaya ya Moshi Bw.Novatus Makunga amesema tatizo hilo kwa mji wa Moshi ni kubwa na kwamba kwa sasa nyumba hiyo imefungwa na kuondolewa watoto hao ili warejeshwe kwa wazazi hao wakati hatua za kisheria zikiendelea.

Mmoja wa wazazi mwenye watoto watatu waliopotea tangu mwezi February mwaka jana na kukutwa katika nyumba hiyo Bw.Ramadhani Mohamedi amesema aligundua tukio hilo baada ya kukutana na mtoto wake wa kike barabarani na kumweleza mateso wanayoyapata huko.

Naye mfanyabiashara huyo Bw.Abdulinasir Abrahamani amesema nyumba hiyo ni familia na ndugu zao wa kiislamu lakini siyo kituo cha yatima, ila ni sehemu ya kutolea mafundisho ya dini ya kiislamu.

KAGAME AMFURAHIA JK

Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kuhudhuria mkutano wa tisa wa nchi zilizoungana kutekeleza Miradi ya Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, akisema ni hatua muhimu katika kufungua utekelezaji wa miradi ya miundombinu katika kanda nyingine za EAC.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana ilisema kuwa Rais Kikwete alihudhuria kikao hicho kwa mwaliko wa Rais Kagame na kwamba mkutano huo ulifanyika kwenye Hoteli ya Serena mjini Kigali.
Naye Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete ameweza kuhudhuria mkutano wa jana kwa sababu sasa njia imefunguka kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central Corridor unaokatisha katikati ya Tanzania.
Marais Kagame na Kenyatta walikuwa wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika zaidi ya saa mbili baada ya Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda. Mbali na nchi hizo, Burundi na Sudan Kusini pia zilialikwa kwenye mkutano huo kujadili hatua za utekelezaji wa miradi mbalimbali kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa nane uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana Marais hao wawili wamekuwa wakitofautiana katika suala la waasi wa Rwanda baada ya Rais Kikwete kumshauri Kagame kukaa meza moja na waasi wa Rwanda ili kumaliza tofauti zao zinazosababisha maisha ya watu kupotea.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa Rwanda wakati akizungumza katika kikao cha Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika mapema mwaka jana mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambao ulikuwa ukijadili suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Ukanda wa Maziwa Makuu.
Ushauri huo pia uliwagusa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila (DRC), ambao aliwataka kufanya mazungumzo na waasi wanaopingana na Serikali zao. Akizungumza katika hotuba yake ya kila mwezi Rais Kikwete alisema: “Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa, kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike.
Rwanda imekuwa ikiituhumu Tanzania kuwa inashirikiana na waasi hao na mara kadhaa magazeti ya nchi hiyo yameripoti taarifa kuwa viongozi wa waasi wa nchi hiyo wamekuwa wakija nchini.


Chanzo: Mwananchi

CHINJA CHINJA MOHAMMED EMWAZI ALIZUILIWA KUINGIA TANZANIA


Mohammed Emwazi ,mtu ambaye alibadilika na kuwa ''chinja chinja'' wa kundi la islamic state kwa jina 'jihad John' Mohammed Emwazi, alifurushwa kutoka nchini Tanzania kwa kuwa mlevi na mtu anayetoa matusi.,afisa moja wa polisi ameiambia BBC.

Emwazi anasema alitishiwa na kuhojiwa chini ya maagizo ya shirika la upelelezi la Uingereza MI5 alipoenda nchini humo mwaka 2009.

Lakini BBC imeonyeshwa rekodi za kuzuiliwa kwake tangu alipokamatwa.
Afisa huyo amesema kuwa Emwazi hakuruhusiwa kuingia nchini Tanzania kwa sababu alikuwa amezua mgogoro katika uwanja wa ndege na kuwa na tabia za mlevi.
Emwazi ambaye ana zaidi ya miaka 20 na ambaye anatoka magharibi mwa London ametambuliwa kama mtu aliyeziba uso katika kanda kadhaa za video ambapo mateka wamechinjwa.
Emwazi amesema kuwa alikuwa mwanafunzi ambaye alikuwa katika likizo ya safari wakati aliposafiri na kuingia Afrika mashariki kupitia uwanja wa ndege wa Dar-e-salaam kutoka nchini Uholanzi miaka sita iliopita.

WAGANGA 32 WATIWA MBARONI

Waganga 32 wakiwa na vifaa vya kupigia ramli chonganishi inayochochea mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi wamekamatwa katika operesheni iliyofanyika jana na juzi mkoani Geita.

Waganga hao pamoja na wengine walitiwa mbaroni baada ya kuwekewa mtego na makachero wa polisi waliojifanya wachimba madini.

Baadhi ya zana zilizokamatwa katika msako huo ni pamoja mnyama aina ya Kakakuona, ngozi za wanyama kama Chui, Fisi, nyoka waliokaushwa na sarafu zinazotumika kupima ubora wa viungo vya albino ambavyo ndani yake hupachikwa sumaku ndogo ili kuwarubuni wateja.

Taarifa zinasema kuwa mkoa wa Geita unakadiriwa kuwa waganga 3,000 huku wilaya ya Geita pekee ikikadiriwa kuwa na waganga 900.

Hatua hiyo inatokana na Jaji aliyetoa hukumu jana aliyehoji kutofikishwa mahakamani waganga wa kienyeji na wanunuzi wa viungo.

Pia, msako huo ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete.

ALBINO WAZUA TIMBWILI IKULU

Vurugu zilizofanywa na baadhi ya walemavu wa ngozi Albino katika Ikulu ya Tanzania zimesababisha kuahirishwa kwa kikao kati ya viongozi wao na Rais Jakaya Kikwete.

Rais Kikwete alikuwa akitarajiwa kufanya mkutano na viongozi wa Albino Tanzania TAS aliowaalika kuzungumzia hoja zao kutokana na mauaji ya walemavu hao yanayoendelea nchini.

Lakini heka heka iliyotokea katika eneo la mapokezi iliwalazimu maafisa wa Ikulu kuwatawanya walemavu hao.

Ni muda mfupi baada ya ukaguzi kuanza kufanyika katika moja ya lango la kuingilia Ikulu, kundi moja la walemavu hao waliokuwa katika moja ya chumba wakaanzisha malalamiko kwa sauti huku viongozi wao wakiwa wanajiandaa kuruhusiwa na kuingia ndani.

Kelele hizo na mabishano hayo miongoni mwa walemavu hao kwa mbali ikaanza kuonekana ni dosari namba moja hasa baada ya kupandisha mori na kila mtu kuanza kusema lake kupinga ushiriki wa viongozi hao.

Kutokana na vurugu hizo maafisa wa Ikulu waliwatawanya Walemavu hao kutoka nje ya Geti, na hapo ikawa mwanzo wa sakata jipya baada ya kuanza kulumbana na viongozi wao na hatimaye kuanza kupigana na mambo yakawa hivi.

Baada ya kutulizwa ugomvi kilichofuata ni nyimbo za kupinga uhalali wa viongozi waoHata hivyi vurugu hizi zinatazamwa tofauti na baadhi ya walemavu hao, ambao wanasema ni vurugu hizo zimepoteza fursa ya kuwasilisha matatizo yao kwa Rais.

DEWJI KIJANA TAJIRI ZAIDI AFRIKA

Mfanyabiashara maarufu nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji kwa mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29, akiwa tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.

Jarida la Forbes la Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri wa Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34 trilioni) unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni yake ya Mohammed Enterprises (Metl Group).

"Dewji alibadilisha biashara aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na viwanda vya Metl," inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo Mtanzania.

"Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti," inaongeza ripoti hiyo.

Metl ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.

Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Kwa mujibu wa tovuti yake, Metl inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Pia inahusika na huduma za simu,fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Dewji anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa CCM na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa nafasi ya mwisho.

Rostam amefungana nafasi ya 26 na mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na Femi Otedola wenye utajiri wa Sh1.8 trilioni kila mmoja.

Orodha hiyo ya 29 bora inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na utajiri wa Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango ambacho ni mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2014/15.

Forbes linamtaja Rostam kuwa na utajiri wenye thamani ya Dola 1 bilioni za Marekani (Sh1.8 trilioni), kiwango ambacho kimebaki pasi na mabadiliko kutoka orodha ya mwaka jana. Rostam anamiliki asilimia 35 ya hisa katika kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom.

MAUFI AHUKUMIWA JELA MIAKA MITANO KWA KUUA BILA KUKUSUDIA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga imemhukumu aliyekuwa Katibu wa Mwenezi na Itikadi wa CCM Mkoa wa Rukwa, Patrick Maufi (48) kifungo cha miaka mitano jela kwa kumuua mpenzi wake bila kukusudia kwa wivu wa kimapenzi.

Alikutwa na hatia ya kumuua Ntuli Mwakibinga (40) ambaye alikuwa mhudumu wa afya katika Hospitali ya Mkoa, Mjini Sumbawanga.

Mshitakiwa alitiwa hatiani kwa kumuua mpenzi wake huyo mwaka 2011.

Mwanasheria wa Serikali, Fadhil Mwandoroma alimweleza Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kakusulo Sambo kuwa usiku wa manane wa Septemba 5, 2011 mshitakiwa alimuua mpenzi wake katika eneo la Kristu Mfalme mjini hapa.

Upande wa mashtaka uliita mahakamani mashahidi wanne ambao hawakuweza kutoa ushahidi wao baada ya mshitakiwa kukiri kosa. Mwanasheria wa Maufi, Boniventura Chambi aliomba mahakama hiyo isitoe adhabu kali dhidi ya mteja wake.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, usiku huo wa tukio, mshitakiwa alimpiga na kumjeruhi vibaya mpenzi wake huyo sehemu mbalimbali za mwili, ikiwa ni pamoja na kumnyofoa nywele zake na kumsababishia kifo. Uchunguzi wa kitabibu ulibaini Ntuli alivuja damu nyingi kwenye ubongo na shingo ilivunjika.

Mshitakiwa katika utetezi wake, alidai mkewe wa ndoa alifariki dunia 2010 na kumwachia mzigo mkubwa wa kulelea watoto watano. Alidai watoto wanne ni wa marehemu mkewe na mwingine ni ndugu ambao wote wanamtegemea.

Alidai alishakaa rumande miezi 22 kabla ya kupewa dhamana baada ya shitaka lake la kuua kubadilishwa kuwa la kuua bila kukusudia.

Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, alisema baada ya kuzingatia utetezi wa mshitakiwa inawezekana kweli ameachiwa mzigo mkubwa wa watoto wanaomtegemea, lakini pia kwa upande mwingine, marehemu pia alikuwa akitegemewa na taifa kitaaluma, rafiki na familia yake.

Chanzo: Habari leo

MABINTI 12 WAKAMATWA KWA UNGA NDANI YA SIKU 30

Licha ya kampeni kubwa ya kupambana na kuzuia usafirishaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini, bado Watanzania wameendelea kufanya biashara hiyo na katika kipindi cha siku 30 mabinti 12 wamekamatwa wakisafirisha dawa hizo ndani na nje ya nchi.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Kamishna wa Kikosi cha Kupamba na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliokamatwa katika kipindi hicho ni mabinti wenye umri mdogo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mabinti wanane wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Hong Kong na wanne katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Kamishna Nzowa alisema ingawa vyombo vya habari na wafungwa walioko Hong Kong wamejaribu kuwashauri Watanzania wasifanye biashara hiyo, bado wamekuwa na 'shingo ngumu.'

Alisema Januari 23, wanawake wawili, Rehema Ndunguru (31) na Moyo Ramadhani (31) walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wakisafirisha dawa hizo kwenda Hong Kong.

"Rehema alikuwa amemeza pipi 78 ambazo ni sawa na kilo 1.2 na Moyo alitoa pipi 86 sawa na kilo 1.5," alisema Kamanda Nzowa.

Alisema Februari 12, mwaka huu alikamatwa mwanamke mwingine Munira Mohamed (27) akiwa amemeza pipi zenye uzito sawa na kilo 1.

Februari 9, mwaka Halmati Tango (21) alikamatwa akiwa na pipi 76 zenye uzito sawa na kilo 1.3.

Nzowa alisema Halmat alikuwa akisafirisha dawa hizo kwenda Nigeria wakati Munira alikuwa akizipeleka Mombasa.


Hong Kong

Wakati huo huo, Padri John Wotherspon aliyekuwa nchini kwa ajili ya kampeni ya kuwazuia vijana wa Kitanzania kusafirisha dawa za kulevya amelieleza Mwananchi kuwa wanawake wanane wa Kitanzania pia wamekamatwa katika uwanja wa ndege wa Hong Kong katika kipindi hicho hicho.

Padri Wotherspon alisema baadhi ya wanawake hao wamekiri kusikia na kuona barua za wafungwa wa China zilizoonya kuhusu biashara hiyo lakini wakachukua uamuzi wa kuzibeba. Kati ya wanawake hao wanane, mmoja alikuwa amemeza kete 135 za dawa za kulevya aina yaheroin na mwingine alikuwa amemeza kete 86.

"Kwangu mimi vita inazaa matunda, tunapowakamata ina maana tunazuia," Nzowa. kusambazwa kwa mzigo," alisema.


Chanzo: Mwananchi